JAMVI: Mradi watia doa azma ya Shahbal kuwania ugavana

JAMVI: Mradi watia doa azma ya Shahbal kuwania ugavana

Na WINNIE ATIENO

SIASA za uwaniaji ugavana katika uchaguzi ujao zimechukua mkondo mpya katika Kaunti ya Mombasa, baada ya mfanyabiashara Suleiman Shahbal kuanza kukosolewa kuhusu biashara zake.

Bw Shahbal, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitumia weledi wake na uaminifu wa usimamizi wa kibiashara kujaribu kuwashawishi wapigakura wamchague kuwa gavana wa pili wa kaunti hiyo, huenda sasa akalazimika kujipanga upya baada ya utata uliozuka kuhusu mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za kisasa mtaani Buxton.

Wachanganuzi wa kisiasa wanasema kuwa, uamuzi wa kamati ya seneti kuagiza ujenzi huo unaoendelezwa na kampuni ya mfanyabiashara huyo usitishwe, umetia doa nyota yake iliyokuwa imeanza kung’aa.

Bw Shahbal amekuwa akijipigia debe kwa wapigakura akitumia mradi huo wa Sh6 bilioni kama mojawapo ya mifano ya jinsi alivyo na uwezo wa kufanikisha mipango itakayoboresha maisha ya wakazi wa Mombasa na kuongeza nafasi za ajira ambazo zimepotea eneo hilo.

“Nyota yake iko hatarini kufifia kutokana na uamuzi wa maseneta. Ikiwa uamuzi huo utatekelezwa, ahadi aliyotoa kwa wakazi ikiwemo kuleta nafasi za ajira haitatimia na hilo litaibua maswali chungu nzima miongoni mwa wakazi,” alisema Bw Philip Mbaji, mchanganuzi wa siasa.

Kwa mujibu wa wadadisi, hatua ya kamati ya seneti inayosimamia masuala ya uchukuzi na ujenzi kuzamia suala hilo, huenda pia ikaibua masuala kuhusu uadilifu wake wa kiusimamizi na biashara.

Wiki iliyopita, kamati hiyo ilisitisha ujenzi hadi pale malalamishi ya wapangaji waliofurushwa yatasikilizwa na kuamuliwa.

Kamati hiyo ikiongozwa na Seneta wa Kiambu, Bw Kimani Wamatangi, ililalamikia pia jinsi mradi huo wa Sh6 bilioni ambao uliruhusiwa na mahakama kuendelea, unavyofanywa kwa usiri mkubwa ilhali ardhi inayotumiwa ni ya umma.

Hata hivyo, ilibainika kuwa agizo hilo lilipuuzwa.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, ambaye ni mmoja wa wapinzani wakuu wa Bw Shahbal katika kinyang’anyiro kijacho cha ugavana, alivalia njuga suala hilo na kuunga mkono msimamo wa maseneta.

“Masuala yaliyowasilishwa na kamati hiyo ya seneti ni mazito na yanafaa yatatuliwe. Hakuna mtu asiyetaka maendeleo, lakini lazima sheria ifuatwe kikamilifu. Sheria kuhusu Ununuzi wa Mali ya Umma inatilia mkazo masuala kama vile utoaji zabuni. Je, zabuni ya huu mradi ilifaa kutolewa bila wawekezaji wengine kupewa nafasi ya kuishindania? Sheria inasema wazi kuwa, iwapo mradi wa umma unagharimu zaidi ya Sh5 bilioni, Mwanasheria Mkuu ni lazima ahusishwe,” akasema mbunge huyo.

Wanasiasa hao wawili wanatarajiwa kushindania tikiti ya ODM kuwania ugavana, baada ya Bw Shahbal kuhamia chama hicho kutoka Wiper miezi michache iliyopita.

Mbali na Bw Nassir, viongozi wengine wanaomkaba koo Bw Shahbal kuhusu mradi huo ni mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali, mwenzake wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, na madiwani Charles Kitula (Freretown) na Faith Mwende (Kipevu).

Gavana Hassan Joho, alitakiwa kufika mbele ya kamati ya seneti kubainisha kandarasi ilivyopeanwa kwa mradi huo wa Buxton Point.

Kamati hiyo pia inataka kufafanuliwa umiliki wa ardhi ya Buxton, kwani baadhi ya walalamishi wanadai kuwepo uwezekano wa njama ya unyakuzi wa ardhi hiyo.

“Ujenzi hauwezi kuendelea bila kuwasikiliza wakazi. Huu mradi una siri nyingi ambazo tunataka Gavana Joho aje kutufichulia,” alisema Bw Wamatangi.

Hata hivyo, afisa mkuu anayesimamia mradi huo, Bw Ahmed Badawy alisema kwamba mradi utaendelea licha ya uamuzi wa maseneta.

Kulingana naye, hakuna agizo lolote lililotolewa kwa wasimamizi wa mradi huo kuusitisha bali maseneta walizungumza tu na wanahabari.

“Mradi unaendelea. Nataka kuwahakikishia kwamba tumekuwa tukifuata sheria kikamilifu, na mahakama zilitoa uamuzi kuhusu suala hili mara mbili na tukaruhusiwa tusonge mbele,” akasema Bw Badawy.

You can share this post!

Gent anayochezea Okumu yabebesha mabingwa Club Brugge kapu...

Umuhimu wa madini ya zinki mwilini