JAMVI: Miungano ya kisiasa inayobuniwa nchini ni ya kufaidi wanasiasa tu!

JAMVI: Miungano ya kisiasa inayobuniwa nchini ni ya kufaidi wanasiasa tu!

Na CHARLES WASONGA

HUKU vigogo wa kisiasa nchini wakiwa mbioni kubuni miungano ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, kuna hisia mseto kuhusu iwapo serikali zinazobuniwa na miungano aina hii huleta manufaa kwa Wakenya au la.

Kuna dhana kwamba miungano hii hubuniwa kwa lengo moja la kuwawezesha vigogo fulani mamlakani huku raia wa kawaida wakiambulia patupu.

Kwa upande mwingine kuna wale wanaoamini kuwa miungano ya kisiasa imesaidia kuleta utulivu nyakati ambapo Kenya ilijipata vibaya baada ya kulipuka kwa mizozo ya kisiasa.

Mfano ambao wanaotoa ni ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambazo zililipuka baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais ambapo Rais mstaafu Mwai Kibaki alitangazwa mshindi. Bw Odinga alikataa kutambua ushindi huo akidai kura zake ziliibwa.

Mzozo huo ulitanzuliwa na wapatanishi waliotumwa na Umoja wa Mataifa (UN) chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa umoja huo marehemu Koffi Annan. Baada serikali ya muungano ulibuniwa ambapo Bw Odinga alipewa wadhifa wa Waziri Mkuu.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa dhana ya miungano ya kisiasa ilijiri nchini baada ya uchaguzi mkuu wa 1997, chama tawala wakati huo, Kanu, kilipotaka kujiongea nguvu ndani na nje ya bunge.

Sababu ni kwamba katika uchaguzi huo Kanu kilichoongozwa rais wa zamani marehemu Daniel Moi kilishinda viti 98 kati ya 210 bungeni. Chama cha Democratic Party (DP) chake Bw Kibaki nacho kikapata jumla ya viti 39 huku kile cha Bw Odinga wakati huo, National Development Party (NDP) kikashinda viti 21.

“Kwa hivyo ili kuweza kupitisha ajenda za serikali bungeni kwa urais Moi alibuni muungano na Bw Odinga mnamo 1998 ambapo Kanu ilimeza NDP na kukabuniwa muungano uliojulikana kama New Kanu. Odinga aliteuliwa Katibu Mkuu wa muungano huo mpya na Waziri wa Kawi serikalini,” anaeleza Profesa Macharia Munene.

Mchanganuzi huyo wa kisiasa anasema baada ya Odinga na chama chake cha NDP kumsaidia Mzee Moi kuongoza, licha ya pingamizi kutoka kwa vyama vya upinzani kama DP na Ford-Kenya, rais huyo alimpiga teke kuelekea uchaguzi mkuu wa 2002.

“Badala yake Moi alimteua Bw Uhuru Kenyatta, ambaye nyakati hizo alikuwa mwanasiasa mchanga, kuwa mrithi wake, hatua iliyomfanya Bw Odinga kuanza harakati za kusaka marafiki wengine wa kisiasa,” anasema Profesa Munene.

Hii, kulingana na mchanganuzi huyu, inaashiria kuwa muungano huo wa kisiasa haukujengwa katika misingi ya sera na itikadi madhubuti. Haukubuniwa kwa nia ya kutimiza malengo ya kufaidi mwananchi wa kawaida bali ni malengo finyu ya wanasiasa viongozi.

Ni msukumo huu uliopelekea vyama vya upinzani wakati huo kama vile Liberal Democratic Party (LDP) kilichobuniwa na Bw Odinga na wandani wake baada ya kugura Kanu, DP na Ford Kenya viliungana na kubuni muungano uliojulikana kama National Rainbow Coalition (NARC).

Ili kudhihirisha kwamba muungano huu pia ulijengwa katika misingi ya uchu wa wanasiasa kujifaidi, vigogo wa Narc waliandaa mkataba wa maelewano (MOU) ambapo waliahidi kugawana mamlaka.

Kwa mfano chini ya MOU hiyo walikubaliana kuwa Bw Kibaki angekuwa Rais huku Bw Odinga alishikilia wadhifa wa Waziri Mkuu ambao ungebuni baada ya Katiba kufanyiwa marekebisho siku 100 baada ya wao kuingia mamlakani. Aliyekuwa mwenyekiti wa Ford Kenya marehemu Michael Wamalwa Kijana aliahidiwa wadhifa wa Makamu wa Rais.

Narc iliposhinda Kanu na Bw Kibaki kuingia Ikulu, alikafeli kutimiza ahadi zilizokuwa katika mkataba huo huku akionyesha dalili za kutounga mkono marekebisho ya Katiba.

Bw Odinga aliteuliwa Waziri wa Barabara na Nyumbani, Wamalwa akatunikiwa wadhifa wa Makamu wa Rais huku vigogo wengi wakiteuliwa mawaziri. Misukosuko ilianza kutokota ndani ya serikali huku kambi ya Odinga ikiweka presha Katiba ifanyiwe marekebisho.

Japo Kibaki alisalimu amri aliunga mkono rasimu ya Katiba ambayo Bw Odinga na wenzake hawakutaka na wakaiangusha katika kura ya maamuzi iliyofanyika Novemba 21, 2005.

Kulingana na mtaalum wa masuala ya uongozi Bw Barasa Nyukuri, mivutano ndani ya Narc wakati huo ndio ilipanda mbegu ya ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo zaidi ya watu 1, 200 walifariki.

“Hii ndio maana kwa mtazamo wangu, miungano ya kisiasa ya hapo awali ilileta madhara makubwa nchini kuliko mazuri. Kando na watu waliofariki na kujeruhiwa katika fujo hizo mali ya thamani kubwa iliharibika na uchumi kudorora kwa kiasi kubwa mno,” anasema.

Kulingana na Bw Nyukuri wanasiasa ambao wanabuni au kujipanga kubuni miungano wakati huu, sawa na wale wa zamani, ni watu ambao wanaongozwa na hamu ya kujitakia makuu bali sio kusaidia raia.

“Kwa mfano, muungano wa NASA umeporomoka kutokana na hali kwamba ulibuniwa kuendeleza masilahi ya vigogo wake. Chama cha Jubilee ambacho kilibuniwa baada ya kuunganishwa kwa vyama 13 mnamo 2016, pia kinaporomoka kwa sababu hizo hizo,” anaongeza.

Lakini aliyekuwa kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen na kingozi wa wachache katika bunge la kitaifa John Mbadi wanapinga kauli ya Bw Nyukuri kwamba miungano ya kisiasa inaongozwa na malengo finyu.

Wawili hao wanashikilia kuwa hali ya siasa nchini wakati huu ni kwamba hakuna chama kimoja ambacho kinaweza kushinda uchaguzi mkuu kivyake.

“Hii ni kwa sababu siasa zetu bado ni za kikabila na kimaeneo. Wakati huu hamna chama cha kisiasa kinachoweza kudai kuwa kina mizizi kote nchi,” anasema Bw Murkomen.

“Kwa hivyo, sisi kama wanachama wa vuguvugu la Hasla tuko mbioni kusaka marafiki kutoka pembe zote za nchi ili tubuni muungano nao,” Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet anaongeza.

You can share this post!

JAMVI: Mkanganyiko mkuu unaogubika siasa za urithi Pwani

FAUSTINE NGILA: Mitandao yabadili sura ya maandamano nchini