MakalaSiasa

JAMVI: Matokeo ya sensa kuzaa miungano mipya ya kisiasa

November 10th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Matokeo ya sensa, yaliyotolewa Jumatatu wiki hii, yameanza kuzua joto huku wanasiasa wakitilia shaka idadi ya wakazi wa maeneo yao.

Hata hivyo, wadadisi wanasema matokeo hayo yatabadilisha siasa za Kenya kabla ya 2022 huku wanasiasa wakiyatumia kubuni miungano ya kisiasa hasa wale wanaomezea mate kiti cha urais.

“Wanasiasa sasa watatumia idadi ya wakazi wa maeneo wanayotaka kujipigia debe. Miungano ya kisiasa itategemea idadi ya wakazi wa eneo ambalo mwanasiasa anatoka.

“Tusidanganyane, ushirika wa siasa huwa unategemea idadi ya kura ambazo mwanasiasa anaweza kuweka kikapuni,” asema mdadisi wa siasa, George Odongo.

Anatoa mfano wa miungano ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013 ambayo ilizaa Jubilee na Cord na kisha chama cha Jubilee na muungano wa NASA akisema ililenga maeneo yaliyo na watu wengi.

“Jubilee ilipata nguvu kutokana na kura za maeneo ya Rift Valley na Mlima Kenya wanakotoka viongozi wao Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Wake William Ruto, NASA ilikuwa na nguvu maeneo ambayo vinara wake wanne walitoka na yote ni maeneo yaliyo na watu wengi,” asema.

Kulingana na matokeo ya sensa, takriban nusu ya Wakenya wanaishi ngome za chama cha Jubilee ya Mlima Kenya, Rift Valley na Kaskazini Mashariki.

Maeneo hayo yana jumula ya watu 22.4 milioni miongoni mwa watu 47 milioni waliohesabiwa.Wadadisi wanasema hii inaweza kuzidisha mgogoro katika chama hicho tawala huku wanaomezea mate kiti cha urais wakitaka kukithibiti.

“Hata kama kitavunjika, wanasiasa watawania kushirikiana na vigogo wa kisiasa wa maeneo hayo kubuni miungano itakayochipuka kabla ya 2022,” aeleza.Ngome za muungano wa NASA ambao pia inakumbwa na mizozo, ina zaidi ya watu 20 milioni ishara kwamba vinara wake wakiutia nguvu unaweza kuitoa jasho Jubilee kwenye uchaguzi mkuu ujao ilivyokuwa 2017.

“Lakini dalili zinaonyesha kuwa miungano iliyo kwa wakati huu itavunjika na wanasiasa kutumia matokeo ya sensa kujipanga upya. Kuanzia sasa, itakuwa ni wanasiasa kujadili miungano huku wanaotoka maeneo yaliyo na watu wengi wakiwa na nafasi ya kujinadi,’ aeleza Bw Simon Kamau, mchanganuzi wa siasa.

Anasema kuna uwezekano mkubwa wa wawaniaji wa kiti cha urais kubadilisha mbinu na kulenga kaunti zilizo na watu wengi.Katika ngome za kiongozi wa ODM Raila Odinga aliyekuwa mgombeaji urais wa muungano was NASA, hali inaweza kubadilika iwapo muungano huo utavunjika.

Kuna juhudi za viongozi wa eneo la Magharibi kuungana na kushirikiana na wanasiasa wengine kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika eneo la Ukambani ambako kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka anatoka sensa ilionyesha kuna watu 3.5 milioni na tayari kuna minong’ono kuwa huenda akatema NASA na kuungana na kushirikana na wanasiasa wengine kubuni muungano mpya wa kisiasa.

Wadadisi wanasema kuna uwezekano mkubwa wa Bw Musyoka, Mudavadi, Wetangula wakaungana na Bw Ruto kabla ya uchaguzi huku mrengo mmoja wa Jubilee, ukiungana na Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Baadhi ya wanasiasa wa chama cha Jubilee wamekuwa wakisema kutakuwa na muungano mkubwa wa kisiasa kabla ya 2022 na wadadisi wanasema matokeo ya sensa yatachangia pakubwa muundo wake.

“Nguvu za siasa ni idadi ya watu na kwa vyovyote vile, mtu hawezi kutenga siasa na idadi ya watu katika demokrasia kama ya nchi yetu.

“Ikizingatiwa vyama vya kisiasa nchini ni vya kimaeneo na mtu hawezi kushinda urais kwa kutengemea eneo lake au jamii yake pekee, matokeo ya sensa yatatoa mwelekeo kwa miungano ya kisiasa kuanzia sasa,” alisema Bw Odongo.

Kulingana na viongozi wa chama cha Amani National Congress za Musalia Mudavadi, eneo la magharibi lina watu 6 milioni na linafaa kutumia idadi hiyo kuhakikisha litakuwa kwenye serikali ijayo.

Naibu Rais William Ruto ambaye ametangaza azma yake ya kugombea urais amekuwa akijaribu kupenya eneo hilo lililopigia NASA kura kwa wingi na kuna tetesi kwamba huenda akaungana na baadhi ya viongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, matokeo ya sensa yatabadilisha mkondo wa siasa nchini. Kaunti ya Nairobi ina watu 4.5 milioni. “ Wanaojipanga kuwania urais lazima walenge Nairobi,” alisema.