Makala

JAMVI: Ndiye mrithi wa Uhuru Mlimani?

July 5th, 2020 3 min read

Na WANDERI KAMAU

JUHUDI za kumjenga upya mwanasiasa Peter Kenneth kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta katika ukanda wa Mlima Kenya zimeanza kushika kasi, huku ikiripotiwa kuwa mpango huo unaendeshwa na wazee, wanasiasa, viongozi wa kidini na mabwanyenye wenye ushawishi katika eneo hilo.

Duru zinasema kuwa mikakati ya kumjenga mwanasiasa huyo imekuwa ikiendeshwa kichinichini kwenye mikutano ya faragha katika maeneo mbalimbali, ambapo mbinu moja itakuwa ni “kumjengea njia” atakayotumia kujinadi kwa wananchi kabla ya 2022.

Kulingana na wadadisi, juhudi hizo zilidhihirika wazi Jumamosi iliyotangulia, wakati baadhi ya viongozi katika Kaunti ya Murang’a walimrai Rais Kenyatta kumteua Bw Kenneth kama waziri, kwenye mageuzi ya baraza la mawaziri yanayotarajiwa wakati wowote.

Viongozi hao walitoa kauli hizo walipofanya ziara maalum katika Shule ya Msingi ya Mabae, eneobunge la Gatanga, wakimsifu Bw Kenneth kwa kuwa kiongozi ambaye ana rekodi nzuri ya maendeleo.

Bw Kenneth anatoka katika kaunti hiyo na alihudumu kwa karibu miaka 15 kama mbunge wa Gatanga.

Viongozi hao walijumuisha wabunge Nduati Ngugi (Gatanga), Peter Kimari (Mathioya), Katibu katika Wizara ya Maji Bw Joseph Wairagu na Naibu Waziri wa Elimu, Bw Zack Kinuthia.

Wakihutubu, viongozi hao walimtaja Bw Kenneth kama “kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kuliunganisha eneo hili”.

“Bw Kenneth ni mmoja wa watoto wetu. Tungemwomba Rais Kenyatta kumkumbuka kwenye mageuzi ya baraza la mawaziri anayotarajiwa kufanya,” akasema Bw Nduati.

Miongoni mwa watu wanaoelezwa kushiriki kichinichini kwenye juhudi hizo ni bwanyenye Peter Munga, Askofu Lawi Imathiu (ambaye ni mmoja wa viongozi wa Chama cha Kitamaduni cha jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru-GCA) na viongozi wa matawi mbalimbali ya Baraza la Wazee la Agikuyu (KCE).

Kulingana na baadhi ya washirika wa karibu wa Bw Kenneth, harakati zake za kuanza kuonekana katika mikutano ya kisiasa ni “matayarisho ya mapema kwa safari ndefu ambayo ameianza.”

Bw Kenneth amekuwa kimya wala hajawa akionekana sana kwenye mikutano ya umma tangu kushindwa na Gavana Mike Sonko kwenye kinyang’anyiro cha ugavana katika Kaunti ya Nairobi mnamo 2017.

Waziri

“Unapojitayarisha kwa safari, lazima uchukue muda kujiandaa vizuri kwa mwendo mrefu utakaosafiri. Hatujawa kimya bila kuangalia mbele,” akaeleza kimafumbo mshirika wake ambaye hakutaka kutajwa.

Wachanganuzi wa siasa wanaungama kauli hiyo, wakisema kuwa hatua ya Bw Kenneth kuanza kuonekana hadharani akitoa semi kali kuhusu mwelekeo wa siasa wa nchi, inamsawiri kama mwanasiasa anayejitayarisha kwa kinyang’anyiro kikubwa cha kisiasa.

Kulingana na Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa, ujumbe fiche kwenye kauli za wanasiasa waliomshinikiza Rais Kenyatta kumteua Bw Kenneth kama waziri ni kuwa, huo ndio mpango mkuu uliopo.

“Kinyume na ilivyo kawaida yake, Bw Kenneth alitumia ndege aina ya helikopta kuwasili kwenye mkutano huo. Hilo liliashiria uwezo mkubwa kisiasa alio nao ama anaojitayarisha kupata. Pili, hatua ya viongozi kutoa kauli hiyo wakiwa katika eneo la Gatanga, inaonyesha kuwa wanamtafutia baraka za nyumbani kabla ya kupewa jukumu la kujipigia debe kwingineko. Hilo linalenga kuhakikisha kuwa atakubalika na watu kama kiongozi wao, ikiwa Rais Kenyatta atamteua kama waziri,” asema Bw Mutai.

Kumekuwa na minong’ono kuwa huenda hadi mawaziri wanane wakapoteza nafasi zao za uwaziri, hasa wale wanaoonekana kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto ama utendakazi wao haumridhishi Rais Kenyatta, anapopania kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo kabla ya kumaliza muhula wake.

Ni kwa mantiki hiyo ambapo Rais anatarajiwa kufanya mageuzi hayo, kama alivyofanya kwenye Seneti na Bunge la Kitaifa mwezi Juni.

Kulingana na wadadisi, hatua ya kumteua Bw Kenneth kwenye baraza la mawaziri inalenga kumpa jukwaa la kujinadi kwa watu, ili kumfahamu kama kiongozi wao.

Wanasema kuwa kwa kufanya hivyo, haitakuwa vigumu kwa Rais Kenyatta na washirika wake “kumnadi” kwa wananchi, kwani watakuwa tayari washamfahamu.

“Kwa namna moja, lengo kuu la waandani na washauri wa karibu wa Rais Kenyatta ni kuhakikisha kuwa hawatarudia kosa la 2017, ambapo walianza kumfanyia kampeni Kenneth akiwa amechelewa sana. Hilo ndilo lililochangia yeye kushindwa na Bw Sonko kwenye ugombezi wa ugavana kwani alionekana kama ‘mgeni’,” asema Bw Charles Mulila, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wadadisi wanaeleza kuwa kwa kuwania ugavana wa Nairobi mnamo 2017, lengo kuu la mabwanyenye kutoka Mlima Kenya lilikuwa kumtumia Bw Kenneth “kulinda maslahi yao” jijini.

Hilo pia lingemweka kwenye nafasi sawa ya kujijenga kuwa mrithi wa Rais Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya.

“Mpango huo ungalipo, ila sasa lengo kuu la mabwanyenye hao ni kumjenga na kumtayarisha Kenneth kulinda maslahi yao kote nchini, kulingana na wadhifa anaotayarishwa kuwania ifikapo 2022,” asema Bw Mulira.

Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wanamtaja Bw Kenneth kuwa mwoga na limbukeni kisiasa, ambaye huenda akashindwa kuhimili mawimbi ya siasa ya baadhi ya viongozi kama vile Mwangi Kiunjuri, ambaye ametangaza mkakati wa kutwaa uongozi wa ukanda huo kutoka kwa Rais Kenyatta.