Siasa

JAMVI: Kitakachomlazimu Ruto kuipinga BBI

October 25th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto amejipata katika njiapanda kuhusiana na ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) itakayozinduliwa rasmi kesho katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Dkt Ruto ambaye amekuwa akipinga mchakato wa BBI, ni miongoni mwa wageni walioalikwa kuhudhuria uzinduzi huo.

Mmoja wa wandani wa Naibu wa Rais alidokezea ukumbi huu kwamba Dkt Ruto atahudhuria.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti ya kwanza ya BBI uliofanyika katika ukumbi huo mnamo Novemba mwaka jana, Naibu wa Rais alihudhuria japo alionekana kukerwa.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa Naibu Rais atakuwa na kibarua kigumu kuwashawishi Wakenya kukataa mswada wa ripoti ya BBI unaolenga kurekebisha Katiba ya 2010. Hii inatokana na ‘chambo’ ambacho Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga wameficha ndani ya ripoti hiyo ili kuwanasa Wakenya wa matabaka na janibu mbalimbali.

Miongoni mwa mambo ambayo yanaonekana kuwavutia Wakenya ndani ya BBI ni kuongezwa kwa fedha zinazotolewa kwa serikali za kaunti kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 35.

Kubuniwa kwa hazina ya ustawishaji wa Wadi pia kutawezesha madiwani kupitisha mswada huo bila kupoteza wakati.

Ili kunasa vijana, mswada wa BBI unapendekeza vijana wanaoanzisha biashara kupata afua ya kutolipa ushuru kwa kipindi cha miaka saba.

Vijana walionufaika na fedha kutoka kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Vyuoni (HELB) pia watatakiwa kuanza kulipa miaka minne baada ya kuhitimu.

Hiyo ni tofauti na sasa ambapo walionufaika wanaanza kulipa mwaka mmoja baada ya kukamilisha masomo yao.

Ili kuwavutia wanawake, mswada huo unapendekeza kuwa kila kaunti itawachagua maseneta wawili; mwanamke na mwanaume.

Katika mikutano ambayo Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakihutubu tangu kukabidhiwa ripoti hiyo katika Kaunti ya Kisii mnamo Jumatano iliyopita, viongozi hao wamekuwa wakiorodhesha ‘mazuri’ yaliyomo ndani ya BBI kuhusu vijana, wanawake, ugatuzi na kadhalika.

Naye Dkt Ruto amekuwa akihimiza vijana kukataa ripoti ya BBI akishikilia kuwa mswada huo unalenga kuwezesha mabwanyenye kujiundia nafasi zaidi za uongozi serikalini.

Lakini katika hafla ya kuwapokeza Rais Kenyatta na Bw Odinga ripoti hiyo, wiki iliyopita, Naibu Rais alioonekana kuanza kulegeza msimamo kwa kutaka kujumuishwa katika mjadala wa kuwaunganisha Wakenya.

Naibu wa Rais tayari amedokeza kuwa hataki kufanya kampeni mbili; ya kura ya maamuzi na Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Kuna uwezekano kwamba Dkt Ruto huenda akakosa kupinga au kuunga mkono BBI. Akipinga na Wakenya wapitishe mswada wa BBI, hatakuwa na nguvu za kuwania tena urais mwaka wa 2022 kwa sababu watu hao hao waliopitisha katiba hiyo ndio bado watakaopiga kura ya urais,” anasema wakili Felix Otieno.

Wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen na Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika, wameshikilia kuwa watapinga mswada huo wa BBI.

Mbunge wa Soy Caleb Kositany anasema iwapo mswada wa BBI utapitishwa jinsi ulivyo, utawatwika mzigo mzito walipa-ushuru.

Anasema kuwa bunge la Seneti lilifaa kufutiliwa mbali badala ya kuongeza idadi ya maseneta maradufu hadi 94.

Bw Kositany ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, pia anasema kuwa kuongezwa kwa mgao wa kaunti hadi asilimia 35 ya mapato hakutawezekana.

“Uchumi wetu ungali dhaifu, hauruhusu serikali ya kitaifa kutoa asilimia 35 kwa serikali za kaunti. Itabidi serikali ya kitaifa iachane na baadhi ya majukumu yake,” anasema.

Lakini Bw Otieno anasema kuwa jaribio la kupinga mgao wa asilimia 35 litafanya Naibu wa Rais kupoteza umaarufu.

Wakili Nzamba Kitonga aliyeongoza kamati ya wataalamu walioandika Katiba ya 2010, anasema kuwa mswada wa BBI ni tiba ya makosa yaliyofanywa kwenye sheria hiyo miaka 10 iliyopita.

“Mswada wa BBI umerejesha mapendekezo ambayo yalitupiliwa mbali katika kongamano la Naivasha wakati wa majadiliano ya Katiba mpya. Kulikuwa na mapendekezo ya kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu pamoja na manaibu wake wawili lakini pendekezo hilo lilitupiliwa mbali,” akasema.

“Pendekezo la kuchagua seneta wa kiume na wa kike ni zuri kwani linaleta usawa wa jinsia,” anasema Bw Kitonga.

Prof Macharia Munene, mhadhiri wa masuala ya kisiasa, anasema kuwa Naibu wa Rais akipinga mswada wa BBI, atachukuliwa kuwa ‘adui’ wa vijana ambao amekuwa akionekana kuwapigania.

“Naibu wa Rais akiunga mkono BBI, ataingia kwenye mtego wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Rais Kenyatta ataenda nyumbani baada ya kukamilisha muhula wake wa pili. Naye Bw Odinga hajatangaza ikiwa anataka kuwania urais 2022 au la. Wawili hao wana njama fiche ambayo Naibu wa Rais haijui. Hivyo itakuwa hatari kwa Ruto kuunga mkono ripoti ambayo wafadhili na wadhamini wake hawajafichua namna wanavyotaka kunufaika,” anaongezea.