MakalaSiasa

JAMVI: Mlima Kenya kuteua msemaji wao katika kongamano la Limuru

May 5th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Huku kambi mbili katika chama cha Jubilee zikiendelea kurushiana lawama kuhusu iwapo eneo la Mlima Kenya linafaa kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto kugombea urais baada ya 2022, eneo hilo linajiandaa kwa kikao cha kumteua atakayerithi Rais Uhuru Kenyatta.

Kulingana na viongozi wa eneo hilo na wadadisi, ni kongamano litakaloandaliwa Limuru kabla ya 2022 ambalo litaamua msemaji wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya na iwapo litamuunga Bw Ruto.

Wanasiasa wa eneo hilo ambao kwa wakati huu hawaegemei mrengo wowote katika chama hicho wanasema kwamba licha ya kongamano hilo kuteua atakayechukua nafasi ya Rais Kenyatta kama msemaji wa jamii za muungano wa GEMA, wataheshimu uamuzi wa rais.

Na kwa vile rais amenukuliwa akisema chaguo la mrithi wake litawashangaza wengi, wadadisi wanahisi kwamba kulingana na yanayoendelea katika chama cha Jubilee, Bw Ruto anapaswa kujiandaa kwa lolote ikiwa ni pamoja na kuachiwa Jubilee kikiwa gae la chama kilichoshinda uchaguzi mkuu wa 2017.

Japo hafai kuzungumzia siasa, waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri wiki hii alinukuliwa akieleza hofu yake na mgawanyiko wa viongozi wa Jubilee eneo la Mlima Kenya akisema kuna haja ya kongamano la kuunganisha eneo hilo.

“Tunapaswa kuunganisha Mlima Kenya kwanza na kuhakikisha tunaongea kwa sauti moja. Tunawajibika kwa watu wetu na tunafaa kuandaa kongamano huko Limuru na kuamua mwelekeo wetu,” alisema Bw Kiunjuri akiwa eneo la Kibirione Kaunti ya Meru.

Katika mkutano huo, Bw Kiunjuri na Gavana wa Meru Kiraitu Murungi, walisema watashauriana na Rais Kenyatta viongozi waliohudhuria kuungana katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, licha ya makundi mawili kuzuka eneo la Mlima Kenya- Tanga Tanga linalomuunga Bw Ruto na Kieleweke linalopinga azima yake, yatakayopitishwa kwenye kikao cha Limuru yataamua mwelekeo wa pamoja wa eneo hilo.

“Kwa sasa inaonekana kama kuna makundi mawili lakini inafaa kueleweka kwamba tangu 2007, eneo la Mlima Kenya limekuwa likichukua mwelekeo mmoja wa kisiasa na unaamuliwa katika mkutano unaofanyika Limuru. Kwa hivyo, ni mkutano huo ambapo jamii zilizo chini ya muungano wa Gema zitaamua iwapo zitamuunga Dkt Ruto na kwa masharti gani,” asema mdadisi wa siasa Raphael Kamau.

Kulingana na Bw Murungi, eneo la Mlima Kenya lina zaidi ya wapigakura milioni sita na linafaa kuwa na usemi mkubwa katika serikali ijayo.

“Siasa zinahusu kujali maslahi ya watu na hatutajiingiza kijinga tu. Ruto ni rafiki yetu lakini kama watu wa Meru, tutalazimika kuketi naye atueleze tutakavyonufaika. Tunasikia kuna miradi ya mabwawa ya maji ya mabilioni ya pesa ilhali hapa Meru ni mtaro wa majitaka wa Sh1 bilioni pekee,” alisema.

Kulingana na Bw Kamau, matamshi ya Bw Murungi yanaashiria kwamba iwapo Mlima Kenya utamuunga Dkt Ruto kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, utafanya hivyo kwa masharti na hilo litafanyika kwenye mkutano wa Gema Limuru.

Aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe ambaye anaongeza juhudi kumzuia Ruto kugombea urais alinukuliwa akisema kwamba eneo la Mlima Kenya liligundua kwamba Ruto hawezi kulinda maslahi ya wakazi wa eneo hilo.

“Kwa sababu ya hofu hii na ikikumbukwa mchango wa Dkt Ruto kwenye kampeni za Rais Kenyatta, iwapo eneo hilo litamuunga mkono, itakuwa kwa masharti yatakayowekwa katika kongamano la Limuru linalohudhuriwa na vigogo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii eneo la Mlima Kenya,” alisema Bw Kamau.

Bw Murungi, mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika jimbo la Mlima Kenya anasema kwamba kuwepo kwa makundi mawili katika eneo hilo ndani ya chama cha Jubilee kunafanya jamii kutumiwa vibaya.

“Hatutaki kusikia Tanga Tanga ambao wanazurura wakisumbua watu. Pia hatutaki kusikia kuhusu Kieleweke. Tunataka umoja jinsi tulivyovunja APK na GNU,” alisema Bw Murungi akirejelea chama cha Alliance Party of Kenya chama alichokuwa akiongoza na Grand National Union of Kenya (GNU) kilichoongozwa na Bw Kiunjuri. Walivunja vyama hivyo kuungana na vingine kuunda Jubilee kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Mchanganuzi wa kisiasa Geff Kamwanah anasema kulingana hali ya kisiasa Mlima Kenya ni wazi haijajiandaa kukabiliana na hali ya kisiasa baada ya Rais Kenyatta kuondoka mamlakani.

“Kwa kawaida, Gema huzungumza kwa sauti moja na uamuzi hutolewa baada ya kongamano la Limuru. Huwa kuna watu wachache wasiokubaliana na uamuzi ambao hunyamazishwa kwenye uchaguzi na wengine wao huwa wamepandwa kama mikakati ya kutimiza malengo ya kisiasa ya kijamii,” aeleza.

Anasema kwamba kabla ya chaguzi kuu zilizopita tangu 2007, eneo la Mlima Kenya huwa limeungana na hali kama hiyo itajirudia kabla ya 2022.

“Mkutano wa Limuru hutanguliwa na mingine ya siri ambayo kwa wakati huu nina hakika inaendelea. Kelele unazosikia pia ni sehemu ya maandalizi wanamikakati wakipima hewa kabla ya wakati huo. Kitaeleweka baada ya kongamano la Limuru,” asema Bw Kamwanah.

Wadadisi wanasema si ajabu eneo hilo likaamua kuwa na chama tofauti kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na kukitema Jubilee iwapo halitamuunga Dkt Ruto ikizingatiwa hatua za viongozi kadhaa wa eneo hilo kusajili vyama vya kisiasa. Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria na mbunge wa Gatundu Kusini ni miongoni mwa waliosajili vyama.