Siasa

JAMVI: Mbinu chafu za vyama kuwasajili wanachama

August 16th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

VYAMA vya kisiasa sasa vinatumia mbinu za kilaghai kusajili wanachama wapya, imebainika.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa (RPP) Ann Nderitu anasema kuwa afisi yake imepokea malalamishi tele kutoka kwa Wakenya wanaodai kusajiliwa kuwa wanachama wa vyama vya kisiasa bila wao kujua.

“Tumepokea malalamishi tele kutoka kwa Wakenya wanaosema kuwa wamesajiliwa kuwa wanachama wa vyama vya kisiasa bila idhini yao.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Jumapili, ulibaini kuwa vingi ya vyama vipya huchukua majina ya wanachama kutoka kwa maduka ya Mpesa.

Baadhi ya vyama pia hutengeneza programu (app) za simu wakijifanya kutoa mikopo ya simu. Lakini baada ya ‘mteja’ kujisajili kwa kuweka taarifa muhimu, ikiwemo nambari ya kutambulisho, mikopo haitumwi.

Hiyo inamaanisha kuwa ikiwa umewahi kujisajili kwenye app kutafuta mikopo ya simu basi kuna uwezekano kwamba jina lako liko kwenye orodha ya wanachama wa moja ya vyama vya kisiasa humu nchini.

Ili chama kusajiliwa kikamilifu ni sharti kiwe na angalau wanachama 1,000 kutoka kaunti zisizopungua 24. Hiyo inamaanisha kuwa chama ni sharti kiwe na wanachama 24,000 kabla ya kusajiliwa.

Ili kutimiza hitaji hilo, vyama vimekuwa vikitumia njia za mkato kupata wanachama.

“Kukomesha ulaghai huo afisi yangu imeanza harakati za kuhakikisha kuwa sajili za vyama vya kisiasa zinasalia na wanachama halali,” akasema Bi Nderitu.

Sheria inahitaji kuwa ni sharti mtu akubali yeye mwenyewe kabla ya kusajiliwa kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa.

Ili kuondoa uanachama wako kwenye chama usichotaka, Bi Nderitu anasema kuwa ni sharti uandikie barua chama kilichoweka jina lako kwenye daftari lake la wanachama.

“Andika barua ya kujiondoa kwa chama husika na uambatanishe nakala ya kitambulisho chako. Toa nakala ya barua hiyo na kitambulisho na uitume kwa [email protected]. Afisi ya ya RPP itakusaidia kuhakikisha kuwa unajiondoa kwenye chama hicho,”anasema Bi Nderitu.

Tangu kutangazwa kwa kisa cha kwanza cha mwathiriwa wa virusi vya corona humu nchini mnamo Machi, mwaka huu, jumla ya vyama 10 vimetuma maombi ya kutaka kusajiliwa.

Chama cha hivi karibuni kutuma maombi ni Party for Peace and Democracy (PPD).

Vyama vingine ambavyo vimewasilisha maombi na kuruhusiwa kuanza safari ya kusaka wanachama huku vikingojea kusajiliwa kikamilifu ni National Reconstruction Alliance, Unified Change, Umoja Summit, Universal Unity, The Great Nationhood, Kenya Moja People’s Party, kati ya vinginevyo.

Kati ya Februari na Mei, mwaka huu, msajili wa vyama vya kisiasa amefutiliwa mbali baada ya kushindwa kutimiza matakwa, ikiwemo kupata wanachama 1,000 kutoka kila angalau kaunti 24.

Vyama vilivyofutiliwa mbali ni Transformation National Alliance, Pambazuko Alliance Party, Sauti Ya Mwananchi, Green Thinking Action na Ideal Democratic Economic.

Tangu Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kushirikiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo 2018, idadi ya vyama vya kisiasa ambavyo vimesajiliwa kikamilifu imeongezeka kutoka vyama 68 hadi 83.

Vyama vilivyosajiliwa hivi karibuni ni National Ordinary People Empowerment Union, The Service Party (TSP) chake aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri na Party of Economic Democracy.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa kuwa huenda chama kinachotumiwa na Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022 ni miongoni mwa vyama vipya vilivyosajiliwa kati ya mwaka jana na mwaka huu.

Licha ya wandani wa Dkt Ruto kushikilia kuwa hawatagura kutoka Jubilee, wadadisi wanasema kuwa Dkt Ruto tayari amepigwa teke ndani ya Jubilee na anafaa kubuni chama chake atakachotumia 2022.

Awali, kulikuwa na tetesi kwamba Naibu wa Rais atatumia chama kinachojulikana kama Jubilee Asili, lakini maombi ya kutaka kusajili chama hicho hayajafikishwa kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa.