MakalaSiasa

JAMVI: Je, Uhuru amenasa Mudavadi na Weta?

April 7th, 2019 3 min read

PETER MBURU na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta sasa anaoenekana kudhibiti viongozi wote wa upinzani baada ya kuonekana kufaulu kuwanasa viongozi wa vyama vya Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na wa Ford Kenya Moses Wetangula.

Bw Mudavadi ndiye alikuwa amesailia kuwa sauti ya upinzani baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka kuamua kuhiari kufanya kazi na serikali ya Jubilee kwa moyo wa muafaka wa maridhiano, almaarufu ‘Handshake’.

Bw Wetangula pia naye amekuwa akisisitiza kuwa yuko upande wa upinzani, japo miezi kadha iliyopita amekuwa akionyesha ulegevu katika kazi ya upinzani, badala yake aidha akiwa kimya ama kuonekana katika hafla pamoja na viongozi wa serikali ya Jubilee.

Seneta huyo wa Bungoma hajakuwa mkakamavu kuikosoa serikali huku uvumi ukienea mwishoni mwa mwaka jana kwamba anaegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto katika chama tawala, Jubilee.

Mnamo Jumanne, viongozi hao wawili walitumwa na serikali kuongoza uzinduzi wa mpango mpya wa usajili wa watu kijidilitali ‘Huduma Namba’ katika kaunti ya Kajiado, katika shughuli hiyo ambayo kwayo Wakenya wote watapewa nambari maalum, “Huduma Namba” watakayotumiwa kufikia huduma za serikali.

Na kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu wa 2017, mnamo Alhamisi Bw Mudavadi alihudhuria kikao cha pamoja cha bunge kusikiza hotuba ya Rais Kenyatta kuhusu Hali ya Taifa ambapo aliungana na wenzake, Bw Odinga, Musyoka na Wetang’ula kuunga mkono masuala kadhaa ambayo Rais Kenyatta alizungumzia.

Hata hivyo, alitofautiana na serikali kuhusu tangazo la Rais kwamba atafuta kazi wale ambao watafikishwa mahakamani pekee wala sio wale ambao bado wanachunguzwa kwa tuhuma za ufisadi.

Itakumbukwa kwamba baada ya Bw Odinga na Bw Musyoka kuamua kushirikiana na serikali mwaka jana, Bw Mudavadi alishikilia kuwa atasalia kuwa sauti ya upinzani ili kukosoa serikali.

“Sitageuka kuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta kama hao wenzangu. Kama mwasisi wa NASA nitakuwa na umuhimu mkubwa kwa kutoa msimamo mbadala na kuwa mtetezi wa wanyonge,” akawaambia wanahabari.

“Nikitangaza kuwa ninaunga serikali, nitadhibitiwa. Sitakuwa na nafasi ya kuzungumzia masuala kama kupanda kwa madeni ya serikali, masaibu ya wakulima wa mahindi na miwa na ufisadi,” Bw Mudavadi akasema huku akiongeza kuwa msimamo huo haumaanishi kuwa yeye sio mzalendo.

Na mapema mwaka huu kiongozi huyo wa ANC alijitangaza kuwa kiongozi rasmi wa upinzani na kutisha kuitisha maandamano kuishinikiza serikali iwaadhibu vikali maafisa wake waliotajwa katika sakata za ufisadi.

Bw Wetangula naye Alhamisi alisifu hotuba ya Rais, akihimiza asasi za kuchunguza ufisadi sasa kufanya kazi ya ziada ili watu fisadi wakamatwe na kufungwa.

“Hotuba ya Rais imekuwa ya kuunganisha, ya kuunganisha taifa, kubaini makosa ya mbeleni na ya kuahidi kuwa tunahitaji kufanya mengi zaidi ili kuponya taifa tunaposonga mbele,” Bw Wetangula akasema baada ya hotuba hiyo.

Kiongozi huyo aidha aliungama na Rais kuwa idara za kuchunguza kesi za ufisadi zinafaa kupewa nguvu zaidi.

Viongozi hao wawili ndio walikuwa wakionekana kuwa sura halisi ya ufisadi nchini, lakini kwa kuongoza shughuli ya serikali katika kaunti ya Kajiado wiki hii na matamshi yao baada ya hotuba ya Rais, wadadisi wanasema Rais Kenyatta sasa amefaulu kuwaweka “box” viongozi wote wa upinzani na hivyo serikali yake kukosa mkosoaji mkuu.

“Hali hii inaweza kupalilia utawala mbaya na hata kurudisha nyumba vita dhidi ya maovu serikalini kama vile ufisadi,” anaonya Bw Barasa Nyukuri, ambaye ni mtaalamu katika masuala ya uongozi.

Wakati wa hotuba hiyo ya Rais Alhamisi, aliyekuwa mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na ambaye ni mwandani wa karibu wa Rais Kenyatta alimsifia Bw Mudavadi kuwa kiongozi pekee ambaye anaweza kufananishwa na Rais kwa kujitolea kukabiliana na ufisadi.

Bw Murathe alisema japo haoni kiongozi mwingine mwenye uwezo wa kupigana vita dhidi ya ufisadi, anafahamu kuwa Bw Mudavadi anaweza.

“Rais anataka kuacha taifa lililoungana na ni yeye tu mwenye uwezo wa kushinda vita dhidi ya ufisadi. Ana uwezo wa kuvishinda kwa kuwa huu ni muhula wake wa mwisho, hana kitu cha kupoteza na hahitaji kuiba,” akasema.

“Ni yeye tu, kama rafiki yangu huyu (Mudavadi, ambaye alikuwa kando yake) ambaye anaweza kumaliza ufisadi. Na tunatumai kuwa atakayechukua hatamu baada yake ataendeleza vita hivi,” Bw Murathe akasema.

Bw Mudavadi akizungumza hakumlaumu Rais Kenyatta kwa kukosa kumfuta yeyote kazi ama kwa kusema watakaofikishwa kortini ndio watahitajika kujiuzulu, ila shoka lake alilielekeza kwa washukiwa wenyewe.

“Amesema kwamba yeye hatafuta watu, atasubiri waingie kortini, lakini ikiwa wewe umekuwa mgeni wa DCI na umekuwa mgeni wa EACC wewe pia huoni unapeana aibu kwa serikali, na kwa Rais na ujiondoe. Usingoje upelekwe kortini ndio utoke,” akasema kiongozi huyo wa ANC.

Viongozi hao (Murathe na Mudavadi) baadaye walionekana wakicheka na kupiga gumzo nje ya makao ya bunge.

Macho sasa yanaangaziwa Bw Mudavadi ambaye ndiye amekuwa akijitaja kuwa sura ya upinzani na ambaye amekuwa akikosoa serikali tangu mwaka jana baada ya Bw Odinga na Bw Musyoka kunyakuliwa na Rais, kuona ikiwa atashikilia kauli yake kuwa yeye ni kiongozi wa upinzani asiyeweza kunyakuliwa na serikali.