MakalaSiasa

JAMVI: Kuondolewa kwa noti ya Sh1,000 pigo kwa kampeni za 2022

June 9th, 2019 3 min read

 Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Benki Kuu ya Kenya (CBK) kuzindiua noti mpya na kubatilisha matumizi ya noti ya sasa ya Sh1,000 kuanzia Oktoba 1, mwaka huu, itaathiri pakubwa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na wadadisi, hatua hiyo ya CBK ni pigo kwa wanasiasa ambao hutumia mabilioni ya fedha kuwahonga wapigakura ili wawachague.

Mahojiano ya kina yaliyofanywa na ‘Jamvi’ imebainika kuwa baadhi ya wawaniaji haswa wa urais, ugavana na hata ubunge wameanza kujilimbikizia mamilioni ya fedha kujiandaa kwa ajili ya kampeni za 2022.

Duru pia zinadokeza kuwa hatua ya CBK kuondoa noti ya Sh1,000 imezua hofu miongoni mwa baadhi ya wanasiasa licha ya kuonekana kuiunga mkono katika majukwaa ya kisiasa.

Ripoti iliyotolewa na CBK kwa ushirikiano na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) kuhusu hali ya uchumi ya familia nchini, inaonyesha kwamba asilimia 23 ya Wakenya wamehifadhi fedha katika maeneo ya kisiri.

Ripoti hiyo iliyotolewa Aprili, mwaka huu, hata hivyo, haikufichua kiasi kilichofichwa na watu hao.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale wiki iliyopita alidai kuwa hatua ya CBK kuondoa noti ya Sh1,000 inalenga Naibu wa Rais William Ruto ambaye amekuwa akitoa mamilioni katika harambee makanisani.

Gavana wa CBK Patrick Njoroge Jumamosi iliyopita, aliwataka Wakenya kuhakikisha kuwa noti za Sh1,000 zinarejeshwa katika benki na kupewa mpya.

Dkt Njoroge alisema serikali iliamua kuondoa noti za Sh1,000 za sasa kama njia mojawapo ya kukabiliana na ufisadi, ulanguzi wa fedha, ugaidi na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Hiyo inamaanisha kwamba wanasiasa walio na marundo ya fedha nyumbani wakingojea kuzitumia katika kampeni kuwashawishi wapigakura sasa watalazimika kuzirejesha fedha hizo katika benki ili wapewe sarafu mpya.

“Watakapozirejesha katika benki itakuwa vigumu kwao kuzichukua tena, kwani watatakiwa kuelezea wanachotaka kwenda kuzifanyia. Masharti ya CBK pia yanahitaji mteja kupata idhini kutoka kwa meneja wa benki kabla ya kutoa zaidi ya Sh1 milioni yatatumika,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Wahasibu nchini (CPAK), Edwin Makori.

Mteja anayeweka katika akaunti yake zaidi ya Sh1 milioni atahitajika kuelezea chanzo cha fedha hizo na hata kutoa ushahidi.

Iwapo mteja atakataa kufichua chanzo, basi benki itatakiwa kuripoti kwa Kituo cha Kupokea Ripoti kuhusu Uhalifu wa Kifedha.

Juhudi za wabunge kutaka kuzima masharti hayo mnamo Februari ziligonga mwamba baada ya Dkt Njoroge kusisitiza kuwa kanuni hizo zinaambatana na matakwa ya taasisi za kifedha za kimataifa.

Kifungu cha 33 cha Sheria ya Benki kinaipa CBK mamlaka ya kubuni kanuni za kudhibiti uwekezaji na utoaji wa fedha kutoka katika akunti ya benki.

Kabla ya uchaguzi wa 2017, Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilipiga marufuku chama cha kisiasa kutumia zaidi ya Sh15 bilioni katika kampeni.

IEBC iliwataka wawaniaji wa urais kutumia kiasi kisichozidi Sh5.2 bilioni, wawaniaji wa ugavana, useneta na mwakilishi wa kike jijini Nairobi waliruhusiwa kutumia fedha zisizozidi Sh423 milioni.

Wawaniaji wa ubunge na madiwani waliagizwa kutumia fedha zisizozidi Sh33 milioni na Sh10 milioni mtawalia katika kampeni zao.

IEBC ilionya kuwa wanasiasa au chama ambacho kingekiuka masharti hayo kingepigwa faini ya Sh2 milioni au kifungo cha miaka isiyozidi mitano gerezani.

Hata hivyo, masharti hayo ya IEBC kuhusu hela za kampeni yalitupiliwa mbali na wabunge kutokana na kigezo kwamba kanuni zilizokuwa zikitumiwa na tume ya uchaguzi hazikuidhinishwa na bunge.

Wabunge walisema kwamba kanuni za IEBC zilikuwa na mapungufu hivyo hazingeweza kutumiwa katika uchaguzi wa 2017.

Uamuzi huo wa bunge ulitoa mwanya kwa wanasiasa kutumia mamilioni ya fedha kusaka viti bila kizuizi.

Ripoti ya shirika la kijamii la Coalition for Accountable Political Financing linakadiria kwamba Rais Uhuru Kenyatta alitumia Sh30 bilioni katika uchaguzi wa 2017 huku kinara wa Upinzani Raila Odinga akitumia Sh10 bilioni kabla ya kujiondoa katika marudio ya uchaguzi wa urais duru ya pili.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi ameelezea nia yake ya kuwasilisha mswada bungeni unaotaka wanasiasa wanaotoa zaidi ya Sh100,000 katika harambe kupasha habari Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.