MakalaSiasa

JAMVI: Muungano wa Isaac Ruto na Gideon Moi ni hatari kwa Ruto

March 31st, 2019 3 min read

Na PETER MBURU

BAADA ya kimya cha miezi kadhaa, aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto siku chache zilizopita alijitokeza mbele ya umma, baada ya kuhudhuria hafla ya kuchangisha pesa, pamoja na seneta wa Baringo Gideon Moi.

Wawili hao walihudhuria hafla hiyo katika Kaunti ya Bomet, karibu miezi minne tangu magavana wa eneo la Bonde la Ufa pamoja na viongozi wengine wandani wa Naibu Rais William Ruto kumtembelea Isaac nyumbani kwake Novemba mwaka jana.

Katika hafla hiyo ya majuzi, Bw Ruto alikashifu viongozi ambao wamekuwa wakishambuliana siku za majuzi, huku akisema anaunga mkono wito wa katiba kufanyiwa marekebisho.

Matamshi yake yalionekana kukinzana na Naibu Rais pamoja na kambi yake ambao kwa muda wamekuwa wakipinga wito wa referenda, huku kwa kukashifu viongozi wanaotoa matamshi ya kugawanya Wakenya, akionekana kuwalenga viongozi wa Bonde la Ufa ambao siku za majuzi wamekuwa kipaumbele kudai kuwa vita dhidi ya Ufisadi ni mpango wa kumchafulia jina Naibu Rais na jamii ya Kalenjin.

“Hatutaki matusi na hatutaki jamii kupigana na nyingine. Mimi naunga mkono mambo ya kueneza umoja katika Kenya yetu, hiyo ni ya lazima. Nawashauri wabunge hatutaki matusi kutoka upande mmoja hadi mwingine, hiyo haitusaidii,” akasema.

“Naunga mkono kubadilishwa kwa hii katiba, kwa kuwa mimi binafsi maoni yangu ni kuwa mawaziri wanafaa kuteuliwa miongoni wa wabunge waliopo,” akasema gavana huyo wa zamani wa Bomet.

Bw Moi naye alituma ujumbe sawa na huo baada ya kuketi na viongozi kadhaa wa kaunti hiyo, akidai kuna viongozi wanaojaribu kutenga jamii ya Kalenjin na Wakenya wengine, jambo ambalo alilikashifu.

“Tujichunge tusije tukatenga jamii yetu kutoka kwa Wakenya wengine. Sharti tulinde heshima yetu na sifa nzuri ambayo jamii imejenga kwa miaka mingi. Pia tusisahau kuwa nafasi ya uongozi ambayo tumepewa na jamii si ya kuendeleza maslahi ya kibinafsi. Sharti tuheshimu na kuhudumia wananchi ipasavyo,” akasema Bw Moi.

Matamshi ya viongozi hao na kushiriki kwao katika hafla moja kulikuja baada ya kimya cha muda mrefu kutoka kwa Bw Ruto, kufuatia ziara ya Magavana Jackson Mandago (Uasin Gishu), John Lonyagapuo (West Pokot), Paul Chepkwony (Kericho) na Samuel Tunai (Narok), pamoja na mwandani wa Naibu Rais, Bw Farouk Kibet awali Novemba 2018, ziara ambayo aidha ilikuja baada ya misururu ya mikutano baina ya Bw Ruto, Rais Uhuru na naibu wake William Ruto.

Wakati huo, Gavana Mandago alidokeza kuwa Bw Ruto angepewa kazi serikalini, japo hilo halijafanyika.

“Nimezungumza na Rais na naibu wake kuhusu kumleta Isaac mezani na uwepo wetu leo ni kumrai ajiunge nasi. Na tunataka awe sehemu ya serikali ili asaidie katika masuala fulani,” Bw Mandago akasema.

Japo hakuzungumza siasa wakati huo, Bw Ruto alialikubali kushirikiana na serikali, lakini baadaye mwezi huo, walipohudhuria hafla pamoja na Naibu Rais alionyesha kumuunga mkono kwenye azma yake ya Urais 2022.

Desemba mwaka jana, takriban miezi miwili baada ya ziara ya magavana hao nyumbani kwake, Bw Ruto aliashiria kukata tamaa na maelewano yake na serikali, wakati alipohudhuria hafla pamoja na mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter ambayo ujumbe ulikuwa kuwa hatavunja chama chake cha ‘Chama Cha Mashinani’ (CCM).

Baada ya miezi miwili tena, amejitokeza akiwa pamoja na Bw Moi, hasimu mkubwa wa Naibu Rais kisiasa, wakati huu akikashifu viongozi wanaodhaniwa kuwa wa kambi ya Dkt Ruto na kueleza kuwa anaunga mkono wito wa referenda.

Kulingana na baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa, kujitokeza kwa viongozi hao pamoja wakieneza ujumbe wa kumchafua Naibu Rais ni hatari kwa Dkt Ruto na ni hali inayoweza kuwa kizingiti kikubwa kwake anapolenga kuingia ikulu 2022.

Wakili Kipkoech Ngetich anahoji kuwa sauti za Isaac Ruto, Gideon Moi, Alfred Keter na viongozi wengine ambao wanazidi kumchafua Dkt Ruto ni tishio kubwa na ikiwa kiongozi huyo hatafanya juhudi kuzizima, huenda akajutia siku za usoni.

“Isaac ni mwanasiasa mwenye nguvu na mwenye uwezo wa kuhamasisha watu wengi kufanya jambo, hili lilidhihirika katika muhula wa kwanza wa ugatuzi. Wanapoungana na Gideon na Bw Keter na wote wana sauti zinazosikika ndani na nje ya Bonde la Ufa, hii inakuwa hatari,” akasema Bw Ngetich “Sharti Naibu Rais atafute mbinu za kumaliza hizi sauti ama atashangaa.”

Wakili huyo anahoji kuwa huenda tofauti baina ya Dkt Ruto na Bw Ruto hazijaisha, lakini wa kuathirika ni Dkt Ruto kwani kwa Bw Ruto kujiunga na Bw Moi, anammalizia umaarufu Naibu Rais.

“Vita vya kumchafua Dkt Ruto machoni mwa raia vinazidi kufanikiwa na hivyo hafai kuwa na pingamizi kutoka ngome yake,” akasema.