MakalaSiasa

JAMVI: Mivutano, pandashuka za utekelezaji wa BBI zaanza kudhihirika

December 1st, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Mchakato wa kujadili na hatimaye kutekeleza ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), ambayo ilitolewa rasmi kwa umma Jumatano katika ukumbi wa Bomas Of Kenya, Nairobi, huenda ukawa mrefu na wenye changamoto tele.

Tayari maoni yanayotolewa na viongozi, umma na wadadisi yanaonyesha kuwa haitakuwa mteremko kutekeleza ripoti hiyo.

Kambi mbili zimeibuka ilivyokuwa kabla ya ripoti kutolewa, moja ikitaka utekelezaji wake ushughulikiwe na bunge na ya pili ikitaka kamati ya wataalamu ibuniwe ili kuandaa mswada baada ya Wakenya kuichanganua na kutoa maoni.

Wadadisi wanasema ni mvutano kati ya kambi hizi mbili ambao unaweza kufanya safari ya kutekeleza ripoti hii kuwa yenye pandashuka tele.

“Hii ni kwa sababu huenda viongozi wakatofautiana kuhusu mchakato wa kisheria unaopaswa kutumiwa na vitisho kutoka kwa baadhi ya wabunge kuipinga au kutaka ibadilishwe kutimiza malengo ya kisiasa,” aeleza mdadisi wa masuala ya kisiasa Geff Kamwanah.Anasema hii ilikuwa dhahiri wakati wa kuzindua ripoti mnamo Jumatano.

“Kauli za wanasiasa waliokuwa wakipinga Jopokazi la Maridhiano zilionyesha kuwa uzinduzi huo ulifanyika katika muktadha ya kutoaminiana. Unaweza kupata haya katika kauli za Aden Duale (kiongozi wa wengi katika bunge) na Kipchumba Murkomen (kiongozi wa wengi katika seneti),” aeleza.

Mnamo Jumatano katika ukumbi wa Bomas, Murkomen na Duale walitofautiana na wanenaji wengine katika uzinduzi wa ripoti hiyo wakisema hatima yake itaamuliwa na wabunge na maseneta kauli ambayo Dkt Ruto aliunga.

Bw Kamwanah anasema ingawa Rais Uhuru Kenyatta ameahidi kutekeleza ripoti hiyo kikamilifu, mvutano unaoendelea katika chama chake cha Jubilee, mmoja ukihisi inapendelea watu wachache, huenda ukaongeza changamoto za kutekeleza ripoti hiyo.

“Ninaweza kukufahamisha wazi kuwa mchakato wa kuitekeleza utakumbwa na hali ati ati, upinzani na mvutano hasa ukiwasilishwa katika bunge,” asema Bw Kamwanah.

Mshirika wa Rais Kenyatta katika handisheki iliyozaa jopokazi lililoandaa ripoti hiyo, Raila Odinga, amekuwa akiipigia debe na kuwataka wanaoipinga kuisoma kwanza.

Kulingana na Rais Kenyatta na Bw Odinga, ripoti hiyo itakuwa mwanzo wa kuunganisha Wakenya ambao wamekuwa wakipigana wakati wa uchaguzi kila baada ya miaka mitano baadhi ya jamii zikihisi kutowakilishwa katika serikali.

Dkt Ruto mwenyewe amekuwa akisisitiza kuwa mjadala kuhusu ripoti hiyo haufai kutumiwa kubuni nafasi za kazi kwa watu wachache.

Kulingana na Bw Murkomen, baadhi ya viongozi wamekuwa wakikaziwa kutoa maoni kuhusu ripoti hiyo na mjadala unafaa kufanyika kwa uwazi.

Ripoti hiyo sio mswada mbali ni mapendekezo kutoka kwa maoni ambayo jopokazi hilo lilikusanya kutoka kwa Wakenya wapatao 7000.

