Siasa

JAMVI: Kitakachosababisha Sonko kutimuliwa sawa na Waititu

December 13th, 2020 4 min read

Na CHARLES WASONGA

JAPO mashtaka dhidi ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko sasa yatasikizwa na maseneta wote 67 katika kikao maalum alivyotaka gavana huyo, kuna uwezekano mkubwa hoja ya kumtimua afisini itaidhinishwa.

Hii ni kwa sababu maafisa wakuu katika serikali kuu na baadhi ya mabwanyenye katika jiji la Nairobi wameungana kuhakikisha kuwa Bw Sonko anavuliwa wadhifa huo alivyofanyiwa aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu Babayao.

Maafisa wakuu katika Ikulu ya Rais na matajiri hao, wengi wao kutoka eneo la Mlima Kenya wamekerwa hatua ya gavana huyo kukiuka mkataba uliobuniwa Idara za Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) Februari mwaka huu.

Hii ni licha ya kwamba Bw Sonko mwenyewe alitia saini mkataba huo ambao majukumu manne makuu ya serikali ya kaunti ya Nairobi yaliwekwa chini ya usimamizi wa serikali kupitia NMS inayoongozwa na Meja Jenerali Mohamed Badi. Majukumu hayo ni kama vile, Afya, Uchukuzi, Mipango na Ujenzi na usimamizi wa idara za usafi na maji.

Kimsingi, Sonko aliamua kuhujumu utendakazi wa NMS, kinyume cha ushauri wa Rais Uhuru Kenyatta, kwa kudinda kutia saini bajeti iliyoitengea Sh27.7 bilioni.

Alidai asasi hiyo inatumiwa na maadui wake wa kisiasa kuwa kuhujumu serikali yake kupitia hatua yake ya kuingilia majukumu yake ambayo hayakuhamishwa hadi serikali kuu, kama vile Elimu na Usimamizi wa Idara ya Fedha.

Lakini akiongea katika kongomano la vijana katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Jumanne wiki iliyopita, Rais Kenyatta alisifu utendakaji wa NMS akisema umebadili sura ya Nairobi na kuimarisha utoaji huduma kwa wakazi.

“Ndani ya miezi tisa pekee tangu kubuniwa kwa NMS, inayosimamiwa na mwanajeshi, idara hii imeweka kujenga upya barabara ya umbali wa kilomita 4000 katika jiji la Nairobi. Zaidi ya hayo, imechimba visima vya maji katika mitaa kadhaa ya mabanda hali ambayo imewezesha wakazi kupata maji bila malipo, tofauti na zamani ambapo walikuwa wakinunua maji kwa bei ya Sh20 kwa mtungi wa lita 20. Kwa hivyo, ningependa kuwaambia wale ambao wanapinga utendakazi wa wanajeshi kukubali kuwa wao wenyewe walishindwa na kazi kama hii,” akasema Rais.

Unga Badi

Wadadisi wa maswala ya kisiasa wanasema kuwa ikizingatiwa kuwa Rais Kenyatta alitoa kauli hii siku chache baada ya madiwani wa kaunti ya Nairobi kupitisha hoja ya kumtimua afisini Bw Sonko, hiyo ilimaanisha kuwa kiongozi wa taifa aliunga mkono hatua hiyo.

“Hatima ya Sonko tayari imeamuliwa. Rais ameonyesha kuwa hatalegeza msimamo wake wa kutaka kuona kwamba NMS inafanikiwa katika utendakazi wake. Hii ndio maana Gavana Sonko ambaye ameonekana wazi kuwa kizingiti, sharti aondolewe alivyofanyiwa aliyekuwa Gavana wa Nairobi Ferdind Waititu Januari mwaka huu,” anasema Bw Martin Andati.

Kulingana mdadisi huyo, mashtaka dhidi ya Sonko yatashughulikiwa sawa na yalivyofanyiwa mashtaka ya Waititu ambapo mawili wa upande wa utetezi walitishwa na kupelekea wao kukanganyikiwa “kiasi cha kushindwa kutetea kikamilifu mteja wao.”

“Isitoshe, katika kesi ya Bw Waititu maseneta wa mirengo miwili walionyesha kutii matakwa ya Ikulu ambayo ilikuwa kwamba kiongozi huyo avuliwe wadhifa huo. Hali kama hii bila shaka itashuhudiwa mnamo Alhamisi na Ijumaa wiki hii wakati wa mjadala kuhusu mashtaka dhidi ya Bw Sonko,” akaeleza.

