JAMVI: Bunge linavyotishia kuongeza masaibu ya mswada wa BBI

JAMVI: Bunge linavyotishia kuongeza masaibu ya mswada wa BBI

Na LEONARD ONYANGO

MASAIBU yanayokumba Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) huenda yakaongezeka iwapo wabunge na maseneta wataafikiana kuondoa makosa yaliyobainishwa katika mswada huo.

Wanasheria na wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa iwapo wabunge na maseneta watarekebisha Mswada wa BBI, hatua hiyo itapingwa vikali mahakamani hivyo kuchelewesha kura ya maamuzi iliyopangwa kufanyika kabla ya Agosti, mwaka huu.

Tayari, kuna kesi 11 za kupinga BBI mahakamani; na wakili Bobby Mkangi – ambaye alikuwa miongoni mwa wataalamu walioandika Katiba ya 2010 – anasema kuwa huenda kesi zaidi zikawasilishwa kortini baada ya Bunge kupitisha mswada huo.

Kesi 11 zimewasilishwa katika Mahakama Kuu na walalamishi mbalimbali, akiwemo mwanauchumi David Ndii na chama cha Thirdway Alliance.Bw Mkangi anasema kuwa tayari kuna dosari tele ambazo zimejitokeza ambazo huenda zikasababisha makundi mbalimbali ya watu na mashirika kuenda mahakamani kupinga uhalali wa Mswada wa BBI.

“Tayari tumeelezwa kuwa miswada inayojadiliwa katika Seneti na Bunge la Kitaifa haifanani. Maseneta na wabunge wanastahili kujadili mswada mmoja wala si miswada miwili tofauti.

“Kwa sababu maseneta na wabunge wanajadili miswada miwili tofauti, kuna uwezekano baadhi ya watu wanangojea kuenda mahakamani kutaka BBI ibatilishwe,” anasema Bw Mkangi.

Wabunge na maseneta wataendelea kujadili Mswada wa BBI Jumanne baada ya kushindwa kuafikiana wiki iliyopita iwapo wanafaa kuufanyia marekebisho au la.

Japo wabunge wameonyesha dalili kuwa huenda wakapitisha mswada huo jinsi ulivyo, maseneta wameshikilia kuwa ni sharti waufanyie marekebisho kuondoa makosa.

Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Bunge kuhusu Hali na Sheria (JLAC) Okongo Omogeni (Seneta wa Nyamira) alipendekeza kuwa maseneta warekebishe makosa yaliyobainishwa katika Mswada wa BBI.

Kwa mujibu wa Bw Omogeni, hatua hiyo itasaidia kuliondolea aibu Bunge.Licha ya kuonekana kuunga mkono, wabunge pia wamemtwika Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi mzigo wa maswali ambayo anafaa kuyafanyia uamuzi watakaporejelea vikao kuanzia Jumanne.

Wabunge wanataka kujua ikiwa mapendekezo yalitolewa na wananchi mbele ya kamati yanafaa kupuuzwa au la.“Kulikuwa na haja gani kuwasilisha maoni ya umma kwa kamati ya bunge? Tunafaa kuyapuuza au kuyatumia kwenye mjadala au kupiga kura?” akauliza mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale.

Mbunge wa Ugenya David Ochieng pia alitaka kujua ikiwa BBI ni mradi wa serikali au ulianzishwa na Wakenya.

You can share this post!

Hatua ya Waiguru kutimua madaktari yamtatiza

Inter Milan washinda taji la Serie A kwa mara ya kwanza...