Rais Kenyatta ametimiza ahadi yake kwa kutoa ripoti kwa umma na kuwahimiza Wakenya waisome na kutoa mchango wao, shughuli iliyoanza kwenye kikao cha Bomas.

Kuna ripoti kuwa atazuru maeneo tofauti nchini akiwa na Bw Odinga na viongozi wanaoiunga mkono kuipigia debe ripoti hiyo.

Wadadisi wanasema kuna uwezekano Dkt Ruto na kikosi chake cha Tangatanga nao watazunguka nchini wakieleza raia kukataa baadhi ya mapendekezo na hasa utekelezaji wake.

Kama ingependekeza mabadiliko ya kisheria yanayohusu kipindi cha rais na ugatuzi miongoni mwa masuala mengine, mswada ungeundwa kuwasilishwa kwa mabunge yote 47 ya kaunti nchini ujadiliwe.

Mswada huo ungehitajika kupitishwa na mabunge ya kaunti 24 kabla ya kuwasilishwa kwa bunge la taifa.

Iwapo kwenye mjadala kuhusu ripoti hii Wakenya hawatapendekeza kura ya maamuzi kufanyika, mswada utaandaliwa na kuwasilishwa ujadiliwe katika bunge la taifa ambako mdahalo mkali unatarajiwa ikiwa wabunge wanaounga Dkt Ruto wataweza kushawishi wengine kuukataa.

Wadadisi wanasema hii ndio sababu wandani wa Dkt Ruto hawataki kamati ya wataalamu ibuniwe hofu yao kuu ikiwa wanaweza kupendekeza refarenda kubadilisha kipindi cha rais kuhudumu.

Bw Duale amewahi kunukuliwa akisema wabunge wataikataa ripoti ikiwa itapendekeza kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi.

Baadhi ya wabunge kutoka Mlima Kenya wameapa kuikataa iwapo watahisi kuwa haitatimiza matakwa fulani kuhusu maeneo na jamii zao.

Wadadisi wanasema safari ya kujadili na kutekeleza ripoti hii inatazamiwa kuwa na panda shuka nyingi hasa bungeni ambako mswada utawasilishwa.

Huku Dkt Ruto na wandani wake wakipendelea bunge ishughulikie utekelezaji wa ripoti hiyo, Bw Odinga na wabunge wa Jubilee wanaoiunga wanasema inafaa kupigiwa kura na Wakenya kwenye referenda.

Ingawa ilitakiwa kutoa mapendekezo kuhusu ghasia za kikabila, ukosefu wa ushirikishi, ugatuzi, uchaguzi, usalama, ufisadi na ustawi kwa wote, wadadisi wanasema huenda masuala haya yakazua mjadala mkali viongozi ikiwa viongozi watashikilia misimamo yao.

“Mchakato huu unafaa kuwa wa raia, haufai kutekwa na wabunge, hii ni ripoti ya raia,” alisema Bw Odinga msimamo ulioungwa na wabunge kadhaa wa vyama vya Jubilee, Wiper, Amani National Congress, Kanu na Economic Freedom Party.

Wabunge hao wanahisi kwamba ripoti hiyo inaweza kuzimwa bungeni ambapo wandani wa Dkt Ruto wanashikilia nyadhifa kuu za uongozi.

Wadadisi pia wanasema ni tofauti hizi ambazo zitafanya mchakato wa kutekeleza ripoti hiyo kuwa mrefu.

Kulingana na mwenyekiti wa chama cha ODM John Mbadi, ni rahisi bunge kusambaratisha BBI.“Itahitaji wabunge 232 kupitisha mabadiliko ya kikatiba jambo ambalo sio rahisi na kwa hivyo kuachia wabunge utekelezaji wa BBI ni kuiua,” alisema.

Kulingana na mdadisi wa masuala ya kisiasa, Dkt James Waikwa, matamshi ya wanasiasa yanaonyesha kuwa mjadala kuhusu BBI utapandisha joto la kisiasa nchini.