JAMVI: Changamoto tele kwa Kenyatta akijaribu kuzima ndoto ya Ruto

JAMVI: Changamoto tele kwa Kenyatta akijaribu kuzima ndoto ya Ruto

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amejipata katika njia panda katika juhudi zake za kujenga muungano mkubwa wa kisiasa utakaozima ndoto za Naibu wake, William Ruto, kuingia Ikulu 2022.

Japo amepanua muungano wa viongozi saba wa vyama vikuu vya kisiasa wanaounga mkono mchakato wa BBI kwa kujumuisha Gavana wa Machakos Alfred Mutua, angali na kibarua cha kusuka umoja kati yao.

Hii, wadadisi wanasema, ni kutokana na tofauti ambazo ziliibuka juzi miongoni mwa viongozi hao, haswa waliokuwa vigogo wenza katika muungano wa upinzani, Nasa.

Wao ni Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya).Tofauti hizo ziliibuka majuma kadha yaliyopita pale Bw Odinga alipokataa kuidhinisha mmoja kati ya vigogo ya hao watatu kwa wadhifa wa urais 2022.

Kenya Moja

Baada ya kumrushia Bw Odinga maneno makali, watatu hao kwa ushirikiano na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi sasa wanaendeleza juhudi za kubuni muungano mwingine kwa jina “One Kenya” (Kenya Moja).

Chini ya mwavuli wa muungano huo, watatu hao waliamua kushirikiana katika chaguzi ndogo za maeneo bunge ya Kabuchai, Matunga na useneta wa Machakos kwa kuunga mgombeaji mmoja.

Ushindi wa mgombeaji wa ANC katika eneo bunge la Matungu, mgombeaji wa Ford Kenya katika eneo bunge la Kabuchai na mgombeaji wa Wiper, Agnes Kavindu katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Machakos umewapa motisha washirika hao wa vuguvugu hilo jipya.Wameingiwa na matumaini kwamba mshikamano kati yao pia utawawezesha mmoja wao kuingia Ikulu 2022.

“Msisimko kutoka na kile kinachoonekana kama ushindi wa muungano wa ‘One Kenya’ katika chaguzi za Matungu, Kabuchai na Machakos utapanua zaidi ufa kati yao na mrengo wa Bw Odinga. Na bila shaka hali kama hii itahujumu juhudi za Rais Kenyatta kuwaleta wanasiasa hawa pamoja kwa lengo la kumwangusha Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao,” anasema Martin Andati ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Hii ndio maana juzi Rais Kenyatta alikutana, kwa njia ya mtandao, na viongozi saba wa vyamba vikuu vya kisiasa nchini, akiwemo Dkt Mutua na kuwataka kukomesha vita miongoni mwao.

Mtazamo wa Bw Andati unashabihiana na wake Bw Dismas Mokua ambaye anaongeza kuwa mvutano kati ya ODM na Katibu katika Wizara ya Usalama Karanja Kibicho kuhusu urithi wa urais na usimamizi wa mpango wa marekebisho ya Katiba kupitia BBI, pia huenda ukahujumu mipango ya Rais Kenyatta.

“Rais Kenyatta anafaa kusuluhisha mvutano kati ya Raila na Kibicho kuhusu udhibiti wa mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia BBI na urithi wake, ili afaulu katika mipango yake ya kuhakikisha kuwa mwanasiasa anayetaka ndiye ataingia Ikulu, 2022,” anasema Bw Mokua.

Juzi, ODM ilimtaka Rais Kenyatta kumwondoa Dkt Kibicho kutoka mipango ya kampeni za kuipigia debe Mswada wa BBI ikisema huo ni wajibu wa wanasiasa.Matakwa hayo yalitolewa na Seneta wa Siaya James Orengo na kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa Junet Mohammed.

“Mpango huu ni wa siasa na unapaswa kusimamiwa na wanasiasa wala sio maafisa wa serikali. Rais atoa BBI mikononi mwa afisa mmoja mkuu katika afisi yake ambao wamekuwa wakiihujumu,” Bw Orengo akasema katika halfa moja ya mazishi katika eneo bunge la Rarieda.

Seneta huyo wa Siaya pia alidai kuwa afisa huyo amekuwa akitumia mchakato huo wa BBI kuzima ndoto ya Bw Odinga kuingia Ikulu 2022.Isitoshe, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amedai, bila kutoa ithibati, kuwa Dkt Kibicho ndiye alichangia kushindwa kwa mgombeaji wao, David Were katika uchaguzi mdogo wa Matungu.

Umaarufu wa Raila Magharibi

Bw Sifuna alidai, Katibu huyo wa Wizara alifadhili kampeni za mgombeaji wa ANC Oscar Nabulindo ili “kutoa taaswira kwamba umaarufu wa Raila katika magharibi mwa Kenya umedorora kabisa,”Baada ya kukimya kwa wiki moja hivi, Dkt Kibicho Alhamisi alijibu shutuma za ODM akisema mpango wa marekebisho ya katiba sio “mradi wa mtu mmoja”.

“Katiba ni yetu sote na kama afisa wa serikali nitaendelea na elimu ya umma bila woga wowote. Sitatishwa,” akasema katika Shule ya Upili ya Gacatha katika kaunti ya Kiranyaga.

Kauli hiyo ya Dkt Kibicho ambayo ilionekana kujibu malalamishi ya ODM dhidi yake, inaonyesha wazi kwamba Rais Kenyatta hajatekeleza takwa la wandani wa Bw Odinga kwamba Katibu huyo wa Wizara asiruhusiwe kusimamia kampeni za BBI.

Kulingana na Bw Mokua, ambaye pia ni mtaalamu katika masuala ya uongozi, hali kama huenda ikaathiri muafaka wa kisiasa kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Isitoshe, huo mpango wa Rais Kenyatta wa kuleta pamoja Raila na vinara wengine kama Mudavadi, Kalonzo, Wetang’ula, Charity Ngilu, Seneta Gideon Moi na juzi kiongozi wa Chama cha Maendeleo Chap Chap Alfred Mutua, huenda utakumbwa na matatizo,” anaeleza.

Juzi Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alithibitisha kuwa Rais Kenyatta anapanga kuwatumia viongozi wa kisiasa wanaounga mkono Mswada wa BBI kuunda muungano wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Alisema lengo kuu la kiongozi wa taifa ni kupalilia umoja nchini ili kukomesha ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika chaguzi zilizopita.“Sisi kama Jubilee tunataka miungano inayowaleta Wakenya pamoja. Miungano ambayo italeta amani na ufanisi kimaendeleo nchini,” Bw Tuju akasema.

“Hii ndio maana tumekuwa tukifanya mazungumzo na ODM, Wiper, Ford- Kenya, ANC, Kanu na vyama vingine. Hii ni kwa sababu kimsingi, sote tu Wakenya, dada na ndugu tunaoishi katika taifa hili tulilorithi kutoka kwa mababu zetu,” akaongeza.

Japo Bw Odinga hajatangaza wazi wazi kuwa atagombea urais kwa mara ya tano mwaka ujao, wandani wake wamesisitiza kuwa atakuwa debeni mwaka ujao.

Hii ndio sababu anasemekana kuwa mbioni kusuka muungano mpya unaoshirikisha wanasiasa kama vile Waziri wa zamani Mukhisa Kituyi, Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana, na mwenzake Charity Ngilu (Kitui), miongoni mwa wengine.

You can share this post!

DINI: Usitishwe na wanaokusema vibaya,vumilia, huwezi...

JAMVI: Gumzo la ugombea-wenza Mlima Kenya lilivyo kiazi...