Siasa

JAMVI: Mbona kufuli Jubilee House miezi 7 sasa?

September 13th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

VITA vya kisiasa katika chama cha Jubilee vinazidi kuchacha huku wandani wa Naibu wa Rais William Ruto wakifungiwa nje ya makao makuu ya chama hicho tawala.

Kwa mujibu wa wandani wa Naibu Rais Ruto, afisi za makao makuu ya Jubilee zilizoko katika mtaa wa Pangani, Nairobi, zimefungwa kwa miezi saba sasa.

Juhudi za Dkt Ruto ambaye ni naibu kiongozi wa Jubilee, kupata majibu kutoka kwa Katibu Mkuu Raphael Tuju zimegonga mwamba, kwa mujibu wa mbunge wa Kimilili Didmus Barasa.

Bw Barasa asema kuwa chama cha Jubilee tayari kimesambaratika na kimesalia ‘gae tupu’.

Jumatano iliyopita, Dennis Itumbi ambaye ni mmoja wa maafisa wa mawasiliano wa kibinafsi wa Dkt Ruto alidai kuwa Bw Tuju hajakuwa akipokea simu za Naibu wa Rais ili kutoa ufafanuzi kwa nini amefunga afisi za makao makuu ya chama.

“Baada ya kukataa kupokea simu za Naibu wa Rais kwa muda mrefu ili kuelezea kwa nini makao makuu ya chama yamefungwa, hatimaye Bw Tuju leo amejibu. Tuju alisema kuwa kuanzia wiki ijayo ataanza kufanya kazi kutoka afisi za makao makuu ya chama,” akadai Bw Itumbi.

Wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Caleb Kositany, ambaye pia ni mbunge wa Soy na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria mnamo Aprili mwaka huu walitishia kuanza kufanya kazi kutoka makao makuu ya Jubilee.

Wawili hao walisema hatua hiyo ingesaidia wandani wa Dkt Ruto, almaarufu Tangatanga, kuwa na ushawishi katika shughuli za chama cha Jubilee.

Wabunge na maseneta wa ‘Tangatanga’ pia walitishia kusitisha mchango wao wa kila mwezi kwa chama wakidai kuwa maafisa wakuu wa Jubilee wamekuwa wakifuja fedha.

Madiwani wa Jubilee hulipa Sh5,000 kila mwezi, wabunge na maseneta Sh20,000 na magavana Sh50,000.

Kifungu cha 7B cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa kinahitaji viongozi waliochaguliwa kutoa michango kwa vyama vya kisiasa.

Kifungu cha 13.3 (1)H cha Katiba ya Jubilee kinasema kuwa kiongozi aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama hicho anayekosa kutoa mchango wa kila mwezi ni sharti achukuliwe hatua ya kinidhamu.

Viongozi wakuu wa Jubilee wanaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta, hata hivyo, walizima jaribio la Tangatanga kutaka kufanya kazi kutoka katika makao makuu ya chama. Bw Kositany aliambia Taifa Jumapili kuwa afisi za makao makuu ya Jubilee zimetwaliwa na ‘wageni’ wasiowatambua.

“Jumba la makao makuu ya Jubilee lina orofa saba lakini nne zinatumiwa na wageni ambao hatuwajui. Jambo la kusikitisha ni kwamba chama cha Jubilee kinalipa kodi ya jumba zima,” akasema Bw Kositany.

Alisema kuwa wageni hao wametwaa hata mahali pa kufanyia mikutano kujadili masuala nyeti ya chama.

“Hiyo ndiyo maana tuliamua kufungua afisi za Jubilee Asili ili tupate pahala pa kukutana na kujadili masuala muhimu ya chama,” akaongeza Bw Kositany ambaye amekuwa akizungumza kwa niaba ya Naibu wa Rais.

Naibu wa Rais William Ruto, amekuwa akilaumu naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na Bw Tuju kwa kusababisha mgawanyiko katika chama cha Jubilee.

Katika mahojiano na runinga mojawapo ya humu nchini wiki iliyopita, Dkt Ruto alisema kuwa ameanzisha juhudi za kuwatimua wawili hao kutoka Jubilee.

“Lakini wakitushinda basi tutawaombea kwa Mungu awatoe,” akasema Dkt Ruto.

Naibu wa Rais pia ameashiria kuwa huenda akatumia chama mbadala kuwania urais 2022 baada ya Bw Murathe kusisitiza kuwa chama cha Jubilee kitaunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Naibu wa Rais anahofia kuwa huenda akanyimwa tiketi ya kuwania urais 2022 baada ya kupoteza udhibiti wa Jubilee.

Wandani wa Rais Kenyatta tayari wameanzisha mpango wa kutaka kumzuia Dkt Ruto kuwania urais 2022 kwa tiketi ya Jubilee.

Miongoni mwa mipango hiyo ni kugawanya wadhifa wa naibu kiongozi wa chama unaoshikiliwa na Naibu wa Rais Ruto, mara nne.

Katika mfumo huo mpya wa uongozi, chama cha Jubilee kitakuwa na manaibu wanne wa kiongozi wa chama.

Hatua hiyo inalenga kuzima na kulemaza ushawishi wa Dkt Ruto chamani na kumnyima fursa ya kupeperusha bendera ya Jubilee 2022.