Siasa

JAMVI: Miungano ya uchumi ni ya nini ikiwa haifaidi kaunti?

August 16th, 2020 3 min read

Na WANDERI KAMAU

KIMYA cha miungano ya kiuchumi ya kaunti mbalimbali kimeibua maswali kuhusu umuhimu na michango yake nchini, hasa wakati huu Kenya inaendelea kupambana na janga la virusi vya corona.

Miungano hiyo pia imelaumiwa pakubwa kwa kutotoa sauti yoyote kwenye utata unaoendelea kwenye Seneti kuhusu utaratibu wa ugavi wa mapato kwa serikali za kaunti.

Mara tu baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi mnamo 2013, magavana waliungana na kubuni miungano hiyo, ikitarajiwa kwamba ingezisaidia kaunti kujikomboa kiuchumi na kisiasa.

Miungano hiyo sita ni Baraza la Maendeleo la Kaunti za Mpakani (FCDC) linalozishirikisha kaunti saba za eneo la Kaskazini Mashariki zikiwemo Garissa, Wajir, Mandera, Isiolo, Marsabit, Tana River na Lamu; Muungano wa Kiuchumi wa Kaunti za Kaskazini Mashariki (NOREB), Muungano wa Kiuchumi wa Kaunti za Eneo la Ziwa (LREB), Jumuiya ya Kaunti za Pwani, Muungano wa Kiuchumi wa Kusini Mashariki mwa Kenya (SEKEB) na Muungano wa Kiuchumi wa Eneo la Mlima Kenya na Aberdares.

Ingawa miungano ilitarajiwa kupiga jeki ushirikiano wa serikali ya kitaifa na zile za kaunti, wadadisi wa siasa na masuala ya utawala wanasema kuwa uwepo wake ni kama hauna manufaa, kwani haijaonekana ikichangia lolote, hasa wakati huu kaunti zinahimizwa kuungana kwenye juhudi za kukabili corona.

Wadadisi wanasema kwamba ingawa jukumu la msingi la miungano hiyo ni kuzisaidia kaunti kuwianisha na kutekeleza mikakati ya kiuchumi, umuhimu wake ungedhihirika wakati huu ambapo kaunti zinapaswa kujitokeza na kutoa sauti kuhusu masuala makuu yanayoziathiri.

“Hatujaona ushirikiano wa kaunti ambazo ni wanachama wa miungano hiyo ukidhihirika kwenye juhudi za kukabili corona hadi sasa. Badala yake, kaunti mbalimbali zinaendeleza juhudi hizo kivyake, bila kushirikisha zingine ambazo ni wanachama wa miungano husika,” asema Bw Felix Otieno, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya utawala.

CORONA

Kwa mujibu wa Bw Otieno, hilo ndilo limemlazimu Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, kwenda katika kaunti kadhaa yeye binafsi, ili kutathmini hatua zilizochukua kujitayarisha kuikabili corona.

“Hatungeshuhudia hali kama hiyo, ambapo waziri analazimika kuenda katika kaunti mbalimbali mwenyewe ili kufuatilia zilivyojitayarisha. Katika hali ya kawaida, miungano hiyo ingekuwa majukwaa muhimu ambapo kaunti zingeshirikiana kuendesha juhudi za pamoja kulikabili janga,” akasema.

Kuhusu utata wa ugavi wa mapato, wadadisi pia wanaonya huenda ukaendelea kuwepo, “kwani taasisi ambazo zipo kutetea maslahi ya kaunti zimenyamaza.”

“Kikatiba, Seneti ndiyo taasisi yenye mamlaka kujadili na kusimamia masuala yanayohusu kaunti. Hata hivyo, hilo halijazizuia taasisi kama Baraza la Magavana (CoG) ama miungano ya kiuchumi kutoa hisia zao kuhusu masuala yanayozihusu kaunti,” asema Bw Charles Mulila, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ugatuzi.

Magavana wamekuwa wakikosolewa kwa kukosa kuweka mikakati ifaayo kuziwezesha kaunti kujitayarisha ifaavyo kukabili corona, licha ya kupokea Sh5 bilioni kutoka kwa Serikali ya Kitaifa.

Vile vile wamelaumiwa kwa kutoonyesha ushirikiano kwenye utatuzi wa utata kuhusu utaratibu wa ugavi wa mapato.

Kulingana na Bi Wanjiru Gikonyo, ambaye ni Mshirikishi Mkuu wa Taasisi ya Uwajibikaji wa Kijamii (TISA), migawanyiko ya kisiasa na ubinafsi miongoni mwa baadhi ya magavana ndicho kikwazo kikuu kwenye ukuaji wa miungano hiyo.

Kwa mfano, baadhi ya magavana wanaohudumu katika mihula ya pili wametangaza azma mbalimbali za siasa, miongoni mwazo ikiwa kuwania urais.

Miongoni mwa wale ambao wametangaza azma hizo ni Gavana Alfred Mutua (Machakos) na Kivutha Kibwana (Makueni). Wengine kama Mwangi wa Iria (Murang’a), Hassan Joho (Mombasa), Jackson Mandago (Uasin Gishu) wameonyesha nia za kuendelea kuwepo siasani hata baada ya mihula yao kuisha.

“Katika hali ambapo magavana wanapania kuendelea kuhudumu kwenye siasa hata baada ya mihula yao kukamilika, ni vigumu sana kwao kuelekeza juhudi zao kuikuza miungano hiyo. Hilo linaifanya tu kuonekana kwenye madaftari lakini si yakiendesha shughuli mbalimbali kwa manufaa ya umma,” akasema Bi Gikonyo.

Miungano pia imelaumiwa kwa kuendelea kusalia kimya hata wakati ambapo kaunti kama Kirinyaga zinakumbwa na mizozo ambayo kando na uwepo wa Seneti, inahitaji mwingilio wao.

Hata hivyo, mwenyekiti wa CoG, Bw Wycliffe Oparanya, anasema miungano hiyo ingalipo na inaendeleza mipango yake katika maeneo ya mashinani.

Anaeleza magavana wengi hukutana katika kaunti zao, hivyo si lazima waonekane kwenye makongamano mbalimbali jijini Nairobi.

“Hii ni miungano inayojikita kwenye masuala yanayohusu maslahi ya wananchi katika maeneo ya mashinani. Hivyo, si lazima ionekane ikiandaa makongamano makubwa jijini Nairobi na kwingineko ili kufasiriwa inafanya kazi,” asema Bw Oparanya.

Hata hivyo, wadadisi wanasema lazima miungano hiyo ijitokeze wazi ili kutetea maslahi ya kaunti na kubuni njia ambazo maeneo iliyomo yatafaidika kiuchumi kutoka kwa serikali na mashirika mengine.