JAMVI: Kusambaratika kwa NASA huenda itakuwa nafuu au kitanzi kwa Raila

JAMVI: Kusambaratika kwa NASA huenda itakuwa nafuu au kitanzi kwa Raila

Na CHARLES WASONGA

VITA vya maneno vilivyotokea majuzi kati ya vigogo wa muungano wa upinzani (NASA), Raila Odinga kwa upande mmoja na Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi kwa upande wa pili ni ishara ya kusambaratika kwa ndoa ya kisiasa kati ya wanasiasa hao.

Hii ni baada ya Bw Odinga kudinda kuunga mkono mmoja wao katika kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao kwa msingi kuwa ni waoga na walimtelekeza alipokula “kiapo” kuwa “Rais wa Wananchi” katika bustani ya Uhuru Park, Nairobi mnamo Januari 31, 2018.

Kwenye mahojiano katika runinga moja ya humu nchini, Bw Mudavadi alisema kuwa japo NASA ingalipo kisheria “imekufa kivitendo” na sasa washirika wake wako mbioni kusuka muungano mwingine wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

“Raila amethibitisha wazi kwamba yeye ni mwanasiasa ambaye hawezi kuaminika. Ikiwa hawezi kudumisha mkataba uliobuni NASA, basi hatuwezi kushirikiana naye tena katika uchaguzi mkuu ujao. Mimi na wenzangu Kalonzo Musyoka, Moses Wetang’ula na Gideon Moi tunajenga muungano mwingine kwa sababu ninaamini kuwa chama kimoja hakiwezi kushinda uchaguzi nchini,” kiongozi huyo wa chama cha Amani National Congress (ANC) alieleza.

Hizi ni habari njema kwa Naibu Rais William Ruto ambaye anamchukulia Bw Odinga kuwa mpinzani wake mkuu katika kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Kenyatta, mwaka ujao.

Bw Odinga alitarajia kutumia mchakato wa BBI kurejesha ukuruba kati yake na vigogo wenza wa NASA ikizingatiwa kuwa wote watatu, akiwemo Seneta Moi, wanaunga mkono marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa chini ya mpango huo.

Kwa mujibu wa wadadisi wa kisiasa, Dkt Ruto na Bw Odinga ndio wanapigiwa upatu kumrithi Rais Kenyatta.

Hii ni licha ya kwamba kiongozi huyo wa ODM hajatangaza waziwazi kwamba atawania urais. Ameahidi kutoa mwelekeo wake kuhusu suala hilo baada ya kura ya maamuzi kuhusu Mswada wa BBI. Lakini wandani wake wa karibu, miongoni mwao; James Orengo (Seneta wa Siaya) na Junet Mohammed (kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa) wameshikilia kuwa Bw Odinga atakuwa debeni kuwania urais 2022.

Hii ndiyo maana baadhi ya wadadisi wa kisiasa wanaamini kuwa talaka katika NASA ni pigo kubwa katika azma ya Bw Odinga kwa sababu ilitarajiwa kuwa Rais Kenyatta angemuunga mkono baada ya kukosana na Naibu wake Dkt Ruto.

Hata hivyo, kuna dhana kuwa kusambaratika kwa NASA kunamweka huru Bw Odinga kusaka ndoa nyingine ya kisiasa kwa ajili ya kufanikisha ndoto yake ya kuingia Ikulu. Inasemekana sharti aandae mikakati mipya haswa itakayomwezesha kunasa kura nyingi za eneo la Mlima Kenya ili aweze kufidia kura ambazo zitamtoka baada ya kukosana na vigogo wenzake katika NASA.

Juzi Bw Odinga alifanya mazungumzo na Gavana wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) Dkt Mukhisa Kituyi; ishara tosha kwamba anasaka marafiki wengine wa kisiasa.

Lakini Bw Javas Bigambo anashikilia kuwa kwa kukosana na vigogo wenzake katika NASA, Mbw Mudavadi, Musyoka na Wetang’ula, Bw Odinga amepoteza pakubwa ikizingatiwa kuwa watatu hao wana ufuasi mkubwa kutoka jamii zao.

