MakalaSiasa

JAMVI: Kenya haina vyama thabiti kisiasa kama mataifa mengi Afrika

February 16th, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Rais Uhuru Kenyatta huenda akadumisha utamaduni wa marais wa Kenya wa kuhama vyama vya kisiasa kila baada ya miaka mitano ikiwa chama cha Jubilee kitasambaratika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Ingawa kikatiba anapaswa kuondoka mamlakani baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili, huenda akaacha chama cha Jubilee kikiwa gae ikiwa migogoro ya ndani kwa ndani haitasuluhishwa kwa amani.

Wadadisi wanasema nchini Kenya, vyama vya kisiasa havina mifumo thabiti ya kuviwezesha kudumu na kutawala kwa muda mrefu kama ilivyo katika mataifa mengine barani Afrika.

“Vyama vya kisiasa Kenya huwa ni vya misimu. Lengo huwa ni kushiriki uchaguzi. Viongozi wa vyama huwa hawana nia ya kujenga vyama thabiti na ndio maana huwa havidumu kwa miaka mingi mamlakani kama mataifa mengine.

“Havina sera na malengo ya muda mrefu. Hii ni kwa sababu huwa vinaundwa kwa misingi dhaifu ya kimaeneo na kikabila,” asema mchanganuzi wa siasa, Benard Some.

“Funzo hapa ni kuwa katika jamii yenye makabila mengi kama Kenya, vyama vya kisiasa huwa vya kikabila pia,” asema.

Katika kipindi chake cha kwanza cha urais mwaka 2013, Rais Kenyatta alitumia chama cha The National Alliance (TNA) alichodadia dakika za mwisho kutoka chama cha KANU alichotumia kugombea urais mara ya kwanza 2002.

Wakati huo aliunda muungano na chama cha United Republican Party (URP) kilichokuwa cha naibu rais William Ruto kubuni muungano wa Jubilee. Siku chache kabla ya uchaguzi wa 2017, aliunda chama cha Jubilee baada ya kuvunja TNA na URP.

Kwa sasa Jubilee kinakubwa na mizozo ya ndani inayotishia kukisambaratisha. Mtangulizi wake, Mwai Kibaki, aliingia mamlakani mwaka wa 2002 kupitia chama cha National Rainbow Coalition (NARC) ambacho kilikuwa muungano wa vyama tofauti. Kwenye uchaguzi wa 2007, Kibaki alitumia chama cha Party of National Unity (PNU) kutetea kiti chake.

Wadadisi wanasema Kenya inakosa vyama thabiti vya kisiasa vilivyo na ufuasi kitaifa kama mataifa mengine ya Afrika.

Tangu 1977, Tanzania imetawaliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichoundwa baada ya Tanganyika kuungana Zanzibar. Kulingana na mtaalamu wa vyama vya kisiasa Mwaura Chege, CCM kimedumu mamlakani kwa sababu ya kuwepo na mfumo thabiti kuanzia mashinani hadi kitaifa.

“Hata baada ya Tanzania kukumbatia mfumo wa vya vingi vya kisiasa 1995, CCM kimekuwa kikishinda kwa urahisi kwa sababu ya mfumo wake wa kuteua wagombeaji urais. Kwa sasa kuna marais watatu wastaafu nchini Tanzania walio hai ambao waling’atuka baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili kila mmoja,” asema Bw Chege.

Anasema hii ni tofauti na Kenya ambapo kuna rais mmoja mstaafu aliye hai na ambaye alitumia vyama tofauti kila muhula aliotawala.

“Umaarufu wa chama cha Kanu kilichotawala kwa miaka 40 tangu uhuru hadi 2001 ulififia kwa sababu ya kutokuwa na mfumo thabiti wa uteuzi,” asema Bw Chege.

Ingawa Uganda hufuata demokrasia tofauti na Kenya ambapo vyama vya kisiasa huwekewa mipaka na kukadamizwa, chama cha National Resistance Movement cha Rais Yoweri Museveni kimekuwa mamlakani kwa miaka zaidi ya 30 kwa sababu ya mfumo wake.

“Ukweli ni kuwa nchini Uganda, NRM ni maarufu maeneo mengi nchini humo kwa sababu ya mfumo wake wa kudumisha uaminifu wa wanachama,” aeleza Bw Chege.

Mataifa mengine ambayo vyama vya kisiasa vimetawala wa miaka mingi kwa sababu ya kuwa na mifumo thabiti ya uteuzi ni African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini.

Ingawa Afrika Kusini ina matatizo yake, ANC kimehimili mawimbi kuanzia rais wa kwanza mweusi Nelson Mandela hadi rais wa nne mweusi Ceril Ramaphosa.

Hali ni sawa katika nchi ya Zimbabwe ambapo chama cha Zimbabwe African National Union Freedom Party (ZANU PF) kimetawala kwa miaka mingi, Namibia ambapo chama cha South West African Peoples Organisation (SWAPO) kimetawala tangu uhuru.

Kulingana na Bw Some, huenda Jubilee kikakosa kushinda uchaguzi mkuu ujao iwapo migogoro inayokikumba itaendelea.

“Ili chama cha kisiasa kiweze kudumu kwa miaka, ni lazima kiwe na mfumo wa kudumisha nidhamu na kutatua mizozo ya ndani kwa ndani.

“Ni lazima kiongozi wake awe msitari wa mbele kuhakikisha nidhamu alivyokuwa akifanya Moi Kanu kilipokuwa mamlakani. Kwa wakati huu, vyama vya kisiasa Kenya ni kama kampuni za watu binafsi wanaoweza kuzifunga wakitaka,” aeleza.

Kulingana na Institute of Democracy and Electoral Assistance (IDEA), demokrasia thabiti na ya kudumu hutegemea vyama thabiti vinavyosimamiwa vyema.

“Hata hivyo, kote ulimwenguni, vyama vya kisiasa hujipata katika mizozo, umaarufu kupungua na kukosa kuaminiwa. Hii inatokana na mifumo duni ya usimamizi na ukosefu wa demokrasia ya ndani,” aeleza katibu mkuu wa IDEA Vidar Helgesen kwenye utangulizi katika ripoti ya utafiti kuhusu vyama vya kisiasa barani Afrika iliyochapishwa mwaka jana.

Kuna uwezekano wa Rais Kenyatta kuungana na viongozi wengine wanaounga mpango wa maridhiano (BBI) kuunda chama cha kitaifa au muungano mpya wa kisiasa kabla ya 2022.