MakalaSiasa

JAMVI: Hali ya Alfred Keter yaanika vita vya ubabe baina ya Ruto na Gideon Moi

March 4th, 2018 3 min read

Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Keter alipokamatwa katika Benki Kuu ya Kenya kwa madai ya kuwasilisha hati ghushi za dhamana zenye kiasi cha Sh633 milioni. Picha/ Maktaba

Na WANDERI KAMAU

Kwa ufupi:

  • Bw Keter alilazimika kuahirisha hafla kwa hofu kwamba uhasama wa kisiasa kati ya wawili hao ungezidi kupanuka
  • Kuna uwezekano kwamba mtandao wa uasi dhidi ya Bw Ruto utaendelea kuwa mkubwa
  • Uwepo wa Bw Moi kumtetea Bw Keter ndiyo ishara ya wazi kwamba masaibu yake yanajikita kiwazi na ung’ang’aniaji wa kisiasa
  • Bw Moi anapania kuwajumuisha watu ‘waasi’ katika ukanda wa Mlima Kenya, ili kumwezesha kupenya katika ngome hiyo

KUFUTILIWA mbali kwa uchaguzi wa Alfred Keter kama mbunge wa Nandi Hills mnamo Alhamisi kulidhihirisha upeo wa vita vikali vya kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na Seneta Gideon Moi wa Baringo katika udhibiti wa Bonde la Ufa kuelekea uchaguzi wa 2022.

Hili linatokana na matukio ya siku kadhaa kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo, ambapo hafla ya kuwashukuru wakazi wa Nandi Hills  kwa kumchagua Bw Keter kama mbunge, ilifutiliwa mbali ghafla katika hali tatanishi.

Duru kutoka wale waliokuwa wakipanga hafla hiyo, walisema kwamba Bw Keter alilazimika kuahirisha hafla hiyo kwa hofu kwamba uhasama wa kisiasa kati ya wawili hao ungezidi kupanuka, hivyo kuzua mgawanyiko zaidi wa kisasa katika ukanda huo.

Na ingawa Bw Keter hakueleza wazi sababu za kufutilia mbali hafla hiyo mara moja, wabunge 16 waliokuwa wamepangiwa kuhudhuria walisema kwamba aliwapigia simu kuwaarifu kwamba hafla hiyo haingefanyika.

“Alitupigia simu na kutwambia kwamba hafla hiyo haingefanyika kama ilivyopangwa, ila hakutoa ufafanuzi zaidi,” akasema mbunge mmoja, ambaye hakutaka kutajwa.

Aidha, duru zilieleza kwamba mbunge wa Cherangany, Joshua Kutuny ndiye alishauri hafla hiyo kufutiliwa mbali, baada ya kuibuka kwamba Bw Moi angehudhuria.

Hafla hiyo ilikuwa imepangiwa kufanyika katika uwanja wa Koitalel Samoei Museum, katika eneo la Nandi Hills.

Kulingana na wadadisi, huo huenda ukawa mwanzo wa vita vikali vya kisiasa kati ya wawili hao, hasa wanapopania kuwania urais mnamo 2022.

 

Vita

“Huu ni mwanzo wa vita vikali ambavyo vitaendelea kupanuka kadri siku zinavyosonga. Kuna uwezekano kwamba mtandao wa uasi dhidi ya Bw Ruto utaendelea kuwa mkubwa,” aonya mchanganuzi wa kisiasa Herman Manyora.

Uhasama wa kisiasa kati ya wawili hao ulijitokeza mapema mwezi huu, pale Bw Keter alikamatwa katika Benki Kuu ya Kenya kwa madai ya kuwasilisha hati ghushi za dhamana zenye kiasi cha Sh633 milioni.

Baada ya kukamatwa kwake, Bw Moi aliongoza kundi la wabunge kutoka Bonde la Ufa katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga, kushinikiza kuachiliwa kwa Bw Keter.

Baadhi ya wale waliozungumza waliyahusisha masaibu ya Bw Keter na “njama za watu maarufu serikalini ambao wamekuwa wakimpiga vita.”

“Huu ni udhalilishaji wa wazi wa kisiasa. Tunashangazwa na kimya cha wenzetu (wanasiasa kutoka Bonde la Ufa) wakati mwenzetu anadhulumiwa kwa visingizio vya wazi,”akasema Bw Kutuny.

Awali, Bw Keter alikuwa amekaidi agizo la Rais Uhuru Kenyatta na Bw Ruto kujiuzulu kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Kuhusu Leba.

 

Ishara ya wazi

Wachanganuzi wa kisiasa wanasema kuwa uwepo wa Bw Moi kumtetea Bw Keter ndiyo ishara ya wazi kwamba masaibu yake yanajikita kiwazi na ung’ang’aniaji wa kisiasa kati ya mibabe hao wawili wa kisiasa.

Baada ya Mahakama Kuu ya Eldoret kutupilia mbali ushindi wake, Bw Keter alionekana mwenye ghadhabu, akisema kwamba “alitarajia hilo.”

“Vita ninavyopigwa ni vikubwa sana kuliko mnavyofikiria. Ni vita vilivyoanzishwa dhidi yangu baada ya kujitokeza wazi kukashifu ufisadi unaoendelezwa na Serikali Kuu,”akasema.

Muda mfupi baadaye, umati mkubwa wa watu uliojitokeza ulianza kuimba nyimbo za kumkashifu Bw Bw Ruto, zikimtaja kuwa kiini kikuu cha masaibu yanayomwandama Bw Keter.

Kulingana na Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za Bonde la Ufa, Bw Moi anajaribu kujijengea himaya yake ya kisiasa, hasa ikiwa dhahiri kwa sasa kwamba Bw Ruto ndiye mwaniaji urais wa Chama cha Jubilee.

“Bw Moi hana lingine kwa sasa ila kubuni mtandao huru wa wanasiasa ambao watamsaidia kupenya zaidi katika maeneo yote ya ukanda huo. Ni kibarua kigumu, ila kinaashiria vita vikali ambavyo vitakuwepo kati yao,”asema Bw Mutai.

 

Mpango wa Moi

Kumeibuka ripoti kwamba katika kupanua mtandao wake wa kisiasa, Bw Moi anapania kuwajumuisha watu ‘waasi’ katika ukanda wa Mlima Kenya, ili kumwezesha kupenya katika ngome hiyo.

Baadhi ya wanasiasa ambao wanalengwa na Bw Moi ni aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo, kiongozin wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua, mwanasiasa Kilemi Mwiria kati ya wengine ambao wameachwa nje na Rais Uhuru Kenyatta katika serikali yake.

Wachanganuzi wanatabiri kwamba huenda muungano huo wa wanasiasa waasi ukawa kikwazo kikubwa kwa Bw Ruto, hasa katika kupenya ngome za Bonde la Ufa na Mlima Kenya.

“Ingawa kulingana na mkataba wa Jubilee, jamii za GEMA na Wakalenjin zitamuunga mkono Bw Ruto, anapaswa kutahadhari kwani kuibuka kwa viongozi kama Keter kunaashiria mchipuko wa kundi la wanasiasa huru ambao watakuwa kikwazo kikubwa kwake kupenya ngome hizo,”asema mchanganuzi Wycliffe Muga.

Licha ya hayo, baadhi ya viongozi wamejitokeza kumtetea Bw Ruto, wakisema kuwa analaumiwa bure na wanasiasa kwa masaibu yanayowakumba.

“Huwezi kumhusisha Naibu Rais (Ruto) kwa kutozingatia nidhamu ya uongozi,”asema mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.