Siasa

JAMVI: Joto la BBI lamtia Ruto kibaridi

December 6th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto anataka Wakenya wapigie kura kila hoja iliyomo katika mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) ili kujinusuru kisiasa, imebainika.

Naibu wa Rais anahofia kuwa umaarufu wake wa kisiasa huenda ukadorora iwapo Wakenya watatakiwa kupigia mswada mzima wa BBI kura ya ‘Ndiyo’ au ‘La’.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Dkt Ruto ameshindwa kuchukua msimamo kuhusiana na mswada wa BBI kutokana na hofu ya kupoteza umaarufu kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Lakini wanaonya kuwa Dkt Ruto atafifisha umaarufu wake kisiasa katika kipindi cha miezi mitano ijayo, iwapo atakosa kuunga au kupinga BBI.

Iwapo Dkt Ruto ataamua kuunga mkono BBI, wadadisi wanasema, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga hawatampa fursa ya kuendesha kampeni hivyo kukosa kuonekana.

“Tayari mswada wa BBI umewezesha wapinzani wa Dkt Ruto kama vile Bw Odinga na Seneta wa Baringo Gideon Moi kupenya katika maeneo ya Mlima Kenya ambayo Naibu wa Rais anategemea pakubwa kupata kura kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa 2022,” anasema wakili Felix Otieno.

Bw Odinga, Jumatano alishuhudia shughuli ya ukusanyaji wa saini kwa ajili ya mswada wa BBI katika eneo la Kangare, eneobunge la Kigumo, Kaunti ya Murang’a.

Alhamisi, Bw Moi alizuru Kaunti ya Embu kupigia debe mswada wa BBI – hatua ambayo imefanya wadadisi kuhisi kuwa kiongozi huyo wa Kanu ameanza kujinoa kisiasa.

Baada ya kufanya mkutano wa takribani saa saba mnamo Jumatano iliyopita, Naibu wa Rais alitoa orodha ya matakwa kuhusu marekebisho ambayo anataka yafanywe kwenye mswada wa BBI.

Dkt Ruto anataka kila hoja ipigiwe kura na Wakenya huku akishikilia kuwa kupigia kura mswada mzima kura ya ‘Ndiyo’ au ‘La’ kutanyima wananchi fursa ya kutupilia mbali baadhi ya masuala wasiyoyataka.

Pendekezo hilo la Dkt Ruto linamaanisha kwamba Wakenya watachagua tu mambo wanayotaka; kwa mfano kuongezwa kwa mgawo wa fedha kwa kaunti kutoka asilimia 15 hadi 35, na kutupilia mbali mengine wanayohisi kwamba hayafai kama vile kuongezwa kwa idadi ya wabunge.

Mswada wa BBI una zaidi ya mambo 70 ambayo unapendekeza yarekebishwe. Endapo pendekezo la Dkt Ruto litazingatiwa, karatasi ya kura itakuwa na maswali 70 ambayo Wakenya watatakiwa kuyajibu kwa kuandika ‘ndiyo’ au ‘la’.

Naibu wa Rais pia alipendekeza kuwa kura ya maamuzi kurekebisha Katiba ifanywe pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 2022 huku akisema kuwa hatua hiyo itazuia ubadhirifu fedha.

Kulingana na Dkt Ruto, hakuna haja ya kutumia Sh14 bilioni katika kura ya maamuzi mwaka ujao na kisha kutumia fedha nyingine Sh42 bilioni kuandaa Uchaguzi Mkuu 2022.

Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Emmanual Wangwe anasema kuwa matakwa hayo ya Naibu wa Rais ni ishara kwamba anajitayarisha kupinga mswada wa BBI.

Naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe pia ameshutumu vikali Naibu wa Rais kwa kujaribu kutatiza juhudi za kutaka kurekebisha Katiba zinazoongozwa na Rais Kenyatta.

“Ikiwa kweli Dkt Ruto anaunga mkono BBI mbona hakujitokeza na kutia saini yake hadharani kama walivyofanya viongozi wengine? Shughuli ya kukusanya saini ilifungwa Alhamisi bila Dkt Ruto kujitokeza,” Bw Murathe akaambia Taifa Jumapili.

Alhamisi, Naibu wa Rais alisema kuwa hatapinga BBI hata kama matakwa yake hayatatekelezwa.

“Tayari pendekezo lililokuwa katika mswada wa BBI kutaka vyama vya kisiasa viteue makamishna wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) limetupiliwa mbali. Hiyo ni ithibati kwamba matakwa yetu yamejumuishwa. Lakini hatutapinga BBI hata kama baadhi ya matakwa yetu hayatajumuishwa,” akasema Dkt Ruto katika mahojiano na runinga moja ya humu nchini, Alhamisi.

“Iwapo Rais Kenyatta na Bw Odinga watakubali kila suala lililomo ndani ya mswada wa BBI kupigiwa kura itakuwa afueni kwa Naibu wa Rais. Hatua hiyo itamwezesha Dkt Ruto kuzunguka kote nchini akipigia debe masuala anayoyataka huku akihimiza Wakenya kukataa baadhi ya vipengele.

“Hata ikiwa baadhi ya masuala ambayo Dkt Ruto anayaunga mkono yatakataliwa na Wakenya, mengine yatapitishwa. Hivyo hatahisi kwamba amepoteza. Lakini akipinga mswada mzima wa BBI na Wakenya wapitishe, huo ndio utakuwa mwisho wake wa kisiasa na itakuwa vigumu kwake kuwania urais 2022,” anasema Bw Otieno.

Huku Dkt Ruto akijaribu kukwepa kampeni ya kupinga BBI, Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, mwanauchumi David Ndii pamoja na wanaharakati wa mashirika mbalimbali ya kijamii wameapa kuongoza vuguvugu la kupinga jaribio la kurekebisha Katiba.

Tayari Prof Kibwana ameenda katika Mahakama ya Juu akitaka kujua ikiwa watumishi wa serikali wanafaa kujihusisha na mchakato wa kufanyia marekebisho Katiba na kutumia rasilimali za umma.

“Iwapo vuguvugu hilo litaendesha kampeni ya ‘La’, Bw Odinga na Bw Moi watapata fursa ya kuzunguka kote nchini kupigia debe BBI. Hatua hiyo itawapa umaarufu kisiasa. Wakati huo huo, Dkt Ruto hatakuwa anaonekana kwa kuwa hatatumwa popote kuenda kupigia debe BBI,” anasema Prof Macharia Munene, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa.