JAMVI: Joho atuliza boli uwanja wa siasa ukialika Nassir, Shahbal

JAMVI: Joho atuliza boli uwanja wa siasa ukialika Nassir, Shahbal

VALENTINE OBARA na ANTHONY KITIMO

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, anazidi kujiweka nyuma nyuma kuhusu ubabe wa kisiasa Pwani wakati ambapo vuta nikuvute yaendelea kushuhudiwa kati ya Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal.

Mabw Nassir na Shahbal wanamezea mate tikiti ya Chama cha ODM kuwania ugavana wa Mombasa mwaka ujao wakati kipindi cha Bw Joho kitakapotamatika.

Kufikia sasa, Bw Joho hajatangaza mwanasiasa ambaye angependelea achukue nafasi yake na hali hii imewafanya wawili hao kujizatiti kujaribu kuthibitisha wametosha kukalia kiti hicho.

Wawili hao wamekuwa wakifuatana na viongozi wakuu wa ODM hasa Bw Odinga na Bw Joho hadharani na faraghani, hata wanapoendeleza mikutano na wananchi mashinani.

Tofauti na jinsi ilivyokuwa katika miaka iliyopita ambapo Bw Joho ndiye alikuwa akisimamia hafla kubwa za kisiasa au kuwakilisha Mombasa na hata Pwani katika hafla nyingine za kisiasa nje ya eneo hilo, gavana huyo ameonekana kuwaachia Mabw Nassir na Shahbal nafasi kabla wakutane katika debe la kupigania tikiti ya ODM kuwania ugavana mwaka ujao.

Hivi majuzi, baadhi ya wandani wa Bw Joho ambao ni madiwani Mombasa waliambia Taifa Jumapili kuwa Bw Joho ameamua kusudi kutoingilia mashindano ya wawili hao kwani msimamo wake unaweza kumharibia sifa alizopata kufikia sasa kisiasa.

Wiki iliyopita, Bw Shahbal alisafiri kwa ndege moja na Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt Oburu Oginga ambaye ni ndugu mkubwa wa Bw Odinga kwa hafla Kaunti ya Murang’a.

Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho akiwa na mfanyabiashara maarufu Suleiman Shahbal (kulia). Picha/ Maktaba

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba walisafiri pamoja kwa hafla hiyo ya wanamuziki ambayo mgeni wa heshima alikuwa Bw Odinga, aliyeandamana na wanasiasa mbalimbali wakiwemo wabunge, maseneta, na magavana kutoka maeneo tofauti ya nchi.

“Shahbal pekee ndiye alikuwa kiongozi kutoka Pwani ambaye aliandamana na ‘Baba’ kwa hafla ya Murang’a. Alisafiri na Oburu Oginga kwa helikopta moja,” mdakuzi wetu akasema.

Bw Oginga huwa ni mmoja wa washauri wakuu wa kinara wa ODM na hivyo basi safari yake na Bw Shahbal ingeonekana kama mojawapo ya mikakati ya mfanyabiashara huyo kutafuta uungwaji mkono kwa Bw Odinga kupitia kwa ndugu yake.

Hii ni licha ya jinsi Bw Odinga husisitiza kuwa, chama chake kitaandaa kura ya mchujo kwa njia huru na ya haki ili yeyote anayetaka tikiti ya kuwania ugavana Mombasa apimane nguvu na wenzake debeni.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, Bw Shahbal alisema alihudhuria hafla hiyo kwa mwaliko wa kinara wa ODM.

“Nilipokea mwaliko kutoka kwa Bw Odinga ili niende Murang’a. Mkutano huo ulikuwa ni wa kupanga mikakati na tuliona hitaji la kuwa hapo. Nilikuwa nawakilisha eneo letu kwa msingi wa mwaliko niliopokea,” akasema Bw Shahbal.

Jukumu hilo la kuwakilisha Mombasa au Pwani kwa jumla katika hafla zinazohusiana na ODM zamani lilikuwa la Bw Joho, ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama.

Wakati Bw Odinga alipofanya ziara kaunti za Pwani hivi majuzi, ni Bw Nassir ambaye alikuwa katika mstari wa mbele kuandamana naye katika maeneo tofauti walikofanya mikutano ya hadhara.

Bw Joho alijitokeza wakati Bw Odinga alipohudhuria hafla ya kusherehekea Idd-Ul-Adha mjini Mombasa.

Hafla hiyo ambayo miaka iliyopita ilikuwa ikiandaliwa na gavana, mwaka huu iliandaliwa na Bw Nassir na hii ikawa ishara nyingine ya jinsi Bw Joho anavyozidi kujiondolea majukumu ya kusimamia siasa za Pwani.

Lakini Bw Nassir alisema anapoonekana akikutana na Bw Odinga au Bw Joho, haifai kuchukuliwa kwamba anataka wamtangaze kuwa ndiye ametosha kukalia kiti cha gavana.

“Uhusiano wangu wa karibu na Bw Odinga na Bw Joho haufai kuchukuliwa kumaanisha kuwa nataka waniunge mkono. Ninapotembea nao huwa ni kwa manufaa ya umoja wa chama. Wapigakura pekee ndio wanaweza kunichagua,” akasema Bw Nassir.

Katika hotuba zake, Bw Joho ambaye tayari alituma ombi kwa ODM kuwania tikiti ya kushindania urais, husisitiza kwamba lengo lake ni kujitosa katika siasa za kitaifa kwa hivyo amewaachia wengine nafasi ya kuongoza siasa za eneo hilo.

“Hivi karibuni nitaelekea kwa siasa za kitaifa nitawaachia hawa kina Abdulswamad washindane huku chini,” alisema Bw Joho katika mojawapo ya hafla alizohudhuria majuzi.

Bw Nassir amekuwa akitumia mafanikio yake ya ubunge Mvita kama kigezo kikuu cha kutafuta uungwaji mkono kwa siasa za ugavana.

Kufikia sasa, azimio lake limeungwa mkono na wabunge wengi wa Mombasa.

Kwa upande mwingine, azimio la Bw Shahbal limeungwa mkono na wandani wa karibu wa Bw Joho wakiwemo washauri wa kisiasa na madiwani.

Ni hali hii ambayo iliibua gumzo kuhusu uwezekano wa kuwa Bw Joho anamuunga mkono Bw Shahbal kisiri, ingawa gavana huyo husema ameacha uwanja uwe wazi.

Mfanyabiashara huyo aliwania ugavana mwaka wa 2013 na 2017 kupitia Chama cha Wiper na Jubilee mtawalia lakini hakufanikiwa kushinda.

Alihama Jubilee hivi majuzi lakini wiki iliyopita ilifichuka hajakamilisha mpango wa kuhamia ODM jinsi alivyokusudia.

Kando na wawili hao tikiti ya ODM kuwania ugavana yamezewa mate pia na Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi.

Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko ambaye awali alitaka kuwania ugavana kupitia ODM, baadaye alibadili nia na sasa anaunga mkono azimio la Bw Nassir.

Viongozi wengine ambao wanatarajiwa kuwania ugavana wa Mombasa mwaka ujao ni aliyekuwa seneta, Bw Hassan Omar na Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo.

Wawili hao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto ambaye amepanga kuwania urais kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

You can share this post!

JAMVI: Vizingiti vya Raila kugeuzwa kuwa mradi wa Uhuru

JAMVI: Namna Raila anapanga kuyumbisha akina OKA