MakalaSiasa

JAMVI: Hakuna dalili za NASA kujifufua tena kwa ajili ya 2022

December 8th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Hakuna dalili zozote za muungano wa NASA kufufuka huku tofauti za vinara wake wanne zikipanuka kila siku uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia.

Kila mmoja wao anaonekana kushikilia msimamo tofauti na wenzake akijiandaa upya kwa uchaguzi ujao.

Vinara hao wamesahau kwamba kuna wafuasi zaidi ya 8 milioni waliowapigia kura kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 na badala yake wamewagawanya kwa misingi ya kimaeneo na hata kikabila.

Kilichobaki kwao ni kurushiana lawama, kuibuka kwa madai ya usaliti na kuumbuana wanapopata nafasi.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye alikuwa mgombea urais wa muungano huo, amezama katika handisheki yake na Rais Uhuru Kenyatta iliyozaa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano maarufu kama BBI.

Chama chake kimekuwa kikilaumu vyama tanzu vya NASA kwa kumuacha alipokuwa akijiapisha kuwa rais wa wananchi na kusema hawafai kulalamika alipotenga vinara wenzake kwenye mazungumzo yake na Rais Kenyatta.

Ingawa ni jinsi handisheki hiyo ilivyoafikiwa kulikowakasirisha vinara wenzake Kalonzo Musyoka wa Wiper, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC) na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya, wadadisi wanasema kwamba hata ripoti ya BBI haiwezi kuwa dawa ya kurejesha muungano wa NASA.

“Ni wazi kuwa ndoa ya kisiasa ya Raila, Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula haiwezi kuokolewa. Pengine iwe chini ya muungano tofauti wa kulazimishwa lakini kulingana na matamshi, vitendo na hisia zao na wandani wao, NASA iliisha na handisheki. Kwa ufupi, Raila aliua NASA na BBI haiwezi kufufua muungano huo,” aeleza mdadisi wa siasa Ben Haraka.

Anasema hatua ya chama cha Mudavadi ya kukataa ripoti ya BBI inaonyesha kuwa makamu rais huyo wa zamani hakubaliani kikamilifu na mkondo wa kisiasa ambao Odinga na chama chake cha ODM walichukua baada ya handisheki.

Mnamo Jumanne, ANC kilisema kuwa hakitaunga BBI kwa sababu haina mapendekezo ya kufufua hali ya uchumi. Bw Mudavadi amekuwa akilalamika kuwa muafaka wa Raila na Uhuru uliua upinzani.

Hayo yalijiri huku akimtaja Bw Odinga kama kiongozi asiyeaminika ambaye alikuwa akilazimisha mambo katika muungano wa NASA na kudharau vinara wenza.

“Yale ambayo Bw Mudavadi amefichua katika kitabu chake Soaring Above The Storm, yanaonyesha kuwa muungano huo ulijawa na usaliti, kutoaminiana na dharau. Ingekuwa balaa kama wangetwaa mamlaka, vinara wangeanza kuvutana na kurushiana lawama kwa kusalitiana,” aeleza Bw Haraka.

Kulingana na Dkt Fred Musila, mdadisi wa siasa na mtaalamu wa masuala ya utawala, yanayojitokeza wakati huu yanaonyesha kuwa NASA ilikuwa kwa jina tu.

“Ni wazi kuwa lengo la Odinga lilikuwa ni kutumia wenzake kushinda urais lakini hakuwa na nia ya kudumisha uhusiano wake na vinara wenza. Kwa sababu aliihitaji kuokoa nyota yake ya kisiasa aliwaacha nje kwenye mazungumzo yake na Uhuru. Kuna kila dalili kwamba mpaka sasa, Musyoka, Musalia na Wetang’ula hawakukumbatia kikamilifu handisheki wakiamini kinara mwenzao aliwasaliti,” aeleza Bw Musila.

Mdadisi huyu anasema hili linadhihirishwa na ujanja wa Odinga wa kutumia wapinzani wa vinara wenzake katika ngome zao hata wakati ambao anadai lengo la BBI ni kuunganisha Wakenya.

“Amekumbatia mahasimu wa kisiasa wa Bw Musyoka eneo la Ukambani magavana Alfred Mutua (Machakos), Kivutha Kibwana (Makueni) na Charity Ngilu (Kitui). Katika eneo la Magharibi ambalo ni ngome ya Musalia na Wetang’ula ana vibaraka wanaosambaratisha umoja wa jamii ya Waluhya,” aeleza.

Mapema wiki hii, Bw Wetang’ula alilaumu chama cha ODM kwa kuwa kizingiti cha kuunganisha jamii ya Mulembe.

Bw Odinga ana wafuasi wengi eneo la Magharibi na naibu kiongozi wa chama cha ODM Wycliffe Oparanya anatoka Kakamega ambayo ni ya pili kwa wingi wa wapigakura miongoni mwa kaunti za eneo la Magharibi baada ya Bungoma anakotoka Wetang’ula.

Wetang’ula alidai kwamba Odinga amekuwa akitumia jamii ya Waluhya wakati wa uchaguzi na kuisahau akisema hata handisheki iliwabagua wakazi wa eneo hilo.

Itakumbukwa kuwa baada ya handisheki, Wetang’ula alidai NASA ilikuwa imekufa.

Kulingana na Bw Haraka, badala ya Bw Odinga kutumia vinara wenza katika NASA kudumisha umaarufu wake katika ngome zao, ameweka vibaraka katika vyama vyao.

“Katika hatua ya kuzika NASA eneo la Magharibi, anatumia akina Malala (Cleopas, seneta wa Kakamega na akina Otsosi (mbunge wa kuteuliwa) miongoni mwa wengine kumpiga vita Mudavadi ambaye wanafaa kuwa wakishauriana. Inasikitisha lakini ni kawaida ya siasa,” asema Bw Haraka.

Wadadisi wanasema kwamba ingawa Musyoka, Musalia na Wetang’ula wanasisitiza kuwa watagombea urais 2022, watakuwa katika moja ya miungano mikubwa ya kisiasa itakayobuniwa kabla ya uchaguzi huo.

Bw Mudavadi anasema kuwa ODM kilivunja mkataba wa muungano wa NASA. “Tuliweka kila kitu katika maandishi hata jinsi ya kugawana mapato lakini ndugu zetu walikiuka,” alisema.

ODM kimekataa kugawia vyama tanzu mapato ya kima cha Sh4.2 bilioni kutoka hazina ya vyama vya kisiasa huku maafisa wake wakiongozwa na katibu mkuu Edwin Sifuna wakitisha vyama hivyo kujiondoa katika muungano huo.