MakalaSiasa

JAMVI: Kilele cha Ruto kumkaidi Uhuru

April 7th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Hatua ya Naibu Rais William Ruto ya kukaidi maagizo kadhaa ya Rais Uhuru Kenyatta ni mbinu ya kuonyesha kwamba amechoshwa na chama cha Jubilee na anajipanga kivyake kuelekea uchaguzi mkuu ujao, wadadisi wanasema.

Wachanganuzi na wanasisasa wa ndani na nje ya chama cha tawala wanasema kwamba hatua yake ya kususia hafla ya kuzindua usajili wa Wakenya kwa njia ya kielektroniki na kujitokeza kwa vijana waliovalia jezi za rangi ya kilichokuwa chama chake huko Kiambu wiki jana ni kilele cha kumkaidi Rais Kenyatta kwa kushirikiana na viongozi wa upinzani.

Wanasema tabia hii imekuwa ikiendelea kwa muda ndani ya kipindi cha pili cha utawala wa Jubilee na haimfurahishi Rais Kenyatta na washauri wake.

Kuna dalili kwamba uwezekano kwama Dkt Ruto anapanga kuhama Jubilee na kutumia chama kingine kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya chama cha Jubilee kukubwa na misukosuko ya ndani.

Inasemekana kuwa Dkt Ruto alianza kwenda kinyume na maagizo ya Rais Kenyatta punde tu baada ya kuapishwa kwa kipindi cha pili kwa kuzuru maeneo tofauti nchini jambo lililomfanya Rais kumuonya dhidi ya kutangatanga.

Kwa upande wake, Ruto anasisitiza kuwa kama Naibu Rais ana jukumu la kuzuru maeneo tofauti kukutana na wananchi na kuendeleza ajenda za serikali japo mikutano aliyofanya na anayoendelea kufanya huwa ya kisiasa.

Wito wa rais kwa wanasiasa ulikuwa waache siasa na kuelekeza juhudi zao kutekeleza Ajenda Nne Kuu za serikali yake. Hata hivyo, Bw Ruto na washirika wake wanaendelea kuzungumzia siasa za uchaguzi mkuu wa 2022.

Dkt Ruto aliendelea kutembelea maeneo tofauti kuzindua miradi ya maendeleo licha ya Rais kusimamisha miradi mipya hadi ile ya zamani ikamilishwe.

Kulingana na Bw Ruto, ana haki ya kuzindua miradi kwa sababu hiyo ndiyo kazi ya serikali anayohudumia na ambayo alitekeleza wajibu mkubwa kuhakikisha iliingia mamlakani.

Rais alipotangaza muafaka wake na kiongozi wa upinzani Raila Odinga mnamo Machi 9, 2019, alisema nia yao ilikuwa ni kuunganisha Wakenya wote na haukulenga siasa za 2022.

Aliwataka viongozi wote kuungana na kuhubiri amani ili kujenga madaraja ya urafiki wajenge nchi yao pamoja.

Wadadisi wanasema japo kabla ya muafaka huo Dkt Ruto alikuwa akikaidi Rais, yeye na wandani wake wa kisiasa walizidisha tabia hiyo baada ya muafaka huo ambao wanahisi unalenga kuzima ndoto yake ya kumrithi Rais Kenyatta.

“Ukifuatilia matamshi na vitendo vya Dkt Ruto na wandani wake baada ya muafaka kutangazwa, utagundua kuwa wamekuwa wakaidi kwa Rais Kenyatta na serikali wanayohudumu,” asema mdadisi wa siasa Nelson Mugambi.

“Ni bayana wamekuwa wakipinga hatua kadhaa za serikali hatua ambayo wandani wa Rais wanahisi kwamba zinalenga kuhujumu utendakazi wa serikali na kumfanya Rais Kenyatta kuonekana kama kiongozi aliyefeli,” aongeza Bw Mugambi.

