MakalaSiasa

JAMVI: Historia ya utengano baina ya Raila na Kalonzo yaanza kubisha hodi tena

March 4th, 2018 3 min read

Vinara wa NASA, Bw Raila Odinga na Kalonzo Musyoka (kushoto) wakihutubia wanahabari awali. Picha/ Maktaba

Na BENSON MATHEKA

Kwa ufupi:

  • Wanasiasa wa ODM wanataka kuvunja muungano wa NASA ili kukwepa makubaliano kati ya Odinga na vinara wenza kwamba hatagombea urais 2022
  • Bw Mathuki, alimuonya Bw Odinga dhidi ya kujitenga na NASA ikiwa anataka kufikia ndoto yake ya kisiasa
  • Chama cha ODM kimekuwa kikidhalilisha vyama tanzu tangu Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula kwa kususia hafla ya kumuapisha Bw Odinga
  • Hakuna dalili kwamba kuna juhudi za kuokoa muungano huo ambao una mamilioni ya wafuasi.

HISTORIA inajirudia katika uhusiano wa kisiasa kati ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na mwenzake wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka huku dalili zikionyesha kuwa muungano wa NASA unaelekea kusambaratika.

Wadadisi wanasema kuwa uhusiano kati ya viongozi hao umedorora mno tangu hafla ya kiapo ya Bw Odinga kuwa rais wa wananchi japo wanasisitiza wameungana.

Bw Musyoka na vinara wenza wawili Musalia Mudavadi na Moses Wetangula walisusia hafla hiyo. Kulingana na mdadisi wa masuala ya kisiasa Dkt Paul Kalei, japo vinara hao wanasisitiza kuwa wangali wameungana, matamshi ya wanasiasa wa vyama vyao na washirika wao wa kisiasa yanaonyesha kuwa huenda Bw Odinga na Bw Musyoka wakajipata katika hali iliyopelekea kutengana kwao kabla ya uchaguzi wa 2007.

“Watajipata katika hali sawa iliyopelekea kutengana kwao kabla ya uchaguzi wa 2007. Wakati huo, Raila alimsaliti Bw Musyoka japo walikuwa wamekubaliana amuunge mkono kugombea urais katika chama cha ODM Kenya.

Raila alisukumwa na wandani wake na kuamua kugombea urais baada ya kutwaa chama cha ODM kutoka kwa waliokuwa wamekisajili naye Musyoka akagombea urais kwa tiketi ya chama cha ODM Kenya kilichokuwa kimesajiliwa na wandani wake wa kisiasa,” asema Bw Kalei.

Anasema wanasiasa wa ODM wanataka kuvunja muungano wa NASA ili kukwepa makubaliano kati ya Odinga na vinara wenza kwamba hatagombea urais 2022. Anasema wanasiasa wa ODM wanataka kutumia hafla ya kumuapisha Bw Odinga kama kisingizio cha kuvunja NASA ili kumtenga Bw Musyoka.

 

Kurudisha mkono 

“Lengo ni kumtenga Bw Musyoka ambaye anaamini kwamba Bw Odinga anafaa kurudisha mkono na kumuunga kugombea urais 2022.

“Hii ndio sababu wanasiasa wa ODM wamekuwa wakimdhalilisha Bw Musyoka kwa kumuita mwoga alipokosa kuapishwa,” asema Bw Kalei.

Hata hivyo chama cha Wiper, kilionya viongozi wa chama cha ODM dhidi ya kumpotosha Bw Odinga, kwa kumtaka kujitenga na muungano huo.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Peter Mathuki na aliyekuwa seneta wa Machakos Johnson Muthama wanasema viongozi wa vyama tanzu vya NASA wanafaa kuheshimiana kwa sababu hakuna chama kikubwa kuliko kingine.

Katika kauli iliyomlenga Katibu Mkuu wa ODM Bw Edwin Sifuna na naibu kiongozi Hassan Joho, waliodai ODM  hakitajadili siasa za 2022 na vinara waliosusia kiapo cha Bw Odinga Bw Mathuki alisema baadhi ya wanasiasa wanaowadhalilisha vinara wa vyama vingine katika NASA hawajui muungano huo ulivyobuniwa na malengo yake.

“Wanaoambia baadhi ya vyama kuhama NASA ndio wanaofaa kuhama kwa sababu ya kudharau wanaojua asili ya NASA. NASA sio mali ya chama kimoja. Hatutakubali yeyote kumdharau kiongozi wetu na hatutoki NASA. Ni wao wanaofaa kutuheshimu,” alisema Bw Mathuki.

 

Tisho la ODM

Mnamo Jumatatu Bw Sifuna alivitaka vyama tanzu vya NASA kuheshimu ODM kwa kuwa ndicho chama kilicho na wabunge wengi au vijitenge na muungano huo.

Alisema vinara wa NASA hawafai kuzungumzia uchaguzi wa 2022 kabla ya kupigania haki katika uchaguzi.

Hata hivyo, Bw Mathuki alisema mikakati ya uchaguzi wa 2022 ni lazima na kushangaa kwa nini ODM kinataka kuipuuza. “Haki katika uchaguzi inahusu 2022 kwa sababu hatuwezi kupigania yaliyopita 2017,” alisema.

Bw Mathuki, alimuonya Bw Odinga dhidi ya kujitenga na NASA ikiwa anataka kufikia ndoto yake ya kisiasa. Alisema ni kupitia muungano huo ambapo viongozi wa vyama tanzu, Odinga, Stephen Kalonzo Musyoka wa Wiper, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC) na Moses Wetangula wa Ford Kenya wanaweza kutimiza ndoto na malengo yao ya kisiasa.

“Ikiwa Raila ataamua kujitenga na NASA na kufuata njia yake, hataenda mbali, atashindwa. Itakuwa hivyo kwa vinara wengine wa NASA kwa sababu hawataweza kutimiza malengo yao ya kisiasa kwa Wakenya,” Bw Muthama alisema kwenye mahojiano na ukumbi huu kwa njia ya simu.

 

Si rahisi

Aliwataka wafuasi wa NASA kutotishwa na kauli ya wanasiasa wa vyama tanzu kwamba vyama hivyo vitajitenga akisema ni vinara wenyewe wanaoweza kuamua kuvunja muungano huo. “Kuvunja NASA sio rahisi. Kuna utaratibu unaohitaji mashauriano ya kina na maazimio makali,” alisema.

Chama cha ODM kimekuwa kikidhalilisha vyama tanzu tangu Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula kwa kususia hafla ya kumuapisha Bw Odinga katika bustani ya Uhuru Park Januari 30.

Bw Mathuki alisema badala ya kumdhalilisha Bw Musyoka, wanasiasa wa NASA wanafaa kumpongeza kwa kutokubali kushiriki kiapo batili.

“Kiongozi wa chama chetu alichukua hatua ya ujasiri kwa kutoshiriki kiapo batili. Wale wanaomdhalilisha wangeelewa alichofanya wangemsifu. Hata Maandiko Matakatifu yanakataa kiapo batili,” alisema.

Hata hivyo Bw Kaleli anasema hakuna dalili kwamba kuna juhudi za kuokoa muungano huo ambao una mamilioni ya wafuasi.  Anakubaliana na Bw Muthama kwamba kuvunjika kwa NASA kutapatia Jubilee fursa ya kuwa na mteremko kwenye uchaguzi wa 2022 ikiwa haitakumbwa na misukosuko.