MakalaSiasa

JAMVI: Ni kushuka mchongoma kwa Kalonzo kuingia Ikuluu 2022 bila Raila

September 1st, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Kauli ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kwamba hatahitaji kuungwa mkono na kinara wa ODM, Raila Odinga, ili kushinda kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2022 linalenga kutuliza wandani wake ambao wamekuwa wakimtaka kugombea urais badala ya kuunga wanasiasa wengine.

Wandani wa Bw Musyoka wamekuwa wakimhimiza kutafuta mwelekeo wake wa kisiasa bila kumtegemea Bw Odinga ambaye wameshirikiana tangu uchaguzi mkuu wa 2013.

Wanahisi kuwa ushirikiano wake na Bw Odinga umemnyima nafasi ya kuunda muungano unaomwezesha kuwa serikalini ilivyofanyika baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 alipoungana na Mwai Kibaki.

Kwenye uchaguzi huo, Bw Musyoka aligombea urais na baada ya uchaguzi uliofuatiwa na ghasia, aliteuliwa makamu wa rais.

“Kuna hisia kwamba Bw Musyoka amekuwa akitupa nafasi ya kuwa serikalini kwa kushirikiana na Bw Odinga kwenye uchaguzi mara mbili. Wandani wake wanahisi kwamba wakati umefika wake kugombea urais au kushirikiana na wanasiasa wengine mbali na Bw Odinga ili kuimarisha nafasi ya kuwa serikalini,” asema mdadisi wa siasa za Ukambani David Kiilu.

Kulingana na aliyekuwa seneta wa Machakosa Johnson Muthama ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Musyoka, makamu huyo wa rais wa zamani anafaa kupanga mikakati yake ya kisiasa bila kutegemea Bw Odinga pekee.

“Bw Musyoka anaweza kuungana na viongozi wengine mbali na Bw Odinga. Anaweza kuungana na Mudavadi, Uhuru, Gedion Moi na viongozi wengine walio na malengo sawa na yake na huu ndio mwelekeo wa siasa za Kenya sasa na siku zijazo,” anasema Bw Muthama.

Wadadisi wanasema hisia za wandani wa Bw Musyoka ni kuwa nafasi ya Odinga kumuunga mkono kiongozi wao kugombea urais ni finyu sana.

“Kuna hisia miongoni mwa wafuasi wa Bw Musyoka kwamba Bw Odinga amemruka kiongozi huyo wa chama cha Wiper mara mbili. Kwao, Odinga amekuwa akimtumia Bw Musyoka tu wakati wa uchaguzi na kisha kumruka baadaye,” asema Bw Kiilu.

Mwishoni mwa wiki jana, Bw Musyoka alisema tayari ameanza kujitafutia uungwaji mkono wa Wakenya akijitayarisha vilivyo kwa kivumbi cha 2022, pasipo kumtegemea Bw Odinga kufaulu katika kinyang’anyiro hicho.

Bw Musyoka alisema aliweka kando azma yake ya kuwania urais mara mbili ili kumuunga mkono Bw Odinga, na kwamba sasa ni wakati wake kutwaa uongozi.

“Huwezi kuomba uongozi, uongozi hunyakuliwa,” alikariri makamu huyo wa Rais wa zamani.

Kulingana na mdadisi wa siasa Bw Nicholas Kyule, matamshi ya Bw Musyoka yanaonyesha kwamba amezinduka na kufahamu kwamba hatakuwa na nafasi ya kugombea urais akiungana tena Bw Odinga.

“Amebaini kwamba hakuna nafasi ya Bw Odinga kumuunga mkono baada ya kumruka mara mbili. Ni uamuzi ambao umechelewa na kumfanya kukosana na aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha Wiper Kivutha Kibwana ambaye alimshauri kujitegemea kisiasa na kuweka mikakati yake binafsi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022,” asema Bw Kyule.

Viongozi kadha wa eneo la Ukambani, wanataka makamu huyo wa Rais wa zamani kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu 2022 huku wadadisi wakisema ni kibarua iwapo hatajipanga vyema kisiasa.

Waliendelea kumshinikiza Bw Musyoka kuwa mstari wa mbele katika muungano wowote wa kisiasa utakaoundwa kuelekea uchaguzi mkuu 2022.

Aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama aliwashauri wanasiasa wanaosaka kura za Ukambani kuzungumza na Bw Musyoka kwanza.

Kulingana na Bw Kyule hakuna mwanasiasa anayeweza kushinda urais nchini kivyake bila kuungana na wanasaisa wengine.

“Siasa za Kenya zilibadilika 2002 wakati wanasiasa waliungana kushinda chama cha Kanu. Hakuna mwanasiasa anayeweza kushinda urais bila kuungana na wengine na Bw Musyoka anafahamu hilo,” asema Bw Kyule kauli ambayo Bw Muthama anakubaliana nayo.

“Viongozi wa maeneo mengine wanaotaka urais, wanafaa kuongea na Kalonzo kama mmoja wa vigogo wakuu wa kisiasa humu nchini ikiwa wanataka kura za eneo la Ukambani,” alisema.

Kulingana na afisa mmoja wa chama cha Wiper ambaye aliomba tusitaje jina lake, mipango inaendelea ya kubuni muungano mkubwa wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 ambao Bw Musyoka atatekeleza jukumu muhimu.

“Kwa kusema kuwa hatamhitaji Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Musyoka alimaanisha kuwa yuko tayari kupanua bawa zake za kisiasa. Alikuwa akiwajibu viongozi wa Ukambani ambao wamekuwa wakidai kwamba hawezi kujitegemea kisiasa bila Bw Odinga. Wanasahau kwamba alikuwa mgombea urais 2007 akishindana na wengine akiwemo Bw Odinga,” akasema afisa huyo.

Kulingana na wadadisi, tamko lolote la kisiasa wakati huu, halifai kuchukuliwa kama uamuzi wa mwisho kwa sababu wanasiasa ni vigeugeu na hawana uadui wa kudumu.

“Mawimbi ya siasa huwa yanabadilika haraka na ikizingatiwa kuwa kuna miaka mitatu kabla ya uchaguzi mkuu, kauli ya Bw Musyoka haifai kuchukuliwa kuwa ya mwisho. Anaweza kuwa katika muungano mpana wa kisiasa pamoja na Bw Odinga japo katika mazingira tofauti na ilivyokuwa 2017,” asema Bw Kyule.