MakalaSiasa

JAMVI: Kimya cha vigogo wa kisiasa Pwani chatisha wafuasi

September 1st, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

KIMYA cha vigogo wa kisiasa eneo la pwani kimeshangaza wengi huku mikutano ya viongozi wanaomezea urais eneo hilo ikipungua.

Joto la kisiasa eneo hilo limetulia huku magavana Hassan Joho wa Mombasa, Amason Kingi wa Kilifi na Salim Mvurya wa Kwale wanaohudumu vipindi vyao vya mwisho wakiamua kuzingatia zaidi masuala ya kaunti zao.

Bw Joho na Bw Kingi waliashiria kuwa watagombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 huku wito ukitolewa eneo la pwani kuungana na kutoa mgombea urais mmoja chini ya jumuiya ya kaunti sita za eneo hilo.

Wadadisi wanasema hatua ya Bw Joho na Bw Kingi ya kuunga muafaka kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ilituliza joto la kisiasa eneo hilo.

Bw Kingi na Bw Joho walichaguliwa kwa tiketi ya chama hicho cha Chungwa na wana ushawishi mkubwa eneo la pwani. Bw Mvurya alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Jubilee.

Wawili hao walikuwa wakikosoa serikali kabla ya kiongozi wa chama chao, Raila Odinga kusalimiana na Rais Uhuru Kenyatta, wamekuwa kimya.

Mwaka jana na mapema mwaka juu, siasa zilichacha eneo la pwani kufuatia ziara ambazo Naibu Rais alikuwa akifanya eneo hilo ambapo wabunge kadhaa wa upinzani walitangaza kumuunga mkono.

Wadadisi wanasema kupungua kwa ziara za Dkt Ruto pwani kumechangia hali ya sasa ya kisiasa eneo hilo. “Kuna hisia kwamba Dkt Ruto haungi muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga na kwa sababu ya matunda ya handisheki, wanasaisa wa pwani waliamua kumuambaa ili wasiwaudhi viongozi hao,” alisema mbunge mmoja wa Kaunti ya Kwale ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Katika ziara zake eneo la pwani, Dkt Ruto alikuwa akimlaumu vikali Bw Odinga kwa kupanga njama ya kuvunja chama cha Jubilee huku akiungwa na baadhi ya wabunge wakiwemo wa ODM.

Wabunge hao akiwemo mbunge wa Malindi Aisha Jumwa wameonekana kutuliza boli japo ODM kilimfukuza chamani kwa kumuunga Dkt Ruto. Mahakama ilizuia kutumuliwa kwake.

Kulingana na Bw Ezekiel Katana, mdadisi wa miaka mingi wa siasa za Pwani, viongozi wa eneo hilo wameonekana kutii wito wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wa kuepuka siasa.

“Ninavyojua ni kwamba kuna mikutano inayofanyika ya kuandaa mikakati ya 2022 eneo la pwani lakini kwa sasa kuna kila dalili kwamba kutulia kwa siasa eneo hilo kunatokana na handisheki,” asema.

Anasema kwamba hatua ya wanasiasa wa eneo hilo kuacha kutoa cheche za kisiasa imechangia utulivu wa sasa.

“Lakini wakazi hawajaridhika kwa sababu wanahisi kwamba wamekosa mwelekeo wa kisiasa kufuatia kimya cha viongozi wao huku wale wa maeneo mengine wakizungumza,” asema.

Mdadisi huyo anasema kwamba mikakati inayofaa ni ya kuweka msingi wa eneo hilo kutoa mgombea urais mmoja kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge wa pwani wamekuwa wakitofautiana kuhusu kiongozi anayestahili kuwania urais katika uchaguzi wa 2022 kati ya Bw Joho na Bw Kingi.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya wakati mmoja alinukuliwa akilaumu wenzake wa kaunti hiyo wanaomuunga Joho akisema wanasaliti Kaunti yao.

Bw Kingi amekuwa msitari wa mbele kuunganisha wakazi wa pwani katika hatua ya kujiandaa kuwaania urais, hatua ambayo wanaomuunga Joho wanatilia shaka.

Wanaomuunga Bw Joho wakati mmoja walimtaka aungane na waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i kugombea urais pamoja.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa siasa za eneo la Pwani huenda zikabadilika baada ya kuibuka kuwa umaarufu wa chama cha ODM eneo hilo umedidimia.

Wadadisi wanasema kwamba, kimya cha vigogo wa kisiasa eneo hilo siku za hivi majuzi ni ishara kwamba linaweza kugeuza mwelekeo wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na utafiti wa hivi punde wa kampuni ya Infotrak, umaarufu wa chama cha ODM katika eneo la Pwani umeshuka hadi asilimia 21 kutoka 50.

Kulingana na Bw Katana, kumekuwa na juhudi za kuunda chama kitakachowakilisha maslahi ya wakazi wa pwani na viongozi wamekuwa wakijadiliana.

“Nafikiri kufuatia muafaka huo, viongozi wa pwani waliamua kutulia ili kujipanga bila kuanika mambo yao. Utagundua kwamba siku hizi hata wabunge wa eneo hilo waliokuwa wakiunga viongozi wa kitaifa wametuliza boli,” asema.

Wabunge Owen Baya (Kilifi North) Paul Katana (Kaloleni) Khatib Mwashetani (LungaLunga), Aisha Jumwa (Malindi) na Suleiman Dori (Mswambweni) ambao walikuwa wakimuunga Naibu Rais William Ruto wamepunguza mikutano ya hadhara.

Wakati wa sherehe za Madaraka mwaka 2019, magavana Joho, Kingi na mwenzao wa Kwale Salim Mvurya walihimizwa kuungana kabla ya 2022.

“Wakati umefika sisi kama Wapwani kuamua mwelekeo wetu wa kisiasa na tunaweza kufanya hivi kwa kuungana,” alisema mbunge wa Kisauni Ali Mbogo.