Makala

JAMVI: Mkono fiche wa mabilionea unaomtetemesha Sonko jijini

April 22nd, 2018 3 min read

Na WYCLIFFE MUIA

KWA mara nyingine, Gavana wa Nairobi, Mike Sonko amemkabili vikali Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho huku ikiaminika kuwa mabwenyenye kutoka Mlima Kenya ndio wanatashia kuangusha utawala wa Sonko jijini. 

Wadadisi wanasema wafanyabiashara wakuu jijini, hasa kutoka Mlima Kenya pamoja na wanasiasa kadhaa kutoka chama cha Jubilee wanahisi Bw Sonko anaendesha masuala ya kaunti bila kuwahusisha ilhali wamewekeza mabilioni ya pesa jijini humo.

“Bw Kibicho ni kipaza sauti tu cha watu wenye ushawishi kutoka Mlima Kenya ambao wanahisi kupuuzwa na uongozi wa Sonko. Uteuzi wa naibu gavana wa Nairobi ndio umesababisha kupanda kwa joto katika City Hall,” anasema Prof Herman Manyora, mhadhiri wa maswala ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

 

Madai ya Sonko ni kweli

Kwa mujibu wa Prof Manyora, kauli ya Sonko kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wanaokutana usiku kupanga njama ya ‘kumruka’ Naibu Rais William Ruto ifikapo 2022, huenda ilikuwa ya kweli kutokana na hisia za kisiasa zinazotoka Mlima Kenya.

“Sonko ana habari zake za kijasusi ambazo amewekeza pesa nyingi. Haitakuwa ajabu watu anaowashutumu kwa kuvuruga utendakazi wake ndio wanaongoza mikutano hiyo,” anaongeza Prof Manyora.

Katika mahojiano na Kameme FM, Sonko alidai Bw Kibicho na maafisa wengine watatu wakuu serikalini wanaongoza kampeni za jamii ya Agikuyu kumtema Bw Ruto kuelekea 2022.

“Kwa sasa nitafichua watu wawili wanaolenga kumhujumu Ruto: Kibicho na Nancy Gitau. Kuna wengine ambao nitawataja baadaye,” Sonko aliambia gazeti moja.

Hata hivyo, Bw Kibicho alikanusha madai hayo akisema kama mkuu wa ujasusi nchini hana habari kuhusu mikutano hiyo ya usiku.

“Ambieni Sonko akome na akabiliane na watu anaotaka kukabiliana na wao kisiasa lakini si kupitia kwangu. Mimi si mwanasiasa na siwezi kuanza kupiga vita naibu rais,” alisema Bw Kibicho.

Kibicho anasema tofauti zake na Sonko zilianza baada ya kumwamrisha atoe bendera ya taifa katika gari lake.

“Ukianza kuzama, unatafuta vitu vya kujishikilia hata vile dhaifu…ambieni Sonko asafishe jiji na aachane na mimi,” alisema Bw Kibicho.

 

Igathe alitetea Jubilee

Masaibu ya Gavana Sonko yanasemekana kuchacha zaidi baada ya aliyekuwa naibu wake Polycarp Igathe kujiuzulu.  Bw Igathe alionekana kuwakilisha na kutetea maslahi ya mabwenyenye wa Mlima Kenya pamoja na wakuu wa chama cha Jubilee.

Ni wakati huo ambapo Sonko, kupitia mtandao wake wa Facebook alidokeza mpango wake wa kutaka kujiuzulu kutokana na ‘changamoto nyingi zinazomkumba.’

“Mjue hii kazi imekuwa ngumu na iko karibu kunishinda. Na sio mambo ya bendera. Hizo nimekubali kutoa kama nilivyoshauriwa na Bw Kibicho lakini nitawaambia hivi karibuni ni kwa nini nataka kung’atuka mnishauri,” taarifa iliyochapishwa katika Facebook yake ilinukuu.

Baadaye, Sonko alipuuzilia mbali taarifa hiyo akishutumu vyombo vya habari kwa kusambaza propaganda.

Miongoni mwa watu waliotajwa kwa kushawishi uteuzi wa Bw Igathe ni pamoja na mwenyekiti wa benki ya Equity Peter Munga, naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe na mmoja wa mshauri wa Rais Uhuru Kenyatta kutoka Ikulu.

Mfanyabiashara Chris Kirubi ambaye alikataa nafasi ya kuwa mshauri wa Sonko vilevile alisemekana kuwa na ushawishi mkubwa katika uteuzi wa Bw Igathe.
Wafanyabiashara hao wanatoka Kaunti ya Murang’a.

 

Wawekezaji wa Murang’a

Mbunge wa Kiharu, Irungu Kang’ata anasema kuondoka kwa Igathe kulipangua mipango ya chama cha Jubilee jijini na sharti nafasi yake ichukuliwe na mtu kutoka eneo la Kati.

“Sisi watu wa Murang’a tumewekeza sana Nairobi na hata kuna mtaa unaofahamika kama ‘Murang’a ndogo’ jijini. Ni muhimu tupate mwakilishi katika usimamizi wa kaunti ya Nairobi,” alinukuliwa Bw Kang’ata.

Mchanganuzi wa kisiasa Martin Andati asema Mlima Kenya walimuunga mkono pakubwa Peter Kenneth katika ugavana wa Nairobi 2017 lakini umaarufu wa Sonko ulilazimu apewe tiketi ya Jubilee, hivyo bado hawana Imani na uongozi wake.

“Walikuwa wanataka mtu atakayechunga biashara zao lakini Sonko anaonekana kubomoa hata makundi haramu ya kibiashara jijini ili kuokoa mabilioni ya pesa zinazoishia kwa mikono ya watu wachache,” alisema Bw Andati.

Kulingana na Bw Andati, iwapo Gavana Sonko atawania tena ugavana, huenda hatatumia chama cha Jubilee.

Tayari Sonko, amefichua kwamba atachagua mwanamke mtaalamu kutoka jamii ya Wakikuyu kuchukua mahali pa Igathe.

 

Ushirikiano na Wakikuyu

“Ninajua nafasi ya naibu gavana inafaa iende kwa Mkikuyu kwa sababu wengi wao waliniunga mkono, lakini nataka niwe huru kumchagua Mkikuyu nimtakaye,” alisema Sonko.

“Nimeshirikiana vyema na Wakikuyu tangu 2010 ambapo walinipigia kura kwa wingi nikiwa Mbunge wa Makadara. Mnamo 2013, pia walinipigia kura kuwa seneta na baadaye nikawa gavana. Wao hawana ukabila na kama wangekuwa wakabila, singekuwa gavana,” akasema.

Miongoni mwa wanawake ambao wamekuwa wakisemekana kuwa kwenye orodha yake ni aliyekuwa Mbunge wa Starehe, Bi Margaret Wanjiru, gwiji wa kibiashara, Bi Agnes Kagure, na aliyekuwa Mwakilishi wa Kaunti ya Kiambu, Bi Ann Nyokabi.

Kutokana na matamshi yake, kuna uwezekano mkubwa kuwa atamchagua Bi Kagure (mzaliwa wa Nyeri) au Bi Nyokabi kwani wengine waliobaki hawajaafiki vigezo alivyoyataja.

Inadaiwa Ikulu pamoja na wafanyabiashara wakuu kutoka Murang’a wanashinikiza kuteuliwa kwa Bi Nyokabi ambaye ni binadmu wa Rais Kenyatta. Hata hivyo Sonko anapendelea Bi Kagure kwa kuwa hana ushawishi mkubwa wa kisiasa, hasa kutoka Mlima Kenya.