HabariMakalaSiasa

JAMVI: Je, Mlima Kenya waweza kumuunga mkono Kalonzo uchaguzini 2022?

February 11th, 2018 4 min read

Kiongozi wa chama cha Wiper Bw Kalonzo Musyoka asema na Rais Uhuru Kenyatta katika hafla ya awali. Picha/ Maktaba

Na MWANGI MUIRURI

Kwa Muhtasari:

  • Baadhi ya wadadisi wa kisiasa wasema yawezekana hasa iwapo maafikiano ya UhuRuto hayatatimilika
  • Hatua ya Kalonzo kuokoa serikali ya Rais Mstaafu Mzee Mwai Kibaki 2007 inaweza kurejelewa ili kuunda ushirika mwingine wa 2022
  • “Kalonzo huyu ambaye hana msimamo thabiti na huwa ni wa kutegea mawindo yatekelezwe, nyama ichinjwe na waliowinda wale kwanza halafu yeye anarukia mabaki”
  • Kalonzo hana uthabiti mkubwa Ukambani kutokana na kuibuka kwa uasi wa wazi

WENGI wetu tutazidi kukumbushwa na matukio ya kila mara kwamba siasa ni sawa na mchezo wa pata-potea. Hivi leo kauli hii inapochanganuliwa, tayari Rais Uhuru Kenyatta amemuahidi naibu wake, Bw William Ruto kuwa ndiye atakayemrithi mwaka wa 2022.

Lakini kuna hisia ambazo zinaibuka katika ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya inayoashiria kuwa urithi huo sio tu wa kusemwasemwa katika mikutano ya hadhara, bali unafaa kuungwa mkono na mkataba wa kimaelewano kuhusu jinsi ushirika wa eneo hilo na serikali inayopendekezwa ya Ruto utakavyotimilika.

Tayari, wanasiasa wasiochuchukuliwa kimzaha katika eneo la Mlima Kenya wameelezea wasiwasi wao kuhusu urithi wa Ruto.
Wale ambao wamekuwa wawazi na kusema sio lazima eneo hilo litii agizo la rais ni pamoja na aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo, aliyekuwa Seneta maalum, Paul Njoroge Ben, Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu na aliyekuwa mbunge wa Maragua, Elias Mbau.

Ikiwa pingamizi hizo zitatimia, basi eneo la Mlima Kenya litajipata katika mustakabali telezi wa kisiasa likisaka ushirika wa kumenyana katika kivumbi cha uchaguzi mkuu wa urais, 2022.

Kunao wanaopendekeza jina la Kalonzo Musyoka ambaye ni kinara wa Wiper Democratic Party-Kenya iwapo maelewano na Naibu Rais yatagonga mwamba.

 

Kuokoa serikali ya Kibaki

Hatua ya Kalonzo kuokoa serikali ya Rais Mstaafu Mzee Mwai Kibaki wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 ambapo alikubali kuunda serikali ya umoja wa Wakamba na Agikuyu ili kuzima makali ya Bw Raila Odinga, inaweza kurejelewa ili kuunda ushirika mwingine wa 2022.

Ni wazo ambalo ukumbi huu ulisaka maoni kulihusu na kukusanya hisia mseto zilitolewa; wengine wakionekana kukataa uwezekano huo moja kwa moja, wengine wakisema mazingira ya kisiasa hubadilika upesi na lolote linawezekana katika siasa.

“Nani aliamini kuwa Odinga mwenyewe mwaka wa 2002 angesema Kibaki Tosha na akae katika mkondo huo hadi kuvuna ufanisi wa jamii ya Luo Nyanza kumpigia Kibaki kura?” anahoji aliyekuwa mwakilishi wa wanawake wa Nyeri bungeni, Priscilah Nyokabi.

Anasema kuwa siasa ni mchezo wa lile ambalo linaweza kuzua ushindi wala si ushirika usiokuwa na hakika ya kuleta mafanikio.
Anasema kuwa hata wazo kama hilo la Kalonzo kujiunga na Mlima Kenya 2022 ndilo lililochezwa 2013 ambapo wengi hawakutarajia jamii za Agikuyu na Kalenjin ziungane dhidi ya Odinga.

“Mimi binafsi siwezi nikapuuza uwezekano huo. Lakini katika hali ya sasa, sioni Mlima Kenya wakimsaliti Ruto,” anasema Nyokabi.

