MakalaSiasa

JAMVI: BBI itakuwa msumari wa mwisho kwa jeneza la Jubilee

September 8th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Ripoti ya Jopokazi la Maridhiano, maarufu kama BBI, huenda ikawa msumari wa mwisho katika jeneza la chama cha Jubilee ambacho kimekumbwa na mgogoro wa ndani kwa ndani, wadadisi wameonya.

Wanasema kujitokeza hadharani kwa Naibu Rais William Ruto kupuuza jopokazi hilo lililoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga baada ya muafaka wao, ni ishara kwamba ripoti yake itazidisha mpasuko katika chama tawala.

Dkt Ruto na washirika wake katika kundi la Tanga Tanga wamekuwa wakikosoa muafaka huo na pendekezo la kura ya maamuzi tofauti na wale wa Kieleweke wanaompiga vita na ambao wameapa kuzima azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wanachama wa Kieleweke wamekuwa wakipigia debe jopokazi hilo na kuunga kura ya maamuzi kubuni wadhifa wa waziri mkuu. Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakipinga kura ya maamuzi inayolenga kubuni nyadhifa zaidi za uongozi.

Wiki jana, Dkt Ruto alipuuza kamati hiyo iliyokusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu marekebisho wanayotaka yatekelezwe kuimarisha uwiano nchini akisema inapotezea wananchi wakati.

Kulingana na Dkt Ruto, BBI haikuwa na haja ya kuzunguka nchini kutafuta maoni ya wananchi, na badala yake ingepata tu maoni ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuhusu namna ya kuzuia ghasia kila baada ya uchaguzi kwa kuwa yeye ndiye amekuwa akipinga matokeo ya kura.

Wadadisi wanasema kauli hiyo ya Dkt Ruto inaashiria kwamba atapinga vikali ripoti ya BBI inayotarajiwa wakati wowote na kuzidisha mgawanyiko katika chama tawala.

“Kwa kukosoa jopokazi ambalo Rais Kenyatta alihusika kuunda ni kuonyesha kuwa hayuko tayari kukubaliana na ripoti yake iwapo itatoa mapendekezo ya kubadilisha muundo wa serikali. Hii inaweza kuvunja Jubilee kabisa. Kumbuka chama hicho kimegawanyika huku Dkt Ruto na washirika wakilaumiana na wale wa Rais Kenyatta kuhusu kila kitu,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Dkt Ruto na wandani wake wanahisi kwamba BBI inatumia rasilimali za serikali kutimiza malengo ya kuzima azima yake, kumaanisha kuwa hawatambui na hawatatambua mapendekezo yake.

“Kwa msingi huu pekee, kinachoweza kutarajiwa ni mvutano zaidi ndani ya chama cha Jubilee wandani wa Dkt Ruto wakikataa mapendekezo ya jopokazi hilo. Kwao, halikufaa kubuniwa na halina maana kwa sababu wanahisi linanuiwa kummaliza naibu rais kisiasa,” aeleza Bw Kamwanah.

Wadadisi wanasema uwezekano wa ripoti ya BBI kupendekeza kura ya maamuzi, ndio unaomkera Dkt Ruto ambaye amekuwa akidai pendekezo hilo linalenga kunufaisha watu au jamii chache.

“Kauli hii inalenga wanachama wa kundi la Kieleweke ambao wamekuwa wakiunga mkono maridhiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga na hii imekuwa ikimwasha Dkt Ruto na wandani wake. Wanahisi kwamba Bw Odinga amezua msukosuko katika chama cha Jubilee kwa lengo la kumwekea Ruto vikwazo, madai ambayo Rais Kenyatta mwenyewe amekanusha akisema muafaka wao haukuhusu uchaguzi wa 2022,” asema mdadisi wa siasa, Peter Wafula.

Anasema ishara kwamba ripoti ya kamati hiyo itazamisha chama cha Jubilee ni hatua ya wandani wa Dkt Ruto ya kuunga mswada wa kura ya maamuzi wa Punguza Mizigo ambao unapendekezwa na chama cha Third Way Alliance.

“Ikiwa kutakuwa na kura ya maamuzi kutokana na mapendekezo ya BBI, kutakuwa na kivumbi katika chama cha Jubilee, Dkt Ruto na washirika wake wakiyapinga. Sio kwa sababu mapendekezo hayo yatakuwa mabaya, yanaweza kuwa mazuri kwa nchi, lakini watayapinga kwa sababu Bw Odinga na Wanakieleweke watayaunga mkono,” asema Bw Wafula.

Anatoa mfano wa bunge la kaunti ya nyumbani ya Bw Odinga ya Siaya kukataa mswada wa Punguza Mizigo huku bunge la kaunti ya nyumbani ya Dkt Ruto ya Uasin Gishu ikipitisha mswada huo.

Kulingana na wandani wa Dkt Ruto, BBI inatumiwa kusambaratisha ndoto yake ya kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na hawawezi kuunga mapendekezo.

Wadadisi wanasema Dkt Ruto anahisi kuwa hakushirikishwa kwenye BBI licha ya kuwa nguzo muhimu katika serikali ya Jubilee na siasa za humu nchini.

Wandani wake wamekosoa kamati hiyo wakidai kwamba inalenga kutimiza maslahi ya watu wachache wanaotaka kutenga jamii nyingine.

“Kwa chama ambacho kimekumbwa na migogoro ya ndani kwa ndani na madai ya usaliti kama Jubilee, ripoti ya BBI inaweza kukivunja kabisa ikizingatiwa tangu mwanzo, Dkt Ruto ambaye ni mshirika mkuu katika chama hicho hakuchangamkia muafaka uliozaa jopokazi hilo,” asema Bw Kamwanah.