Makala

JAMVI: Hasla anavyojengwa kisiasa na maadui badala ya kubomolewa

October 4th, 2020 3 min read

Na WANDERI KAMAU

IMEIBUKA kuwa wakosoaji wakuu wa Naibu Rais William Ruto wanamsaidia kujijenga kisiasa, badala ya kupunguza umaarufu wake miongoni mwa Wakenya.

Miongoni mwa wale ambao wameibukia kuwa wakosoaji wake wakuu ni kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli, Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee (JP) David Murathe, Katibu wa JP Raphael Tuju, viongozi wa mrengo wa ‘Kieleweke’ na wengineo.

Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa, mwelekeo wa sasa, ambapo viongozi hao wameungana kumkosoa Dkt Ruto na mbinu anazotumia kufanyia kampeni, unamfanya kupata umaarufu zaidi kwani karibu wote wanamtaja kwenye semi zao.

Wanasema kwa kumkosoa yeye binafsi kwa kutumia neno “Hustler” (Maskini) kwenye kampeni zake, wanasahau kuwa wanamsaidia kulipa umaarufu neno hilo, kama mengine ya awali.

“Lengo kuu la Dkt Ruto ni kuwa na neno maalum litakalompa utambulisho miongoni mwa Wakenya wa tabaka la chini, kama walivyofanya marehemu Daniel Moi, Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta miongoni mwa wafuasi wao. Ni hali iliyowapa umaarufu mkubwa hata ikiwa hawakupendwa katika baadhi ya sehemu nchini,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Bw Moi alisifika kwa kutumia neno “Nyayo”, Bw Odinga “Tinga” ama “Agwambo” huku Rais Kenyatta akipewa msimbo wa neno “Kamwana” (Kijana) au “Uhunye” na wafuasi wake katika ukanda wa Mlima Kenya na miongoni mwa vijana mtawalia.

Viongozi hao wamekuwa wakimkosoa vikali Dkt Ruto kwa kukita kampeni zake kwenye taswira ya ‘Maskini’ dhidi ya ‘Matajiri’ (Hustlers vs Dynasties), wakisema kuwa anawahadaa Wakenya kwamba yeye ni maskini.

Vilevile, wamekuwa wakimkosoa kwa kuwapa vijana vifaa vya “kujiendeleza” kama vile wilbaro, mashine za kuoshea magari, mapipa ya maji kati ya nyingine.

Dkt Ruto amekuwa akitoa vifaa hivyo kwa makundi ya vijana ambayo yamekuwa yakimtembelea kwenye makazi yake katika mtaa wa Karen, jijini Nairobi.

Zaidi ya hayo, amekuwa akitoa michango ya fedha kufadhili ujenzi wa makanisa katika sehemu tofauti nchini. Wadadisi wanasema kama kambi shindani, viongozi hao wanaonekana kushindwa kubuni mbinu za kumkabili Ruto, bali wamemgeukia yeye binafsi na njia anazotumia kujipigia debe.

“Tuko katika hali ambapo lazima viongozi wabuni mbinu na kaulimbiu za kujipa umaarufu miongoni mwa Wakenya wala si kila mara kuwakosoa washindani wao. Mtindo wa kumkosoa mshindani ni njia nyingine ya kumpa umaarufu,” asema Bw Linford Mwangi, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Baadhi ya “makosa” ambayo viongozi hao wanaelezwa kufanya ni kujaribu kurejelea usahihi wa neno “Hustler”, ambalo Dkt Ruto amelikumbatia kuonyesha taswira kamili kwamba yeye amejijenga kutoka kuwa mtu maskini hadi kuwa Naibu Rais.

Kwenye kikao na wanahabari wiki iliyopita, Bw Atwoli aliwatahadharisha Wakenya dhidi ya kukubali kubandikwa jina hilo, akitaja maana yake halisi kuwa “mtu aliyejipa mali kwa njia ya mkato”.

“Ninawaomba Wakenya kutokuwa taifa la “mahustlers” (maskini). Wao ni watu wenye uwezo mkubwa. Wanapaswa kukubali hali ambayo watoto wao wanasoma na kupata ajira za hadhi zinazolingana na viwango vya masomo yao,” akasema Bw Atwoli.

Hata hivyo, Bw Mwangi anakosoa vikali hatua ya Bw Atwoli, akisema kuwa kama mabwana Moi, Odinga na Rais Kenyatta, ni vigumu sana kwa wafuasi wa kiongozi yeyote kubadilisha misimamo yao, hasa wanapomtambua kuwakilisha maslahi yao.

“Bw Moi alifanikiwa kuitawala nchi kwa miaka 24 tangu 1978, msingi mkuu ukiwa kauli yake kwamba ‘angefuata nyayo za Mzee Jomo Kenyatta.”

“Huo ni usemi ambao ulimpa umaarufu mkubwa miongoni mwa wafuasi wake, hata baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali mnamo 1982.

“Waliendelea kuonyesha uaminifu mkubwa sana kwake, hadi alipostaafu mnamo 2002. Baadhi hata walisikika wakilia, hukiu wakiapa kuwa walikuwa tayari kufuata agizo lolote ambalo angewapa,” asema Bw Mwangi.

Anasema uzalendo huo ndio umemjenga Bw Odinga miongoni mwa wafuasi wake tangu 1997, alipowania urais kwa mara ya kwanza.

Vivyo hivyo, wanataja hilo kama sababu kuu ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto kupigiwa kura mnamo 2013 licha ya mashtaka yaliyowakabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa madai ya kuchochea ghasia za uchaguzi wa 2007/2008.

“Uwepo wa neno linalomtambulisha kiongozi huzua mshikamano fulani kati yao na wafuasi wao, ambapo huwa vigumu kuuondoa. Ni kwa sababu hiyo ambapo lazima wakosoaji wa Dkt Ruto wabuni njia huru za kampeni badala ya kurejelea mbinu zake. Hilo litaendelea kumjenga,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji hao wanasema kuwa msimamo wao ni kuhakikisha Wakenya hawapumbazwi na viongozi wanaojifanya kujali maslahi yao.

“Hatutakubali kamwe kuona watu wetu wakidanganywa kwa kurushiwa punje za mahindi kama kuku. Lazima tuwaeleze ukweli,” asema mbunge Ngunjiri Wambugu wa Nyeri Mjini, ambaye ni mwanzilishi wa kundi la ‘Kieleweke.’