“Ukweli ni kwamba Kalonzo Musyoka angali mfalme wa kisiasa wa Ukambani. Mbw Mudavadi na Wetang’ula pia wana ushawishi si haba katika eneo la Magharibi. Kura za kutoka maeneo mawili, Pwani na Nairobi ndizo zilizomfaa zaidi Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2017. Kupotea kwa sehemu ya kura hizo bila shaka ni pigo katika azma yake ya kwenda Ikulu,” anasema mchanganuzi huyo wa masuala ya kisiasa.

Kulingana na Bw Bigambo, itakuwa hatari zaidi kwa Bw Odinga kutegemea kura za eneo la Mlima Kenya kwa sababu dalili zaonyesha kuwa huenda Dkt Ruto akapata sehemu kubwa ya kura hizo.

“Ni kweli kwamba Raila anaweza kutumia ukuruba wake na Rais Kenyatta kupata sehemu za kura kutoka eneo la Mlima Kenya. Hata hivyo, hakuna uhakika kuwa hilo litafanyika kwa sababu baadhi ya wakazi wamemuasi Rais na kuegemea mrengo wa Dkt Ruto,” anasema.

Bw Martin Andati anakubaliana na kauli ya Bw Bigambo lakini anasema huenda nyota ya kisiasa ya Bw Odinga ikang’aa katika eneo la Mlima Kenya kwa mara nyingine kutokana na kupitishwa kwa Mswada wa BBI katika mabunge ya kaunti zote 10 katika eneo hilo.

“Kabla ya Rais Kenyatta kuandaa mkubwa wa Sagana III ambao naamini ndio ulichangia kupitishwa kwa Mswada wa BBI katika mabunge ya kaunti za Mlima Kenya, Bw Odinga alikuwa hana chake kisiasa katika eneo hilo. Lakini sasa baada ya kupitishwa kwa mswada huo nyota yake huenda ikang’aa eneo hilo,” anaeleza Bw Andati ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Wakati kama huu ambapo vumbi la kupitishwa kwa Mswada wa BBI halijatulia, Bw Andati anamshauri Odinga kuandamana na Rais Kenyatta katika kampeni za kuvumisha mchakato wa marekebisho ya Katiba katika eneo la Mlima.

“Mkakati kama huu utamsaidia Bw Odinga kuvuna uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya. Anapasa kujinadi kama mmoja wa waasisi wa BBI na hivyo ndiye anayeweza kufanikisha utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo kwenye mswada wa BBI baada ya Rais Kenya kuondoka mamlakani,” anaeleza.

Kwa upande wake aliyekuwa kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale anasema kuwa muungano uliobuniwa na Mudavadi, Musyoka, Wetang’ula na Seneta Moi, ni butu na hauwezi kumtikisa Bw Odinga.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini, ambaye zamani alikuwa mshirika wa karibu wa Bw Odinga, anasema kusambaratika kwa NASA kumemwondolea kiongozi huyo wa ODM “mzigo wa kisiasa”

“Kwetu katika kambi ya Ruto, mshindani wetu mkuu ni Raila. Sioni ni kwa nini watatu hao wamsumbue Raila wakimtaka aidhinishe mmoja wao ilhali kiongozi huyo wa ODM yu kinyang’anyironi? Hii inaonyesha kuwa Kalonzo, Mudavadi na Wetang’ula hawana uwezo na nguvu za kusimama kivyao pasina kushikiliwa,” Duale akaeleza kwenye mahojiano na Jamvi la Siasa.

Mwanasiasa huyo anaamini kuwa Bw Odinga ana uwezo na mikakati ya kusuka muungano mwingine thabiti bila usaidizi wa wenzake.

You can share this post!

Newcastle United na mbwa-mwitu Wolves nguvu sawa kwenye...

JAMVI: BBI yaacha Tangatanga Mlima Mkenya kwenye njiapanda...