Siasa

JAMVI: Jinsi ilivyo ni siasa za 2022 zitaamua mrithi wa Maraga

December 20th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

SIASA za Uchaguzi Mkuu wa 2022 zitaamua atakayekuwa mkuu wa Idara ya Mahakama ambaye atamrithi Jaji Mkuu David Maraga anayestaafu Januari 12, 2021.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Rais Uhuru Kenyatta atateua mkuu wa Idara ya Mahakama ambaye atakuwa mwaminifu kwake tofauti na Maraga ambaye alikuwa na msimamo mkali.

Japo wanasiasa wa muungano wa NASA wanaonekana kumpigia debe Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kumrithi Maraga, baadhi ya maafisa wa ngazi za juu serikalini wameapa kuhakikisha kuwa anapigwa breki.

Msimamo wake mkali na uhusiano wa karibu na Jaji Mkuu David Maraga umemfanya Naibu Jaji Mkuu Mwilu kuonekana mwiba kwa serikali.

Kabla ya kuenda likizoni, Jaji Mkuu David Maraga alimteua naibu wake Mwilu kuwa kaimu Jaji Mkuu. Uteuzi huo ambao umekosolewa na baadhi ya wanasheria, ulimfanya Jaji Mwilu kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Idara ya Mahakama japo kwa muda.

Siku moja kabla ya Jaji Mkuu Maraga kuenda likizoni, mwanaharakati Okiya Omtatah alienda mahakamani akitaka Naibu Jaji Mkuu Mwilu azuiliwe kushikilia wadhifa huo kwa muda hadi pale atakapoondolewa lawama kuhusu madai ya kuhusika na ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Jaji Mwilu anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi na kukwepa kulipa ushuru.

Kwa mujibu wa Bw Omtatah, kuna malalamishi manne mbele ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) ya kutaka Jaji Mwilu atimuliwe kutokana na matumizi mabaya ya mamlaka yake.

Jaji Mwilu hivi karibuni alifichua kuwa anaandamwa na serikali kutokana na msimamo wake wakati ya kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, 2017 ambapo ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta ulibatilishwa na uchaguzi kurudiwa Oktoba 26, 2017.

“Masaibu yangu yanatokana na jinsi Mahakama ya Juu ilishughulikia kesi ya kupinga matokeo ya urais 2017,” akasema jaji Mwilu kupitia malalamishi yake aliyowasilisha mbele ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) mnamo Disemba, mwaka jana.

Alidai kuwa Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki amekuwa akiandaa vikao kisiri kuunda njama ya kutaka kumng’oa afisini.

“Ninafahamu kwamba mikutano mitatu, iliyohudhuriwa na maafisa wenye ushawishi serikalini, imefanywa ili kupanga njama ya kuniondoa katika Mahakama ya Juu,” akasema Jaji Mwilu kupitia ombi lake kwa JSC kumtaka Mwanasheria Mkuu Kariuki asiruhusiwe kusikiliza kesi ambapo Naibu Jaji Mkuu anakabiliwa na madai ya matumizi mabaya ya mamlaka.

Wadadisi wanasema kuwa kesi hiyo ya Bw Omtatah ni kati ya vikwazo ambavyo Jaji Mwilu anawekewa ili kumzuia kuwa Jaji Mkuu.

Uhusiano wa Jaji Mkuu Maraga na Rais Uhuru Kenyatta ulidorora baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Maraga amekuwa akishutumu serikali ya Rais Kenyatta kwa kutatiza uhuru wa mahakama, kupuuza maagizo ya korti na kupunguza bajeti ya Idara ya Mahakama.

Uteuzi wa majaji

Rais Kenyatta pia amekataa kuidhinisha uteuzi wa majaji 41 waliohojiwa na majina yao kupitishwa na JSC.

Mwanasheria Mkuu ambaye ni mshauri mkuu wa serikali kuhusu masuala ya sheria, amekuwa akitumiwa na serikali kumshambulia Maraga.

Japo hajatangaza hadharani, ripoti zinadai kuwa Kariuki huenda akajitosa kwenye kinyang’anyiro cha kutaka kumrithi Jaji Maraga.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Githu Muigai ametangaza kuwa hana mpango wa kutuma maombi kuwa Jaji Mkuu wa 15 wa Kenya.

Naibu Jaji Mkuu Mwilu pia anatarajiwa kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha kutaka kumrithi Maraga.

“Namtakia kila la heri Jaji Mwilu anapohudumu kama Kaimu jaji Mkuu licha ya kushambuliwa na baadhi ya wakuu serikalini. Tunafahamu kwamba kumekuwa na mvutano mkali kuhusu wadhifa wa Jaji Mkuu lakini wanasheria wataunga mkono mtu jasiri atakayejitolea mhanga kupigania uhuru wa Idara ya Mahakama,” anasema Bw Nelson Havi, Rais wa Chama cha Mawakili nchini (LSK).

Wakili Felix Otieno asema kuwa Mwilu yuko huru kutuma maombi ya kutaka kuwa Jaji Mkuu licha ya kukabiliwa na madai ya kuhusika katika ufisadi.

“Hakuna kinachomzuia Jaji Mwilu kutuma maombi yake kuwa Jaji Mkuu kwani madai yaliyowasilishwa mbele ya JSC hayajathibitishwa,” anasema Wakili Otieno.

Iwapo Jaji Mwilu atawasilisha ombi la kutaka kuwa Jaji Mkuu, Bw Otieno anasema, huenda kukawa na msururu wa watu watakaowasilisha malalamishi katika juhudi za kumzuia kuwa Jaji Mkuu.

“Kadhalika, serikali inaweza kutumia uwezo wake kushawishi wajumbe wa JSC kuhakikisha kwamba Jaji Mwilu hafaulu. Shughuli ya kuteua Jaji Mkuu itaongozwa na masilahi ya Uchaguzi Mkuu wa 2022. Inaonekana serikali haitaki kupitia ‘aibu’ kama iliyoshuhudiwa 2017 ambapo matokeo ya urais yalibatilishwa,” anasema Bw Otieno.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo anasema kuwa mtu anayestahili kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu ni sharti awe na ujasiri kama ule wa Maraga.