MakalaSiasa

JAMVI: Njama ya Jubilee kubadili sheria za uchaguzi

June 23rd, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

HUKU mjadala kuhusu marekebisho ya Katiba kupitia kura ya maamuzi ukiendelea kushika kasi, chama cha Jubilee kimeanza mchakato wa kubadilisha tena sheria za uchaguzi zilizopitishwa kwa haraka siku chache kabla ya uchaguzi wa urais wa marudio mnamo Oktoba 26, 2017.

Wanasiasa wa Jubilee walikimbilia kubadili sheria za uchaguzi kama njia mojawapo ya kuzuia Mahakama ya Juu kubatilisha tena matokeo ya uchaguzi wa urais wa marudio.

Mahakama ya Juu ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8 baada ya kubaini kwamba uliendeshwa bila kuzingatia Katiba na sheria za uchaguzi.

Hii ilikuwa baada ya Jaji Mkuu David Maraga kutishia kwamba Mahakama ya Juu ingebatilisha tena matokeo endapo Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ingefeli kufuata katiba na sheria katika uchaguzi wa marudio.

Wabunge wa Jubilee walibadilisha sheria ili kuzuia Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo kutokana na kigezo cha IEBC kutozingatia sheria.

Kadhalika, Jubilee walibadili sheria ili kuruhusu naibu mwenyekiti wa IEBC kutangaza mshindi wa urais, tofauti na hapo awali ambapo mwenyekiti pekee ndiye aliyetwikwa jukumu hilo.

Huenda Jubilee walihofia kwamba mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati angejiuzulu hivyo kutatiza uchaguzi wa marudio.

Jubilee pia walisema kuwa si lazima kwa IEBC kupeperusha matokeo kwa njia ya kielektroniki tofauti na awali ambapo matokeo katika karatasi zinazobeba matokeo hayo yalifaa kuwa sawa na yale yanayopeperushwa kwa njia ya kielektroniki.

Sheria hizo zilipingwa vikali na upande wa Upinzani, ulioongozwa na aliyekuwa mwaniaji wa muungano wa NASA Raila Odinga, kutokana na kigezo kwamba zililenga kutoa mwanya kwa Jubilee kuiba kura.

Seneta wa Meru Mithika Linturi sasa anasema kuwa chama cha Jubilee kimeanza mchakato wa kubadili sheria za uchaguzi kwa lengo la kuzuia vurugu katika uchaguzi wa 2022.

Bw Linturi ambaye pia ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Sheria na Haki za Kibinadamu, anasema kuwa mabadiliko hayo yatahakikisha kuwa Wakenya hawapigani au kuharibu mali baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2022.

“Tunalenga kubadilisha sheria ili kuzuia uhasama wa kikabila wakati na baada ya uchaguzi. Tutahakikisha kuwa Kenya ina sheria zitakazozuia umwagikaji wa damu au uharibifu wa mali,” akasema Bw Linturi.

“Tunataka kila Mkenya kufahamu kuwa lengo la uchaguzi ni kushindana kwa sera na wala si uadui,” akaongezea.

Hata hivyo, kinara wa upinzani Bw Odinga amesalia kimya kuhusiana na mabadiliko ya sheria za uchaguzi licha ya kuzitaja kama sumu kwa demokrasia zilipopitishwa na wabunge wa Jubilee takriban miaka miwili iliyopita.

Kadhalika, haijulikani ikiwa Naibu wa Rais William Ruto ataunga mkono mabadiliko ya sheria za uchaguzi.

Dkt Ruto alipokuwa akihutubia wasomi katika taasisi ya Chatham jijini London, Uingereza, mapema mwaka huu alisema kuwa sheria za uchaguzi na tume ya IEBC hazifai kulaumiwa kwa machafuko ambayo hushuhudiwa nchini kila baada ya uchaguzi.

Dkt Ruto alisema machafuko hayo yanasababiswa na viongozi wanaokataa kukubali matokeo ya uchaguzi.

“Siasa za Kenya ni safi na wala tume ya IEBC au sheria zetu za uchaguzi hazina dosari. Shida ni wale wawaniaji wanaoingia kwenye kinyang’anyiro lakini hawako tayari kukubali matokeo,” akasema Dkt Ruto huku akionekana kumwelekezea kidole cha lawama Bw Odinga.

Tayari tume ya IEBC imependekeza kuwa Katiba ifanyiwe mabadiliko ili uchaguzi wa rais, wabunge na maseneta ufanyike tarehe tofauti na ule wa magavana na madiwani.

Katika ripoti yake tathmini ya uchaguzi wa 2017, IEBC ilisema ni vigumu kwa maafisa wake kushughulikia kura za viti sita kwa mpigo.

“Kuendesha uchaguzi wa nyadhifa sita kwa mpigo kunasababisha maafisa wetu kuchoka, hivyo kuandika matokeo yaliyosheheni makosa,” ikasema ripoti ya IEBC.