Dkt Ruto hakuchangamkia handisheki ambayo amekuwa akiitaja kama ndoto licha ya Rais kuungwa mkono na wanasiasa wa mirengo tofauti. Hisia zake ni kuwa Bw Odinga anatumia handisheki kujipenyeza katika serikali na kuvunja chama cha Jubilee.

Mwaka jana, Rais alipotangaza kuwa mitindo ya maisha ya maafisa wa serikali itakaguliwa, Bw Ruto na washirika wake walipinga na kudai ni yeye aliyekuwa akilengwa.

Dkt Ruto pia amepinga vita dhidi ya ufisadi licha ya Rais Kenyatta kuapa kwamba vitaendelea. Huku Rais akisifu idara za upelelezi wa jinai na mashtaka kwa kuzidisha vita hivi, Dkt Ruto anadai kwamba vimeingizwa siasa.

Kulingana na Dkt Ruto, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) na mwenzake wa Mashtaka ya Umma (DPP) wanatumiwa kutekeleza ajenda za kisiasa katika vita dhidi ya ufisadi.

“Mtu akitofautiana na mkubwa wake kuhusu jambo fulani kama vile Ruto anavyotofautiana na Rais Kenyatta kuhusu masuala kadhaa huwa anachukuliwa kuwa mkaidi,” asema Bw Mugambi.

Anasema Rais amejipata katika njia panda kwa sababu hana mamlaka ya kumfuta naibu wake hata akimkaidi.

“Dkt Ruto anafahamu kwamba katiba inamkinga hivi kwamba hawezi kufutwa. Aidha, anafahamu kwamba mchango wake katika ushindi wa chama cha Jubilee ni mkubwa. Kwa ufupi, amemfanya Rais kuwa mateka wake na hii ndio imemfanya kwenda kinyume na maagizo ya rais,” asema.

Wadadisi wanasema kwamba kwa kuendelea kukaidi hatua na maamuzi ya serikali anayohudumia, kuna kitu ambacho Dkt Ruto analenga.

“Ukweli wa mambo ni kuwa ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ulizua mgawanyiko katika Jubilee na hii haikuwa ajali. Dkt Ruto anahisi kwamba wapinzani wao kwenye uchaguzi mkuu uliopita hawafai kushirikishwa serikali naye Rais anahisi kwamba ni jukumu lake kuunganisha Wakenya wote,” asema.

Kulingana na wadadisi, Dkt Ruto hafurahishwi na mabadiliko ya hali ya siasa nchini tangu Rais Kenyatta na Bw Odinga walipoanza kushirikiana na anahisi kwamba ametengwa katika serikali ya Jubilee.

Akiwa Kisii wiki jana, alidai kwamba kuna njama fiche kwenye muafaka na kwamba anajua kinachoendelea.

“Mnafikiri mimi ni mjinga. Ikiwa ni maendeleo tuyafanye kwa nia njema. Hauwezi kutumia salamu kunitisha. Niko tayari kwa mapambano. Najua wanapanga njama lakini tuko tayari,” alisema Bw Ruto.

Mwishoni mwa wiki jana, kundi la vijana waliovalia jezi za rangi ya majano ya kilichokuwa chama chake cha United Republican Party (URP) ambacho alivunja wakati wa kuunda chama cha Jubilee walijitokeza kaunti ya Kiambu alikohudhuria ibada na harambee.

“Hiki kilikuwa kilele cha ukaidi au uasi katika chama cha Jubilee. Ulikuwa ujumbe kwamba anajua rangi ya chama chake au ulikuwa ujumbe kwake kwamba anaweza kufufua chama chake na kuhama Jubilee,” asema Dkt Shadrack Owino, mdadisi wa kisiasa.

Wiki hii Dkt Ruto alisusia hafla ya kuzindua usajili wa Wakenya kwa njia ya kielektroniki ambayo Rais Kenyatta, mawaziri na viongozi wa upinzani walishiriki.