JAMVI: Mwaura alivyojikwaa na kujiponza kisiasa

JAMVI: Mwaura alivyojikwaa na kujiponza kisiasa

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Chama cha Jubilee (JP) kumtimua aliyekuwa Seneta Maalum, Bw Isaac Mwaura, kutoka chama hicho imezima nyota ya mojawapo ya wanasiasa waliotazamwa kwa matumaini makubwa.

Bw Mwaura alipoteza nafasi yake rasmi Jumanne, baada Spika wa Seneti, Kenneth Lusaka kutangaza nafasi yake kuwa wazi.Hali iliendelea kumzidia maji Bw Mwaura baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumtangaza aliyekuwa Seneta wa Samburu, Bw Sammy Leshore, kuchukua nafasi yake.

Hata hivyo, masaibu hayo yalimwandama licha yake kupata agizo la mahakama kuizuia Jubilee kujaza nafasi yake.Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi wanasema hatua hiyo ni pigo kubwa kwa Bw Mwaura, kwani alionekana kama mwanasiasa ambaye angeleta mwanga mpya, hasa kwa walemavu.

“Kama mwanasiasa aliyekuwa akiendelea kujijenga kisiasa, hilo ni pigo kubwa kwake. Angetumia nafasi hiyo kujijenga badala ya kuanza kufarakana na wakubwa wake katika Jubilee,” asema Bw Martin Andati, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kenyatta mnamo 2006, Bw Mwaura alijiunga na chama cha ODM kama mwanachama wa kawaida, lakini akapanda ngazi hadi kuwa Katibu Mkuu wa Walemavu.Kwenye uchaguzi mkuu wa 2007, Bw Mwaura alishiriki pakubwa kumpigia debe Bw Odinga.

Kutokana na hilo, aliteuliwa kuwa mshauri mkuu kuhusu masuala ya makundi yaliyotengwa katika jamii katika Afisi ya Waziri Mkuu kati ya 2010 na 2012.Mnamo 2013, aliteuliwa kama mbunge maalum na ODM.Mwaka 2016, aligura ODM na kujiunga na Jubilee.

Alijaribu kuwania ubunge katika eneo la Ruiru, kaunti ya Kiambu, lakini akashindwa kwenye shughuli za mchujo.Hata hivyo, “aliokolewa kisiasa” na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuteuliwa kama Seneta Malum mnamo 2017, kuwakilisha watu wenye ulemavu. Kutokana na kutimuliwa kwake, wadadisi wanamlaumu kwa “kujikwaa mwenyewe kisiasa.”

Wakosoaji wake wanamtaja kuwa mwanasiasa anayetapatapa na asiyekuwa na msimamo wa kisiasa hata kidogo.“Baada ya kuteuliwa na Jubilee, Bw Mwaura alikuwa na nafasi nzuri kujiboresha kisiasa ili kuhakikisha hangekumbwa na vikwazo alivyokumbana navyo 2017,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wanasema ukakamavu wake ulionekana mnamo 2014, wakati aliwaongoza wanachama wa ODM kulalamikia kuondolewa kwa majina yao katika sajili ya upigaji kura katika hali tatanishi.

Ni kwenye kizaazaa hicho ambapo alikuwa miongoni mwa waliowakabili watu waliovuzua ghasia kwenye uchaguzi huo maarufu kama “Men in Black.”

Licha ya ukakamavu huo, masaibu ya kiongozi huyo yanadaiwa kuanza Desemba mwaka uliopita, baada ya kutangaza kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Bw Mwaura alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa kusherehekea ushindi wa mbunge Feisal Bader (Mswambweni) katika Kaunti ya Kwale.Kwenye mkutano huo, alisema imefika wakati kwa “vijana kuchukua uongozi wa nchi, ambao umeendelea kushikiliwa na familia chache.”

“Kuanzia leo mimi ni mwanachama wa ‘Hustler Nation (Muungano wa Watu Maskini). Tumechoshwa na uongozi wa familia chache tangu tulipojipatia uhuru. Wakati umefika tuikomboe Kenya,” akasema.

Alizilaumu za Mzee Jomo Kenyatta na marehemu Daniel Moi, akisema zimeitawala Kenya kwa zaidi ya miaka 50.Matamshi yake yalionekana kumkera Rais Kenyatta, aliyesema kuwa ikiwa kuna yeyote katika chama hicho aliyechoshwa na uongozi wake, basi aondoke.Rais pia alijitetea vikali, akisema wananchi ndio walimchagua.

“Kama umechoshwa na uongozi wa watu wa familia chache basi waendee wananchi uchaguliwe pia kwani hata nafasi ulio nayo ni kitokana na kura yangu,” akasema Rais, kwenye kauli iliyoonekana kumlenga Bw Mwaura.

Ni kuanzia hapo ambapo wadadisi wanasema “kitumbua chake kilianza kuingia mchanga.”“Huwezi kumtukana kiongozi aliyekupa kazi na utarajie kuendelea kuwa kazini. Ilikuwa wazi lazima angetimuliwa chamani. Huo ni ukaidi wa wazi,” asema Bw Muga.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe, anamtaja Bw Mwaura kama “mwanasiasa mwenye tamaa” anayetegemea “kuvuna tu kutoka kwa vyama vya kisiasa.”

“Alisaidiwa na ODM kwa kuteuliwa kama mbunge maalum. Jubilee ilimteua kama Seneta Maalum. Aligura Jubilee na kujiunga na UDA akilenga kupata uteuzi baada ya uchaguzi mkuu ujao,” akasema Bw Murathe.

Kando na Bw Mwaura, maseneta wengine wanaotarajiwa kukabiliwa na chama kwa madai ya kukiuka kanuni za chama ni Bi Millicent Omanga, Victor Prengei, Mary Seneta, Falhada Dekow na Naomi Waqo.

Kama Bw Mwaura, watano hao wanalaumiwa kwa kukiuka kanuni za chama, hasa kwa kujiunga na mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao umekuwa ukimpigia debe Dkt Ruto kuwania urais 2022.

Watetezi wa Bw Mwaura wanamtaja kuwa mwanasiasa mwenye shujaa na mwenye msimamo huru, anayeadhibiwa kutokana na imani zake za kisiasa.

Maseneta James Orengo (Siaya) na Irungu Kang’ata (Murang’a) wanamtaja kuwa mwanasiasa mchanga, aliye na mustakabali mzuri kwenye siasa za Kenya.

Wawili hao wanasema vyama vya kisiasa vinapaswa kuwa huru katika maamuzi yake, wala havipaswi kudhibitiwa na viongozi wake vinapofanya maamuzi muhimu.

You can share this post!

JAMVI: Mbio za Ngilu kutuliza zogo, uasi katika ODM

KNUT: Walalama Sossion amesambaratisha chama