MakalaSiasa

JAMVI: Hofu kuwa katiba inayopendekezwa itakuwa ghali zaidi

March 10th, 2019 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

KATIBA mpya inayopendekezwa huenda ikawa ghali zaidi kutekelezwa kuliko Katiba ya 2010.

Wanaunga mkono kubadilishwa kwa katiba wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, wanapendekeza kupanuliwa kwa serikali kuhakikisha kuwa jamii zote zinawakilishwa.

Rais Kenyatta anasema mfumo wa sasa unaruhusu wachache kuingia serikalini huku watu wa jamii nyingine zikiachwa nje hivyo kuhisi kutengwa.

Hiyo inamaanisha kwamba, kuna uwezekano wa kubuniwa kwa nyadhifa zaidi, ukiwemo wadhifa wa waziri mkuu ambaye ofisi yake itakuwa na wafanyakazi watakaolipwa mamilioni ya fedha.

Bw Odinga anataka katiba mpya kuwa na serikali za kanda mbali na serikali za kaunti.

Bw Odinga alipokuwa akihutubia Kongamano la Magavana katika kaunti ya Kakamega mwaka jana, alipendekeza kuwepo kwa serikali za kanda 14.

“Ili kuboresha ugatuzi, kuna haja ya kuboresha ugatuzi kwa kubadili mfumo wa usimamizi,” akasema Bw Odinga.

Wadadisi wamekosoa pendekezo hilo kwa kusema kwamba likitekelezwa walipa ushuru watatwika mzigo wa ziada hivyo kufanya gharama ya maisha kuongezeka.

Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za serikali Edward Ouko ilionyesha kuwa Katiba ya 2010 iliyobuni Seneti na serikali za kaunti ilikuwa ghali mno.

Kwa mfano, Bw Ouko alisema kuwa gharama ya kuendesha Bunge la Kitaifa na Seneti iliongezeka hadi Sh23 bilioni kwa mwaka ikilinganishwa na Sh10.2 bilioni kabla ya kupitishwa kwa katiba ya sasa.

“Gharama ya kuendesha mabunge mawili yaliyo na jumla ya wawakilishi 418 imeongezeka maradufu ikilinganishwa na zamani ambapo kulikuwa na bunge moja lenye wawakilishi 222,” akasema Bw Ouko.

Licha ya kumiminiwa sifa tele na jamii za kimataifa kwa kuitaja kama ‘Katiba ya Mwananchi’, Katiba ya 2010 ni ghali mno kutekelezwa.

Kufikia sasa, baadhi ya vipengele havijatekelezwa. Miongoni mwa mambo ambayo hayajetekelezwa ni kifungu kinachohitaji kuwepo kwa usawa wa kijinsia bungeni. Kifungu hicho kinahitaji watu wa jinsia moja wasizidi theluthi mbili.

Mswada wa kutaka wanawake zaidi wateuliwe katika Bunge la Kitaifa na Seneti umegonga mwamba tangu 2016. Wanaoupinga wanasema kuongeza wabunge zaidi wa kike kutawagharimu walipa ushuru.

Naibu wa Rais William Ruto ambaye ametofautiana na Rais Kenyatta, anasisitiza kuwa hakuna haja ya kupanua serikali.

Dkt Ruto anapendekeza kubuniwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani.

Iwapo pendekezo hilo la naibu wa rais litajumuishwa katika mabadiliko hayo ya katiba, basi huenda walipa ushuru wakajitwika mzigo mzito kwani afisi ya kiongozi wa upinzani itahitaji kutengewa bajeti.

Huku Rais Kenyatta na Bw Odinga wakipigania kupanuliwa kwa serikali, kiongozi wa chama cha upinzani cha Third Alliance Ekuru Aukot tayari amewasilisha saini milioni 1.4 kwa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) akitaka wabunge wapunguzwe hadi 147 kutoka 416.

Dkt Aukot anataka wabunge wawili pekee kuchaguliwa kwa kila kaunti.

Mkurugenzi wa Shirika la International Center for Policy and Conflict Ndung’u Wainaina anaunga mkono Dkt Aukot kwa kutaka idadi ya wabunge na madiwani kupunguzwa.

Bw Wainaina, hata hivyo, anasema kuwa suala linalofaa kupewa kipaumbele katika mabadiliko ya katiba ni kupewa nguvu zaidi kwa Idara ya Mahakama na Bunge.

“Licha ya katiba kutenganisha Serikali Kuu, Idara ya Mahakama na Bunge bado tunaona utendakazi wa korti na wabunge ukiingiliwa na wakuu serikalini. Kuna haja ya kubuni mbinu za kuhakikisha kuwa asasi hizo zinatekeleza majukumu yao bila kuingiliwa,” anasema Bw Wainaina.

Kamati iliyobuniwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga kukusanya maoni ya Wakenya kuhusu jinsi ya kutatua changamoto zinazokumba nchi, linatarajiwa kuwasilisha ripoti yake rasmi Mei, mwaka huu.

Bw Odinga, mwezi uliopita, alidokeza kwamba kura ya maamuzi kubadili katiba huenda ikafanyika mwaka huu.

“Mwaka huu ni wa mabadiliko, wanaopinga mabadiliko hayo wanafaa kutangaza msimamo mapema,” akasema Bw Odinga.

Wadadisi wanatabiri kwamba rasimu ya Katiba mpya huenda ikabuni vyeo tele na ili kuyafurahisha makundi mbalimbali ili kuiunga mkono.

“Rasimu ya katiba ambayo mpya itakuwa na vigezo vya kufurahisha wabunge, madiwani, wabunge, wanawake, magavana ili waunge mkono rasimu hiyo,” anasema George Mboya, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

“Iwapo mapendekezo hayo yatalenga kupunguza, kwa mfano, viti vya madiwani au wabunge, inaweza kupingwa vikali hivyo kuwa pigo kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga,” anaongezea.