JAMVI: Mvutano ODM wazidisha ubutu kwa makali ya Raila

JAMVI: Mvutano ODM wazidisha ubutu kwa makali ya Raila

Na LEONARD ONYANGO

MVUTANO unaoendelea ndani ya ODM huenda ukamfanya kinara wa chama hicho Raila Odinga kukosa makali iwapo ataamua kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanaonya kuwa hatua ya chama cha ODM kumwadhibu mbunge wa Rarieda Otiende Amollo kwa kumng’oa kutoka wadhifa wa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) na kutishia kumchukulia hatua Seneta wa Siaya James Orengo, ni pigo kwa juhudi za Bw Odinga kutaka kuingia Ikulu 2022.

Aliyekuwa Katibu wa Mipango wa ODM Wafula Buke anasema kuwa mvutano huo utakosesha ODM nguvu hivyo kumnyima Bw Odinga fursa ya kushinda urais.

“Kumekuwa na ripoti kwamba kuna baadhi ya wakuu serikalini ambao wamekuwa wakipanga njama ya kutaka kumwacha Bw Odinga akiwa mpweke kisiasa.

“Ikiwa kweli kuna mpango huo, basi mvutano huo ndani ya ODM itakuwa fursa murua kwao kuendeleza juhudi hizo. Mvutano huo hauna tija kwa ODM bali unasababisha chama kuwa dhaifu,” anasema Bw Buke.

Kumekuwa na ripoti kwamba baadhi ya wakuu serikalini wamekuwa wakiunda njama ya kutaka kumaliza ushawishi wa ODM katika ngome zake; ambazo ni maeneo ya Pwani, Magharibi, na Nyanza. Huku viongozi wa ODM wakiendelea na juhudi za kutaka kuunda chama kitakachotetea masilahi yao, juhudi zinaendelea kuzima umaarufu wa chama hicho katika maeneo ya Magharibi.

Kumekuwa na juhudi za kuvumisha chama cha Amani National Congress (ANC) chake Musalia Mudavadi na Ford Kenya kinachoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Bw Mudavadi na Seneta Wetang’ula wameafikiana kushirikiana katika kinyang’anyiro cha Urais.

Vyama hivyo viwili viko ndani ya muungano wa Kenya One Alliance (OKA) ambao pia unajumuisha chama cha Kanu kinachoongozwa na Seneta wa Baringo Gideon Moi.

Rais Uhuru Kenyatta anaegemea muungano wa OKA. Gavana wa Kakamega ambaye ndiye muhimili wa Bw Odinga katika maeneo ya Magharibi amejitokeza na kuunga mkono kundi la Seneta Orengo na Dkt Otiende.

Bw Orengo, Gavana Oparanya na Dkt Otiende wanapinga ugavi wa maeneobunge mapya 70 yaliyopendekezwa ndani ya Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Viongozi hao wanasema kuwa eneo la Mlima Kenya limependelewa kwa kutengewa maeneobunge 35 huku maeneo mengine yakipunjwa.

Kumng’oa dkt Otiende kutoka wadhifa wake bungeni, kulingana na Gavana Oparanya, hakukufaa na hakuna manufaa kwa ODM.

Bw Orengo amejitokeza kuwa hatatishika na yuko tayari kukabiliana na Bw Odinga ‘kupigania haki’.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bw Odinga kutofautiana kisiasa na Bw Orengo tangu 2002.

Japo baadhi ya wadadisi wanasadiki kwamba uasi huo unasababisha na siasa za ugavana 2022 katika Kaunti ya Siaya, mdadisi wa masuala ya kisiasa Mark Bichachi anasema kuwa mvutano huo unatokana na juhudi za kutaka kumrithi Bw Odinga.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga. Picha/ Maktaba

“Mvutano tunaoshuhudia ndani ya ODM unatokana ubabe wa kutaka kurithi uongozi wa jamii ya Waluo. Bw Orengo anajiona kwamba yeye ndiye atakuwa kiongozi wa jamii baada ya Odinga.

“Orengo anatumia maeneo 70 kujidhihirisha kwamba yeye ndiye mtetezi wa jamii. Lakini juhudi hizo huenda zikagonga mwamba kwani huu si wakati mwafaka wa kupigania urithi,” anasema Bw Bichachi.

Bw Orengo tayari ameonyesha nia yake ya kutaka kuwania ugavana wa Siaya 2022. Dkt Otiende aliambia Taifa Jumapili kuwa atatetea kiti chake cha ubunge wa Rarieda.

“Sina nia ya kuwania ugavana, azma yangu ni kutetea kiti cha ubunge,” akasema Dkt Otiende.

Gavana wa Migori Okoth Obado pia ameapa kumaliza ushawishi wa Bw Odinga katika maeneo ya Nyanza.

Bw Obado wiki iliyopita alikutana na Bw Mudavadi wiki chache baada ya kutembelewa na Gavana wa Nandi Stephen Sang ambaye ni mwandani wa Naibu wa Rais William Ruto.

Profesa Medo Misama anasema kuwa iwapo Bw Odinga atakuwa na maadui wengi katika eneo la Nyanza, atakosa nguvu ya kisisa hivyo kutoa mwanya kwa muungano wa OKA na Dkt Ruto kupenya.

You can share this post!

TAHARIRI: Ongezeko la ajali linatia wasiwasi

NASAHA ZA RAMADHAN: Mwenyezi Mungu hurehemu na kusamehe...