JAMVI: Kibarua kwa Ruto Mlimani Tangatanga wakitunga masharti

JAMVI: Kibarua kwa Ruto Mlimani Tangatanga wakitunga masharti

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto anakabiliwa na kibarua kipya kuendeleza ushawishi wake katika ukanda wa Mlima Kenya, baada ya wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ kuorodhesha matakwa ambayo wanataka ayatimize ikiwa eneo hilo litamuunga mkono katika azma yake ya urais 2022.

Ingawa wabunge hao wanasisitiza kwamba matakwa hayo si masharti kwa Dkt Ruto, imeibuka kuwa huenda kuna mkono wa nje uliowashawishi kuchukua hatua hiyo.

Swali jingine ambalo limeibuka ni sababu yao kuorodhesha masuala hayo wakati huu, ikizingatiwa wamekuwa wakimpigia debe katika sehemu mbalimbali nchini kwa karibu miaka mitatu.

Masuala hayo yalijumuishwa kwenye kikao kilichofanyika katika makazi ya mbunge Rigathi Gachagua (Mathira), mtaani Karen, jijini Nairobi, wikendi. Kikao hiki kilihudhuriwa na wabunge 48 kutoka kaunti 11 za ukanda huo.

Miongoni mwa matakwa hayo ni kumtaka Dkt Ruto kubuni mikakati ya kufufua uchumi wa eneo hilo, hasa sekta ya kilimo kama majanichai, kahawa, pareto na sekta ya ufugaji.

Vile vile, wanamtaka abuni utaratibu utakaozuia makazi ya watu kubomolewa bila mpangilio maalum.

Mbali na hayo, wanamtaka abuni mkakati utakaohakikisha kwamba Wakenya wanaoagiza bidhaa zao za kibiashara kutoka nje wanalindwa dhidi ya kuhangaishwa na idara kama Halmashauri ya Kukusanya Ushuru (KRA).

Ingawa viongozi hao walisema “walijumuisha matakwa ya wananchi kwanza”, imebainika pia kuwa wanamshinikiza Dkt Ruto kuwapa nafasi ya mgombea-mwenza na kuwatengea nyadhifa kadhaa za uwaziri zenye ushawishi mkuu serikalini.

Ili kuzingatia utaratibu rasmi, tayari wamebuni kamati maalum itakayowasilisha masuala hayo kwa Dkt Ruto.

Kamati Kuu inawajumuisha Bw Gachagua, Seneta Mithika Linturi (Meru), Kimani Ichungw’a (Kikuyu), Alice Wahome (Kandara), Seneta John Kinyua (Laikipia), Beatrice Nkatha (Tharaka Nithi), Faith Gitau (Nyandarua), Wangui Ngirichi (Kirinyaga) na Bi Cecily Mbarire (mbunge maalum).

Kamati itakayoendesha masuala ya kiuchumi inawajumuisha wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), John Kiarie ‘KJ’ (Dagoretti Kusini), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Seneta Susan Kihika (Nakuru), George Kariuki (Ndia) na John Muchiri (Manyatta).

Katika mkakati huo, wabunge walieleza kwamba licha ya kumfanyia kampeni Dkt Ruto, lengo lao ni kuwa na “mazungumzo rasmi” yatakayoamua vile wenyeji watafaidika kwa kumuunga mkono.

Ukubalifu

“Kufikia sasa, ni wazi kwamba tumemuuza Dkt Ruto kwa watu wetu na hatuna shaka wamemkubali. Hata hivyo, lazima pawe na mazungumzo rasmi kuhusu vile watakavyofaidika kwa kuunga mkono azma yake kuwa rais,” akasema Bw Gachagua.

Mbunge huyo alisema serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imekosa kuwasaidia wenyeji wa ukanda huo, licha ya rais kuwa mmoja wao.

“Sisi hatujali kuhusu nyadhifa tutakazopata. Hakikisho letu kwanza ni kuona wafuasi wetu wana pesa mifukoni mwao kinyume na sasa ambapo kila mmoja analia kutokana na sera kandamizi za serikali dhidi ya wananchi, hali ambayo imeongeza umaskini,” akasema.

Hata hivyo, hatua hiyo imekosolewa vikali na mrengo wa ‘Kieleweke’, unaosema viongozi hao wanajitwika mamlaka ambayo si yao, kwani msemaji na mwakilishi mkuu kisiasa wa Mlima Kenya ni Rais Kenyatta.

Wadadisi wa siasa wanaeleza kuwa ingawa mkakati huo ni hatua nzuri ya kisiasa kwa Dkt Ruto kudumisha ushawishi katika ukanda huo, bado kuna kibarua kikubwa kilicho mbele ya wabunge hao.

Mchanganuzi wa siasa Wycliffe Muga anasema hadi kufikia sasa, Rais Kenyatta bado ana ushawishi mkubwa katika eneo hilo, hivyo itakuwa kibarua kigumu kuwarai wenyeji kubadili misimamo yao kisiasa.

“Ushawishi wa Rais Kenyatta ulidhihirika alipoandaa kikao kwa siku kadhaa katika Ikulu Ndogo ya Sagana mnamo Februari, kujaribu kuwarai wenyeji kuunga mkono ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI). Usemi wake ulionekana kuzingatiwa kwani karibu madiwani wote katika mabunge ya kaunti eneo hilo waliipitisha ripoti. Hilo liliashiria wazi kwamba bado Rais ana usemi na ushawishi mkubwa,” akasema Bw Muga.

Kauli kama hiyo ilitolewa na wakili Wahome Mwangi, ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa, aliyeeleza kuwa ni kinaya kwa wabunge hao kuanza kutaja matakwa watakayomwasilishia Dkt Ruto, ikizingatiwa taswira ambayo imekuwepo kwamba tayari wamekubaliana kuhusu hatua watakazochukua kulainisha hali Mlima Kenya.

Mbali na hayo, anasema wabunge hao wanajitwika majukumu mazito, bila kufahamu ikiwa watachaguliwa tena au la.

“Ingawa maana halisi ya siasa ni kubuni taswira na kuonyesha imani kwa hatua unazochukua, uhalisia uliopo miongoni mwa wenyeji wengi ni kwamba Rais Kenyatta bado ndiye kiongozi na msemaji wao. Hivyo, yeyote anayeonekana kubuni njia tofauti ni mwasi na ‘adui’ wao,” akasema.

Mbunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri) anataja mkakati huo kama “hadaa” kwa wenyeji Mlimani, hasa ikizingatiwa kwamba serikali ya Rais Kenyatta bado inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama barabara.

“Baadhi ya wabunge hao hata hawana ushawishi wowote katika ngome zao. Je, ni miujiza ipi watafanya kuwashawishi wenyeji kumuunga mkono Dkt Ruto? Wanamhadaa!” akasema Bw Wambugu.

Mbunge Kanini Keega (Kieni) alisema ukanda huo utangoja sauti ya Rais Kenyatta kuhusu mwelekeo utakaofuata 2022, wala si “uvamizi wa kisiasa kutoka nje.”

“Hatua ya Rais kunyamaza haimaanishi hajui yanayoendelea. Anatazama kwa kina,” akasema Bw Kega.

You can share this post!

Betis wadidimiza matumaini ya Real Madrid kuhifadhi ufalme...

JAMVI: IEBC yawaniwa kutekwa nyara kabla ya kura 2022