MakalaSiasa

JAMVI: Huenda Ekuru Aukot ni mradi wa serikali kuhusu kura ya maamuzi

June 16th, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

MJADALA kuhusu mageuzi ya Katiba kupitia kura ya maamuzi sasa umechukua msukumo mpya kufuatia hatua ya Kiongozi wa Wengi bungeni Aden Duale kuuunga mkono juhudi zinazoendeshwa na chama cha Thirdway Alliance kinachoongozwa na Ekuru Aukot.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) tayari inakagua sahihi milioni 1.4 za wapiga-kura zilizowasilishwa na chama hicho chini ya mpango maarufu kama “Punguza Mzigo”.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati ametoa hakikisho kwamba shughuli itakamilika “hivi karibuni” ili kutoa nafasi ya kuanzishwa rasmi kwa mchakato wa marekebisho ya katiba.

Akichangia mjadala kuhusu ripoti kuhusu makadirio ya bajeti iliyoandaliwa na Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, Bw Daule alisisitiza kuwa kura ya maamuzi sharti ifanyike ili kuboresha utawala nchini. Alisisitiza kuwa atahakikisha kuwa mswada wa kufanikisha zoezi hilo unapita bungeni.

Kauli ya hiyo imeibua hisia kwamba huenda wakili Aukot ni “mradi” wa wakuu fulani serikalini ikizingatiwa kuwa Bw Duale ni mwakilishi na mtetezi wa sera, maongozi, ajenda na misimamo yake ndani na nje ya bunge.

Lakini kwenye mahojiano na Taifa Jumapili Bw Aukot alisisitiza kuwa mpango wa “Punguza Mzigo” haupati usaidizi wowote kutoka kwa viongozi serikali ila Wakenya ambao wanaumizwa na mzigo mzito wa kulipa ushuru kugharamia nyadhifa nyingi za uongozi.

“Punguza Mzigo ni mradi wa wananchi wote 45 milioni wala sio wachache kama Duale na wengine. Lakini hatutawazuia kuunga mkono juhudu zetu za baada ya wao kung’amua kuwa zinalenga kuwasaidia Wakenya. Wako huru kutuinga mkono kufanikisha mradi huu wa kuwakomboa Wakenya,” akasema Bw Aukot ambaye aliwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Baadhi ya matakwa ya Thirdways Alliance ni kwamba katiba ifanyiwe mageuzi ili kupunguza idadi ya wabunge na maseneta kutoka 416 hadi 147 kwa kuondolewa kwa nafasi za Wabunge Wawakilishi wa Kaunti na wabunge maalum.

Vile vile, chama hicho kinapendekeza kuwa idadi ya madiwani ipunguzwe kutoka 2225 hadi 700 kupitia kupunguzwa kwa idadi ya wadi na kufutiliwa mbali kwa nafasi za madiwani maalum.

Kwa mujibu wa Bw Aukot Kenya inahitaji nyadhifa chache za uwakilishi ili kupunguza gharama kwa mlipo ushuru na kuelekeza fedha nyingi kwa miradi ya maendeleo.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anahisi kuwa kauli ya Bw Duale kuunga mkono kura ya inapasa kuchukuliwa kwa uzito kwa sababu kuna uwezekano mkubwa kwamba inaakisia fikra na msimamo wa Rais Uhuru Kenyatta.

“Bw Duale ni macho na masikio ya serikali inayoongozwa na Rais Kenyatta bungeni. Wajibu mkuu kama kiongozi wa wengi ni kutoa, kutetea na kuvumisha ajenda na misimamo ya serikali katika jumba hilo. Hii ndio maana yeye ndiye hutia saini na kuwasilisha miswada na hoja zote za serikali bungeni,” anasema.

Bw Andati anaongeza kuwa ingawa Duale ni mmoja wanasiasa wandani wa Naibu Rais William Ruto ambaye amekuwa akipinga mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maamuzi cheo anachoshikilia kinamhitaji kuwajibika moja kwa moja kwa Rais Kenyatta.

