MakalaSiasa

JAMVI: Kushindwa kudhibiti Pwani ni dalili Joho hatoshi kuwania Urais 2022

March 31st, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

MVUTANO unaendelea kati ya serikali ya Gavana Hassan Joho na bunge la kaunti hiyo huenda ikaathiri ndoto zake za kisiasa haswa ndoto yake ya kuwania urais mwaka wa 2022, baadhi ya wadadisi wanaonya.

Kilele cha mzozo huo kilikuwa na kufurushwa afisini kwa Waziri wa Uchukuzi na Miundo Msingi na Ujenzi Tawfiq Balala kutokana na kile madiwani walitaja kama matumizi mabaya ya mamlaka yake, utendakazi usioridhisha na kutoheshimu wajibu wa kamati bunge hilo.

Hoja ya kumtimua Bw Balala ilidhaminiwa na diwani Jomvu Kuu Shebe Salim, aliyedai waziri huyo alifeli kuwajibikia matumizi ya Sh181 milioni za kufadhili mradi wa kuweka taa barabarani.

Bw Shebe, na madiwani wenzake walidai kuwa waziri huyo alidinda kufika mbele ya kamati ya uchukuzi kuelezea ni kwa nini ni taa 200 pekee ziliwekwa badala ya 2000 ilivyoratibiwa. Walidai Bw Joho anamtetea Bw Balala anapotakiwa kuwajibikia matumiza ya pesa za umma, madai ambayo gavana huyo alikana alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi hivi majuzi.

Suala hilo liliwasilishwa katika Seneti na Seneta wa Mombasa Mohammed Faki baadhi ya madai kuchipuza kwamba gavana huyo ana uhusiano na vuguvugu moja linalokusanya sahihi likitaka bunge la kaunti ya Mombasa livunjwe. Mwezi jana wanachama wa vuguvugu hilo kwa jina; “Operesheni Fagia Bunge” walifanya maandamano nje ya bunge la Mombasa wakisema wanalenga kukusanya zaidi ya sahihi 200,000 kufanikisha mpango huo.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya uongozi Barasa Nyukuri, yanayojiri katika kaunti ya Mombasa yanatia doa uongozi wa Gavana Joho na uwezo wake wa kudhibiti hali katika kaunti hiyo.

“Gavana Joho anapaswa kudhihirisha mfano mzuri wa uongozi kwa kudhibiti hali katika kaunti ya Mombasa. Kupitishwa kwa hoja ya kumtimua afisini mmoja wa mawaziri wake hakutoi picha mzuri kwa kiongozi ambaye ana ndoto ya kuwania kiti kikubwa cha urais,” anasema mtaalamu masuala ya uongozi Bw Barasa Nyukuri.

“Madai kwamba anaingilia utendakazi wa bunge la kaunti ya Mombasa huenda yakafasiriwa kumaanisha kuwa anahujumu ugatuzi ambao ni kichocheo kikuu cha maendeleo katika ngazi za mashinani,” anaongeza.

Bw Joho ambaye anahuhumu muhula wake wa pili na wa mwisho kama gavana wa kaunti ya Mombasa ametangaza kuwa atawania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Lakini alipofika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Laikipia John Kinyua Joho alitaja madai kwamba anaunga mkono shinikizo za kuvunjwa kwa bunge la Mombasa, kama “uvumi usio na msingi wowote”

“Wanaoleta uvumi kama huu mbele ya bunge hili la Seneti wanapaswa kufahamu kwamba sina uwezo wa kulivunja bunge la kaunti ya Mombasa. Na sina habari kwamba kuna kundi la watu huko nje wanaokusanya sahihi kwa malengo kama hayo,” akasema huku akisema yeye ni mtetezi sugu ugatuzi.

“Sitajibu uvumi na sarakasi za kisiasa ambazo zimeletwa mbele ya kamati hii na seneta wangu. Sijui alizitoa wapi. Juzi niliwaona maseneta wakijadili kile walichotaja kama mzozo katika kaunti ya Mombasa huku wengine wakitumia lugha ya matusi dhidi yangu,” akaongeza pale maseneta walipomtaka afafanue kuhusu chimbuko la uhasama kati ya madiwani na mawaziri wake.

Bw Joho aliwaambia maseneta hao kwamba yeye kando na kuwa “Sultan wa Mombasa” pia ni “Sultan wa Ugatuzi” na kwamba atahakikisha kuwa kaunti ya Mombasa imenufaika kwa ugatuzi.

Hata hivyo, aliungama kuwa kuna “masuala madogo” yanayoisibu kaunti ya Mombasa na ambayo yanapasa kutatuliwa.

“Kuna madiwani wachache ambao wanagombana na mawaziri wangu kuhusu usimamizi wa tenda za kuweka taa za barabarani. Na wengine wamekuwa wakimshinikiza Waziri wangu wa Uchukuzi Tawfiq Balala wakitaka kusimamia baadhi ya zabuni katika wizara yake,” akasema Bw Joho.

“Ikiwa madiwani wanataka kumfurusha afisini Waziri huyo kwa sababu hizo basi ningependa kuwaeleza kuwa nitamtetea waziri wangu kwa jino na ukucha,” akasisitiza.

Lakini baada ya madiwani kutekeleza tishio lao na kumfurusha Bw Balala, Bw Joho alionekana kutaka kupoesha joto hilo kwa kuwataka wakazi wa Mombasa kudumisha utulivu

Kwenye taarifa iliyowasilishwa kwa vyombo vya habari kwa niaba yake na mkurugenzi wa mawasiliano Richard Chacha gavana Joho alisema yu tayari kurejesha hali ya utulivu na ushirikiano kati ya madiwani na maafisa wake kwa “ajili ya kulinda na mafanikio ya ugatuzi”.

Makundi kadha ya mashirika ya kijamii pia yameingilia mzozo huo huku yakilaumu serikali ya Bw Joho huku yakielezea kutoridhishwa kwao na utendakazi wake kama mkuu wa serikali hiyo.

Chini ya mwavuli wa muungano wao kwa jina, “Mombasa Civil Society Network” viongozi wa mashirika hayo wanailaumu serikali ya Joho kwa matumizi mabaya ya fedha za umma na kutotekeleza miradi ya maendeleo iliyoritibiwa, katika mkakati wa maendeleo wa mwaka wa 2016/2017, shutuma ambazo zimepuuziliwa mbali na serikali hiyo.

Kwa upande wake Seneta Faki anaitisha utulivu kati ya madiwani wa kaunti ya Mombasa na serikali ya Joho ili kaunti hiyo iweze kuvuna matunda ya maendeleo yaliyoletwa na muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Hatima ya Bw Tawfiq Balala sasa imo mikononi mwa kamati ya madiwani watano iliyoteuliwa na Spika wa Bunge la Mombasa Aharub Khatri kuchunguza mienendo yake.