Mabwanyenye

Kwa upande wake, Bw Javas Bigambo anasema masaibu ya Sonko pia yanachochewa na mabwanyenye jijini Nairobi ambao wamekerwa hatua ya kiongozi huyo kuwanyima zabuni katika serikali yake.

“Matajiri hawa hawampendi Sonko kwa sababu aliwakatizia mifereji ya fedha kupitia zabuni. Alipoongia mamlakani aliapa kupambana na ufisadi katika idara ya utoaji zabuni, hatua ambayo iliwakwaza watajiri hao kwani iliyowanyima nafasi ya kupata zabuni,” anasema.

“Lakini kinaya ni kwamba hatua hiyo ilimweka Sonko pabaya kwani amejipata akishtakiwa kwa ufisadi baada ya kubainika kwamba alishawishi utoaji zabuni za kima cha Sh345 milioni kwa marafiki zake. Hii ndio maana wakati huu anakabiliwa na kesi za ufisadi mahakamani,” anaongeza Bw Bigambo.

Madai ya ukiukaji wa Sheria za utoaji wa zabuni za umma na matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake ni miongoni mwa mashtaka yaliyomo kwenye hoja iliyopitishwa na madiwani mnamo Desemba 3, 2020 na ambayo itachambuliwa na maseneta kuanzia Alhamisi wiki hii.

Dalili kwamba mabwanyenye wanachochea kutimuliwa kwa Bw Sonko zilidhihirika siku chache zilizopita kupitia kauli za Mbunge Maalum Maina Kamanda.

Mbunge huyo ni mzaliwa wa Murang’a alinukuliwa akisema kuwa Gavana Sonko anafaa kutimuliwa ikizingatiwa kuwa hakuhitimu kimasomo na kimaadili kuongoza kaunti ya Nairobi kama Gavana.

“Huyu ni mtu ambaye alilazimishiwa wakazi wa Nairobi na Naibu Rais William Ruto ili kuendeleza masilahi yake (Ruto). Hii ndio maana alipekea kazi kwa kampuni ambazo zilifanya kazi chapwa ambayo sasa inarekebishwa na idara ya NMS,” Bw Kamanda akanukuliwa akisema.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta pia alidai kuwa baadhi ya kampuni ambazo zilipewa zabuni katika serikali ya kaunti ya Nairobi, kupitia ushawishi wa Sonko, hazikuhitimu na “zinamilikiwa na marafiki wake.”

Bw Kamanda alitoa mfano wa kampuni moja ya bima inayohusishwa na Dkt Ruto kama mojawapo ya zile ambayo Sonko alitumia kufyonza fedha za umma kwa kuzipa zabuni.

Kampuni hiyo (tunalibana jina lake) ni moja ya zile ambazo zimetajwa katika kesi za ufisadi zinazomkabiliwa Sonko.

Endapo Sonko atatimuliwa, Spika wa Bunge la Nairobi Benson Mutura ndiye atashikilia wadhifa huo kwa siku 60 kutoa nafasi kwa kufanyika kwa uchaguzi mdogo kujaza nafasi hiyo.

Hii ni kwa sababu Sonko alidinda kuteua Naibu Gavana tangu Polycarp Igathe alipojiuzulu mnamo Januari 2018.

Jaribio lake la kumteua Bi Anne Kananu Mwendwa mwaka jana lilikabiliwa na changamoto baada ya mchakato wa kumpiga sasa kusimamishwa na Mahakama Kuu

Hoja ya kumwondoa afisini Bw Sonko ilipitishwa na katika bunge la naibu kwa kuungwa mkono na madiwani 88 kati ta 122 wa bunge la kaunti ya Nairobi.

Hoja hiyo ilidhaminiwa na kiongozi wa wachache Michael Ogada.

Wengi wa madiwani walipiga kura kwa njia ya mtandaoni wakati wa kikao baada ya mjadala kuhusu hoja hiyo.

Ni madiwani wawili pekee walipinga hoja hiyo.

Kulingana na hoja hiyo, Bw Sonko aliondolewa mamlakani kwa matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake, mienendo mibaya, kudinda kuidhinisha bajeti iliyotengea Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) Sh27.7 bilioni na kutokuwa na uwezo kimwili na kiakili kuendesha shughuli za serikali ya kaunti hiyo.

Maseneta 47 watahitajika kupigia kura mashtaka hayo moja baada ya nyingine. Endapo 24 kati yao wataidhinisha hata shtaka moja pekee, Sonko atakuwa ametimuliwa. Hata hivyo, atasalia na nafasi ya kukataa rufaa mahakamani.