Makala

JAMVI: Mwaka wa kwanza bungeni ulivyomfifisha Jicho Pevu

October 22nd, 2018 3 min read

Na VALENTINE OBARA

DAU la kisiasa la Mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali, linazidi kuyumbishwa na mawimbi makali, mwaka mmoja pekee baada ya kushinda kiti cha kisiasa cha kitaifa kwa mara ya kwanza.

Sawa na wanasiasa wengine wengi wanaotoka katika maeneo yaliyo na ushindani mkubwa, safari ya kisiasa ya Bw Ali almaarufu ‘Jicho Pevu’ ambaye alipata umaarufu nchini na kimataifa kwa weledi wake wa habari za kiupekuzi, haijawa rahisi kufikia sasa.

Amekuwa akikashifiwa vikali hasa kwenye mtandao wa kijamii na kubandikwa jina ‘Jicho Pesa’ kutokana na ushirikiano wake wa karibu na Naibu Rais William Ruto ambaye huandamana naye kwenye baadhi ya ziara zake za harambee.

Lakini kwenye mahojiano ya awali, mbunge huyo amekuwa akijitetea kwamba ushirikiano huo ni kwa minajili ya kuletea wakazi wa Nyali maendeleo waliyotamani kwa muda mrefu.

Wengi wanaomkashifu wanafanya hivyo kwa kuwa wakati alipokuwa mwanahabari, Bw Mohammed alikuwa katika mstari wa mbele kukosoa maovu yaliyokuwa yakitendeka kwenye Serikali ya Jubilee na aliahidi kuendeleza upekuzi huo kama angeshinda ubunge.

Miongoni mwa maovu aliyokuwa akifichua ni kuhusu ufisadi na mauaji ya kiholela yaliyokuwa yakitekelezwa na polisi na hivyo basi haikutarajiwa angekuwa mwandani wa kisiasa wa kiongozi mkuu katika serikali hiyo hiyo baada ya kushinda ubunge.

Masaibu yake mikononi mwa wakosoaji yaliongezeka wakati video ilipofichuka majuzi kumwonyesha akimbebea Bw Ruto bahasha lenye Sh5 milioni wakati wa harambee kanisani Mombasa.

Bw Mohammed sasa amepanga kupeperusha habari za kiupekuzi kuhusu maovu mbalimbali ambayo yametokea nchini tangu wakati wa kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita.

Kwenye maelezo aliyotoa kuhusu ripoti hiyo, alisema itahusu mauaji ya aliyekuwa mkuu wa Teknolojia za Habari na Mawasiliano katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Chris Msando, kiapo cha ‘rais wa wananchi’ Bw Raila Odinga, na mauaji yaliyotekelezwa na polisi kwa watu wasio na hatia.

Upekuzi huo kwa jina Dunia Gunia pia unalenga kufichua masuala kuhusu “siasa za usaliti” na kujibu swali kuhusu tunapoelekezwa na mwafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

“Ni nani anayempumbaza mwenzake? Jiamulie mwenyewe,” anasema.

Nia yake katika kuwania ubunge ilianza kuonekana miaka michache kabla ya 2017 wakati maandishi ya kumpigia debe yalipoanza kuonekana kwenye kuta za majengo ya sehemu mbalimbali za eneobunge la Nyali.

Wakati huo, Bw Ali hakujitokeza wazi kukubali wala kukataa kuhusu ombi hilo na kuacha wengi wakijiuliza kuhusu waliohusika katika kuandika maandishi hayo kutani.

Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu kabla mwanahabari huyo aanze kuonekana hadharani na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, ndipo dalili zikawa wazi kwamba alinuia kujitosa katika siasa.

Aliamua kuwania bunge kama mgombeaji huru baada ya kulalamikia dhuluma katika ODM kwenye kura za mchujo huku uhasama kati yake na Gavana wa Mombasa Hassan Joho ukizidi kutokota.

Baadaye ushindi wake ulipingwa mahakamani lakini ikaamuliwa alishinda kwa njia ya haki.

Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu Boniface Mwangi, ambaye ni mwandani wa mbunge huyo, alisema inaridhisha kumwona akianza kurejelea upekuzi wake wa maovu serikalini lakini atahitaji juhudi zaidi kurudisha imani kwa wafuasi ambao wanamtilia shaka.

“Ameamua kurejea upande wa Wakenya ambao hawakujali kuhusu vyama vya kisiasa walivyounga mkono wakamsaidia na kumpigia kura akiwa mgombeaji huru. Natumai sasa atasalia upande huu,” akasema Bw Mwangi, kwenye mtandao wa kijamii.

Hata hivyo, Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen, anamshauri mbunge huyo apuuze watu wanaomkashifu mitandaoni na badala yake atilie maanani chochote kile kinachoweza kusaidia wakazi wa eneobunge lake.

Kulingana na Bw Murkomen, maoni mengi ya watumizi wa mitandao ya kijamii hayafai kutegemewa na wanasiasa kwani huwa yanapotosha.

“Jitolee kikamilifu kuhudumia wakazi wa eneobunge lako kwani wao ndio watakaokupa alama za utendakazi baada ya miaka mitano. Ni huduma unazotoa kwa wananchi ambazo zitakusaidia kushinda uchaguzini na kukuletea sifa ya kudumu kwa miaka mingi,” akasema.

Kwa sasa, inasubiriwa kuonekana kama ripoti hiyo ya upekuzi wa Jicho Pevu itasaidia kumrudishia Bw Ali sifa aliyokuwa nayo awali, hasa katika mitandao ya kijamii, au kama itachochea Wakenya kumkashifu hata zaidi ya jinsi ilivyo.