MakalaSiasa

JAMVI: Kuzomewa kwa Raila ni dalili ‘Jakom’ hawiki katika ngome yake tena

May 19th, 2019 4 min read

NA CECIL ODONGO

KUZOMEWA kwa Kinara wa ODM Raila Odinga katika eneo la Muhoroni, Kaunti ya Kisumu mapema wiki hii kumeibua mjadala iwapo umaarufu wa mwanasiasa huyo unaendelea kupungua miongoni mwa kizazi cha sasa katika eneo la Nyanza.

Bw Odinga ambaye anafahamika kama ‘Jakom’ kwa maana ya Mwenyekiti, miongoni mwa wenyeji wa Luo Nyanza, amekuwa mfalme wa siasa za eneo hilo kwa karibu miongo mitatu tangu kifo cha babake, marehemu Jaramogi Oginga Odinga ambaye alikuwa Msemaji wa jamii ya Waluo kabla na baada ya Kenya kupata uhuru

Bw Odinga akiwa ameandamana na Mawaziri Peter Munya, John Munyes, James Macharia, Naibu wa Gavana wa Kisumu Dkt Mathews Owili, alizomewa vikali na sehemu ya umati alipowarai wenyeji kuruhusu ardhi zao zitwaliwe na serikali ili kujenga Kituo Kikubwa cha Viwanda kama njia ya kuyainua maisha yao.

Hata hivyo, wakazi hao walionyesha ghadhabu zao kwa kuyabeba mabango na kumpigia Bw Odinga kelele naye akiwauliza kwa nini walikuwa wakimwaibisha ilhali alikuwa amewaletea miradi ya maendeleo.

“Kwa nini mnaniabisha? Nimewaletea maendeleo ila hamuonekani kuimakinikia miradi itakayowanufaisha,” akasema Bw Odinga.

Kando na kupinga wazo la kutoa ardhi zao kwa serikali kujenga viwanda, wakazi hao walikasirishwa na tamko la Bw Odinga kuwa kizazi chao cha awali kilikumbwa na umaskini mkubwa nao pia watakumbwa na uchochole usiopigiwa mfano wakikataa mradi huo.

“Babu wa babu zenu hawakutumia ardhi hii na wakafa maskini, babu zenu walifariki wakiwa hawana chochote kwa kufuata nyayo za wazazi wao na hata wazazi wenu wakafuata mkondo huo wa uchochole.

“Hauwezi kumiliki ardhi na kuingalia tu bila kuitumia kwa shughuli za uwekezaji, hata nyinyi mtakufa maskini kama wao mkikosa kubadilika. Lazima tuwekeze miradi katika vipande hivi vya ardhi ili kuwaletea watu wetu maendeleo,” akasema Odinga wakati wa vuta ni kuvute kati yake na baadhi ya wakazi.

Kilichoshangaza zaidi ni kwamba waliokuwa wakilalamika walipokezwa kipigo kikali na wafuasi wa Bw Odinga waliorarua mabango yao na kuwatimua kwenye mkutano huo huko wakazi walioangushiwa mateke, magumi na kuchapwa wakiapa kupinga mradi huo na liwe liwalo.

Kihistoria hakuna anayeamini kwamba ‘Jakom’ angekumbana na hali kama hii hasa katika eneo ambalo kumpinga kwa matamshi jukwani au wakati wa mjadala kunatosha kuvutia yeyote maadui lukuki.

Kabla ya kuibuka kuwa nguli wa siasa za Nyanza, Bw Odinga alikumbana na vizingiti kadhaa ikiwemo kudhalilishwa na uliokuwa utawala wa chama cha KANU na baadhi ya viongozi wakati huo kumwona kama mwanasiasa mwenye tamaa ya uongozi.

Hata baada ya kifo cha babake, alilazimika kuwapiga dafrau vigogo wa chama cha Ford Kenya kama James Orengo ambaye sasa ni Seneta wa Siaya na Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o, ambao wakati huo walikuwa viongozi wenye ushawishi mkubwa machoni mwa Waluo kumliko.

Joto lilipozidi kati yake na aliyekuwa Makamu wa Rais marehemu Kijana Wamalwa, Bw Odinga aligura Ford Kenya na kubuni National Democratic Party (NDP) alichotumia kuunganisha jamii ya Waluo na kuanza safari yake kama jagina wa siasa za Nyanza.

Ingawa hivyo, himaya aliyojenga Bw Odinga sasa inayumbayumba na kuelekea kuporomoka baada ya kuchipuka kwa matukio kadhaa yanayomponza kisiasa katika ngome yake.