Itakumbukwa kuwa tangu Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga waliporidhiana kisiasa mnamo Machi 9, 2018, kiongozi huyo wa taifa amedokeza mara si moja kuhusu uwezekano wa katiba kufanyiwa mageuzi kupitia kura ya maamuzi. Naye Bw Odinga amebashiri kuwa kuna mabadiliko makubwa ambayo yatatokea nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Itakumbukwa kuwa katika ziara yake ya kwanza Kisumu Novemba mwaka 2018 Rais Kenyatta alielezea haja ya kubadilishwa kwa mfumo wa uongozi nchini kupitia kupanuliwa kwa kitengo cha utawala.

“Tunataka serikali jumuishi; ambayo itahakikisha kuwa kile eneo linawakilishwa. Haja kubwa ya muafaka kati yangu na ndugu yangu Raila ni kuondoa huu mtindo wa sasa ambapo upande ulioshinda katika uchaguzi mkuu ndio unachukua nyadhifa zote,” akasema alipohutubia wananchi katika eneo la Ahero.

Rais Kenyatta alirudia kauli hiyo mnamo Februari mwaka huu alipozuru kaunti ya Kisii ambapo aliwataka Wakenya kuunga mkono Kamati ya Maridhiano (BBI) ambayo imekuwa ikikusanya maoni na mapendekezo ya Wakenya kuhusu njia za kuleta umoja na maridhiano ya kudumu nchini.

Na akizungumza juzi katika msikiti wa Jamia, jijini Nairobi aliposhiriki sala ya Iftar Rais Kenyatta aliwahakikisha waumini wa dini ya Kiislamu kwamba baadhi ya matakwa yao yatashughulikiwa katika mageuzi ya Katiba. Viongozi wa Kiislamu waliohudhuria hafla hiyo, akiwemo Bw Duale, walitaka Sikuu za Idd Fitri na Idd Uldha zitambuliwe rasmi kikatiba.

Mbali na hayo, baadhi ya wabunge wa ODM wamekuwa wakimshikiniza Katiba ifanyiwe marekebisho kupitia kura ya maamuzi ili kubuniwe wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka.

Wabunge John Mbadi (Suba), Anthony Oluoch (Mathare), Tom Odege (Nyatike), Junet Mohammed (Suba Mashariki), Seneta wa Siaya James Orengo na Katibu Mkuu Edwin Sifuna juzi walidai kuwa muafaka kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta haitakuwa na maana pasina kura ya maamuzi kufanyika.

“Ili kuonyesha kuwa handisheki ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ilikuwa ya kweli serikali haina budi kutenga pesa za kufadhili kura ya maamuzi katika bajeti ya mwaka ujao wa kifedha wa 2019/2020,” akasema Bw Orengo ambaye ni kiongozi wa wachache katika seneti.

Viongozi hao walitoa makataa ya hadi Machi 2020 kwa Rais Kenyatta na Odinga kuhakikisha kuwa Katiba inafanyiwa mageuzi “ili kuimarisho mfumo wa uongozi nchini” huku wakiongeza kuwa jopo la BBI tayari limekubali kufanyike kura ya maamuzi.

Hata hivyo, Naibu Mwenyekiti wa jopo la BBI Dkt Adams Oloo ametofautiana na wanasiasa hao akisema jopo hilo halijafikia uamuzi kama huo. Alishikilia kuwa jopo hilo halitayumbishwa na “kauli za kisiasa” zinazotolewa na viongozi kama hao bali litaendelea kutekeleza kazi yake kwa uadilifu.

“Hatujatoa mapendekezo yoyote kufikia sasa. Na wajibu wa kamati yetu sio kukusanya maoni kuhusu mageuzi ya katiba, bali njia za kuhakikisha kuna umoja na maridhiano nchini,” akasema Dkt Oloo.

Kamati hiyo inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga mwezi Oktoba mwaka ambapo inatajiwa kutoa mwelekeo kuhusu namna ya kuboresha utawala nchini.