 

Kalonzo ajitakase kwa Mlima Kenya

Anasema ili Kalonzo akubalike kuwa thabiti katika ushirika wa kuleta ushindi, ni lazima ajitakase kwa Mlima Kenya “ambao siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017 aliwaahidi watu wa Agikuyu kuwa Nasa ikiibuka na ushindi, watalala chini kama bahasha.”

Lakini mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa ambaye anatajwa kama miongoni wa walio guu mbele katika kutwaa ugombezi wa pamoja na Ruto 2022, anasema kuwa hilo haliwezekani.

“Ni Kalonzo huyu ambaye hana msimamo thabiti na huwa ni wa kutegea mawindo yatekelezwe, nyama ichinjwe na waliowinda wale kwanza halafu yeye anarukia mabaki?” anasema.

Anasema kuwa kujaribu kufikiria Kalonzo akiwa mwaniaji wa urais wa kuungwa mkono nje ya Ukambani ni ndoto ya ujuha kisiasa.

“Kwa sasa hana jina ndani ya mrengo pana wa National Super Alliance (NASA) baada ya kujipa nembo ya usaliti alipokataa kujitokeza kula kiapo cha afisi sawia na Odinga aliyejiapisha kama ‘rais wa wananchi,” asema Ichung’wa.

 

Ni muujiza kupata umaarufu tena

Anasema kuwa kwa sasa uwezekano wa Kalonzo kujipa thamani ya kisiasa umeyeyuka kama hewa, na ni muujiza tu na maajabu makuu yanayoweza kumrejesha katika soko la kisiasa.

Hata hivyo, Prof Ngugi Njoroge ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa anasema kuwa “wanasiasa ni wale wale, hali ikibidi, na iwe hakuna lingine la kutekelezwa ila tu muungano wa Kalonzo na Agikuyu, itakuwa hivyo”.

Anasema kuwa “wanasiasa wakijipanga upya katika miungano mipya na wajipambe katika taswira ya kusisimua raia, huenda wakawashangaza Wakenya kwa kuunda ule muungano ambao haukutarajiwa.”

Anasema kuwa ingawa kwa sasa maoni ya wengi ni kuwa “Kalonzo hawezi akaaminika na hata ni mtu anayeweza akakusaliti wakati wowote, bado ni mapema kumtuma kwa pipa taka la kisiasa.

Anaonya kuwa hatari kuu itakuwa hali ambapo wafuasi wa Nasa wafike katika uchaguzi huo wa 2022 wakiwa na hisia za ghadhabu kuhusu usaliti wa Kalonzo katika kiapo cha Odinga na pia wakiwa na ghadhabu kuhusu utawala wa Mlima Kenya.

“Katika hali hiyo, muungano wa Kalonzo na Mlima Kenya ukiwa hauna Ruto ni kigae tu cha kujiwasilisha debeni kwa manufaa ya kuonekana ukiwania. Utashindwa kabla ya saa tatu asubuhi,” asema.

 

‘Wazo butu’

Aliyekuwa mbunge wa Mwingi ya Kati, Joe Mutambo anasema kuwa “hilo ni wazo butu kwa sasa, labda hali imwendee vinginevyo Kalonzo kabla ya 2022, na iwe ni mapema.

Anasema kuwa kwa sasa Kalonzo hana uthabiti mkubwa Ukambani kutokana na kuibuka kwa uasi wa wazi na siasa za kukaidi ukiritimba wa Kalonzo eneo hilo wa kuwafanyia maamuzi.

“Kwa sasa tuko na viongozi limbukeni kama Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua. Kwa sasa, eneo hilo lia wabunge wa Jubilee ambao ni Victor Munyaka wa Machakos Mjini aliyemrambisha sakafu mwaniaji wa Wiper, Ulbanus Mutisya kwa pengo la kura 22, 000.

Kuna wengine ambao ni washirika wa Jubilee wakiwa ni Rachel Nyamai wa Kitui Kusini na pia Vincent Musyoka wa Mwala na pia Charles Kilonzo wa Yatta.

Katika hali hiyo, Kalonzo anaishia kuorodheshwa kama mshirika dhaifu zaidi kwa Mlima Kenya katika kujaribu kuendeleza ukiritimba wa kunyakua urais.