Kando na kuzomewa na wakazi wa Muhoroni majuzi, Bw Odinga alilazimika kumeza mate machungu pale mgombeaji wa chama chake cha ODM kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ugenya Chris Karan, aliposhindwa vibaya na mgombeaji wa Movement for Democracy and Growth (MDG) David Ochieng’.

Kinara huyo wa ODM japo hakumfanyia kampeni mgombeaji wa chama chake aliwaomba wakazi wasimwaibishe debeni. Baadaye alijiliwaza kupitia vyombo vya habari kwa kusema uchaguzi huandaliwa ili kuwe na mshindi na mshinde.

Pili, Waziri huyo Mkuu wa zamani alilazimika kukita kambi Migori wakati wa uchaguzi mdogo wa Useneta ili kuhakikisha Seneta wa sasa Ochillo Ayacko anambwaga Eddie Oketch Gicheru wa chama cha Federal Party Of Kenya (FPK).

Hata hivyo, Bw Oketch alimtoa kijasho chembamba Seneta Ayacko licha ya kushindwa, alipata kura 60,555 ikilinganisha na 85,234 zake seneta huyo.

Ikizingatiwa kwamba hii ilikuwa ngome ya kisiasa ya ODM, wengi walitarajia mgombeaji wao angembwaga mshindani wake kwa kura nyingi kuliko mwanya finyu wa karibu kura 16,000 pekee.

Hata hivyo, wachangunuzi walisema kwamba Bw Gicheru ambaye alikuwa akiungwa mkono na Gavana Okoth Obado angeshinda kiti hicho iwapo gavana huyo hangekuwa akizuiliwa kutokana na kesi ya mauaji yaliyokuwa yakimkabili kortini.

Ingawa hivyo, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anahoji kwamba eneo la Nyanza linaendelea kupata mwamko mpya wa kisiasa hasa kutokana na idadi kubwa ya vijana wa kizazi cha sasa wasioelewa au walikosa kushuhudia masaibu ya Bw Odinga miaka ya nyuma.

“Wajua kizazi cha sasa kinaelekea kukosa uvumilivu hasa baada ya kumtetea Bw Odinga katika chaguzi zilizopita bila kufikia malengo yao. Wengi wao wanakosoa sera zake baada ya kukisia kwamba huenda hatakuwa debeni mwaka wa 2022 kutokana na matamshi yake ya kila mara kwamba hataki kuzungumzia siasa za uchaguzi huo,

“Vilevile maasi anayokumbana nayo Bw Odinga ni kwa sababu vijana wengi hawakuwa wamezaliwa wakati wa kupigania mfumo wa vyama vingi. Wengi wao wamekosa subira baada ya kupigania kigogo wao wakidai jitihada zao hazizai matunda yoyote,” akasema Andati akizungumza na Jamvi.

Mchanganuzi huyo hata hivyo, anakiri kwamba tukio la kuzomewa kwa Bw Odinga, Kaunti ya Kisumu halifai kutumiwa kama kipimo cha kusema umaarufu wake umepungua.

“Bw Odinga bado ana ushawishi mkubwa licha ya matukio yanayoashiria kushuka kwa umaarufu wake. Yeye ni mwanasiasa mweledi ambaye anasoma akili ya wapigakura na anajua wakati wa kuwasisimua kwa kauli nzito. Mambo yanaweza kuwa tofauti tu iwapo atasema hadharani hana nia ya kusimama Urais 2022 lakini bado atakuwa mwelekezi wa wapi Waluo watapigia kura zao,” akaongeza Bw Andati.

Seneta wa Homa bay Moses Kajwang’ hata hivyo anasema suala la kizazi cha sasa kumuasi Bw Odinga ni jambo linalobuniwa tu na wapinzani wake.

“Ukiangalia tukio la Muhoroni walikuwa watu wachache tu waliobeba mabango ishara kwamba walikuwa wamelipwa fedha kuvuruga mkutano wa kinara wetu. Kwa sasa Bw Odinga yupo sawa kisiasa katika eneo la Nyanza kuliko miaka ya nyuma hasa kutokana na uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wote, kinyume na kabla ya uchaguzi wa 2017 ambapo baadhi ya wabunge walikuwa wakimpinga waziwazi

“Kumbuka baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2013 kila mtu alisema siasa za Bw Odinga zimeisha lakini alibadilisha hali na kuwa kipenzi cha wananchi.

“Kuna viongozi wengi vijana Nyanza na madai kwamba kizazi cha sasa kinapinga sera yake ya uongozi ni uongo. Haya matukio madogo hayafai kutumika kudai Bw Odinga ameisha kisiasa,” akaongeza Bw Kajwang’.