MakalaSiasa

JAMVI: Kalonzo kona mbaya, awazia kuungana na Ruto

November 10th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Huenda kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, akajipata katika hali ngumu kisiasa iwapo hatabadilisha mbinu zake kufuatia hatua ya magavana watatu kutoka ngome yake ya Ukambani kumchangamkia kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Wadadisi wanasema kwamba taswira iliyojitokeza wakati magavana wa Ukambani Charity Ngilu, Alfred Mutua na Kivutha Kibwana walipojiunga na Bw Odinga kwenye kampeni za ODM, katika uchaguzi mdogo wa Kibra, ni kwamba Bw Musyoka anatengwa katika ngome yake na kutemwa na mshirika wake mkuu katika siasa za kitaifa.

Kuanzia 2013, Bw Musyoka amekuwa akishirikiana na Bw Odinga katika siasa za kitaifa huku akitegemea umaarufu wake kama msemaji wa jamii ya Wakamba.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuungana kwa magavana hao kumpiga vita kunaweza kuyeyusha imani ya viongozi wengine wa kisiasa nchini kwa Bw Musyoka wakati wa kubuni miungano ya kisiasa.

“Bw Musyoka hafai kupuuza muungano wa magavana hao. Anafaa kuuchukulia kuwa tishio kwa maisha yake ya kisiasa kwa sababu ni umaarufu wake katika ngome yake unaovutia viongozi wa maeneo mengine kuungana naye,” asema mdadisi wa siasa Albert Kiilu.

Mdadisi huyu anahisi kwamba hatua ya magavana hao kuunga mgombeaji wa chama cha ODM kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra ilikuwa ni sawa na kumsuta Bw Musyoka ambaye chama chake kiliunga mgombeaji wa chama cha Ford Kenya Khamisi Butichi.

Baadhi ya wadadisi wanasema hatua ya magavana hao ilidhihirisha kuwa wamejitolea kwa hali na mali kumhujumu kisiasa Bw Musyoka.

“Nasema ni hujuma kwa sababu walianza mashinani katika ngome ya Bw Musyoka ya Ukambani na wakatumia uchaguzi mdogo wa Kibra kumwonyesha kuwa wana uwezo wa kumzima katika siasa za ngazi ya kitaifa,” asema Bw Kiilu.

Ingawa chama cha Wiper ndicho chama kikubwa Ukambani, magavana hao wameapa kubadilisha siasa za eneo hilo na wanaonekana kupata nguvu baada ya chama cha Maendeleo Chap Chap cha Dkt Mutua kushinda uchaguzi mdogo wa wadi ya Mutonguni, Kitui, kaunti ya nyumbani ya Bw Musyoka.

“Nina hakika ushindi wa Maendeleo Chap Chap uliwapa nguvu magavana hao wakaamua kukweza uhasama wao wa kisiasa na Bw Musyoka kutoka mashinani hadi kitaifa fursa ambayo ilijitokeza katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra,” alisema Bw Kiilu.

Ilisemekana kuwa Bw Odinga alimrai Dkt Mutua kumsaidia kwenye kampeni ili jamii ya Wakamba inayoishi Kibra impigie kura mgombeaji wa chama chake Imran Okoth. Wiper hakikuwa na mgombeaji kwenye uchaguzi huo.

Kulingana na Dkt Stephen Maweu, mdadisi wa siasa za Ukambani, kuna hisia kwamba hatua ya magavana hao kuungana na Bw Odinga, ililenga kudhihirisha kuwa amemtaliki kisiasa Bw Musyoka.

“Ninachofahamu ni kwamba Bw Musyoka amekuwa akitangaza kuwa chama chake kinatandaza mabawa yake kutafuta washirika wapya wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Hisia kuwa Bw Odinga amemtema Bw Musyoka kisiasa sio geni na hazifai kuchukuliwa kupima umaarufu wake kwa wakati huu,” aeleza Dkt Maweu.

Hata hivyo, anasema Bw Musyoka anafaa kubadilisha mbinu za kisiasa kuondoa taswira kwamba umaarufu wake Ukambani umefifia.

“Ni kweli magavana hao wanalenga kumpiga vita Bw Musyoka na wanataka kuchochea hisia za watu kwa kumsawiri kama mtu asiye na umaarufu katika ngome yake. Lakini ni kweli pia kati ya magavana watatu wa Ukambani, wawili wanahudumu vipindi vya mwisho na umaarufu wao utapungua wakiondoka mamlakani.

“Ni kweli pia magavana hao hawatoki chama kimoja ilhali Wiper ina mizizi Ukambani ikiwa na wabunge na madiwani wengi na itakuwa kibarua kuitikisa,” asema Dkt Maweu.

Kubadilisha Mbinu

Wadadisi wanasema iwapo Bw Musyoka hatabadilisha mbinu, huenda akajikwaa mapema katika azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi wa 2022.

“Inaonekana hasimu wake mkuu kisiasa eneo la Ukambani, Dkt Mutua, ameamua kumkabili katika ngazi ya kitaifa kwa kushirikiana na Bw Odinga. Itabidi Bw Musyoka atumie uzoefu wake wa kisiasa kujipanga upya huku akidumisha umaarufu wake Ukambani,” alisema Bw Kiilu.

Dkt Mutua amekutana mara mbili na Bw Odinga baada ya handisheki akisema amekumbatia muafaka huo unaolenga kuunganisha Wakenya.

Hata hivyo, wadadisi wanasema hii ni mbinu ya kutaka kujisawiri kama msemaji wa jamii ya Wakamba, hatua ambayo imekuwa chanzo cha uhasama kati yake na Bw Musyoka.

Kulingana na aliyekuwa mbunge wa Kathiani Wavinya Ndeti, Bw Musyoka angali kigogo wa kisiasa na msemaji wa jamii ya Wakamba.

“Msitishwe na sarakasi za watu wachache ambao wanajipiga kifua wakidhani wanaweza kujitawaza kuwa wasemaji wa jamii. Tuna kiongozi wetu ambaye ni Bw Musyoka,” alisema.

Duru zinasema kuwa Bw Musyoka amekuwa akizungumza na viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa akiwepo Naibu Rais William Ruto kwa lengo la kubuni muungano wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Sio lazima chama cha Wiper kiungane na Bw Odinga wanavyodhani mahasimu wa Bw Musyoka. Tuna mikakati yetu, kuanzia mashinani hadi kitaifa na hata kimataifa ambayo inaendelea na wakati ukifika, watajua hawajui,” alisema mbunge mmoja wa Wiper aliyeomba tusitaje jina lake.