JAMVI: Nyachae alivyomtayarisha Matiang’i kuwa kiongozi wa jamii ya Abagusii

JAMVI: Nyachae alivyomtayarisha Matiang’i kuwa kiongozi wa jamii ya Abagusii

Na WANDERI KAMAU

IMEFICHUKA mwanasiasa mkongwe, Simeon Nyachae, alikuwa ashamtayarisha Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, kuwa mrithi wake kama kiongozi na msemaji wa jamii ya Abagusii baada ya kifo chake.

Duru zimeliambia ‘Jamvi la Siasa’ kwamba mikakati hiyo ilianza zaidi ya miaka miwili iliyopita, ingawa imekuwa ikiendeshwa kichinichini.Juhudi hizo zimekuwa zikijumuisha mikutano ya faragha iliyowashirikisha viongozi wenye ushawishi katika jamii hiyo kwenye serikali kuu na zile za kaunti.

Viongozi hao wanajumuisha magavana, maseneta, wabunge, makatibu wa wizara, wenyeviti wa mashirika ya serikali miongoni mwa wengine.

Dkt Matiang’i alithibitisha hayo alipoamka kuhutubu kwenye mazishi ya Mzee Nyachae, mnamo Jumatatu, aliporejelea kwa kina ukaribu aliokuwa nao na mwendazake.

“Tangu nilipoteuliwa kuhudumu kama waziri mnamo 2013, nimekuwa karibu sana na Mzee Nyachae. Tulikuwa tukifanya mikutano ya mara kwa mara kuhusu uongozi wa nchi. Alikuwa akinipa ushauri katika masuala mbalimbali kuhusu utumishi wa umma. Kinaya ni kuwa, kila alipohisi mawaziri wamekosea mahali fulani, mimi ndiye niliyebeba lawama kuu,” akasema Dkt Matiang’i.

Kwenye hotuba yake, alieleza walikosa tu kukutana naye mwaka uliopita, kutokana na hali yake ya kiafya.Kufuatia kauli hiyo, wadadisi wanasema ni wazi Mzee Nyachae alikuwa katika mstari wa mbele kwenye juhudi za “kumtayarisha Dkt Matiang’i kama mrithi wake, licha ya hali yake mbaya kiafya.”

“Inaonekana kwamba kwa juhudi hizo, Mzee Nyachae alifahamu muda wake ulikuwa ukikaribia kukamilika na palikuwa na haja ya kumtawaza mrithi wake. Hilo ndilo lililokuwa lengo fiche la mikutano hiyo,” asema Bw Kiprotich Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Wadadisi wanaeleza kuna uwezekano Rais Uhuru Kenyatta pia alishauriana na Mzee Nyachae kuhusu hatua ya kumkweza Matiang’i, ikizingatiwa marehemu alikuwa na ukaribu mkubwa na familia za Mzee Jomo Kenyatta na Daniel Moi tangu miaka ya sitini, alipoanza kuhudumu kama afisa wa utawala wa mikoa.

Wanasema ukaribu wa Mzee Nyachae na Mzee Kenyatta uliongezeka pakubwa alipohudumu kama Mkuu wa Mkoa wa Kati kati ya 1965 na 1979.

Vivyo hivyo, ukaribu wake na Mzee Moi ulikua alipohudumu kama waziri katika wizara kadhaa na kama Mkuu wa Utumishi wa Umma.

“Kimsingi, Rais Kenyatta alikuwa na ukaribu wa kipekee na Mzee Nyachae, kwani alikuwa rafikiye babake, Mzee Kenyatta, kabla ya kifo chake mnamo 1978. Hilo linaonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa Rais Kenyatta aliamini ‘baraka’ ambazo Mzee Nyachae alimkubalia Dkt Matiang’i kuwa mrithi wake kama msemaji wa Abagusii,” asema Dkt Godfrey Bosire, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kando na kuibuka kuwa miongoni mwa washirika wakuu wa karibu wa Rais Kenyatta, tayari juhudi zimeanza “kumtengenezea mapito,” Dkt Matiang’i katika eneo hilo.Imeibuka kuna mikakati ya kichinichini kuwarai wabunge wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto katika eneo hilo kuvuka kambi ya Dkt Matiang’i kama “mmoja wao.”

Tayari, juhudi hizo zinaonekana kuanza kuzaa matunda, baada ya wabunge watatu kuhama kambi ya Dkt Ruto mapema wiki hii na kutangaza kumuunga mkono Dkt Matiang’i, ikiwa ataidhinishwa kuwania urais 2022.Kwenye mazishi Jumatano katika Kaunti ya Nyamira, wabunge Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini), Shadrack Mose (Kitutu Masaba) na Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi) walisema wako tayari kumuunga mkono “ndugu yao” ikiwa atatangaza azma ya kuwania urais.

“Ningetaka kumhakikishia Dkt Matiang’i kwamba tunamuunga mkono kikamilifu. Asidanganywe na yeyote kuwa sisi ni maadui wake. Hatuna sababu ya kumpiga vita. Hatuwezi kwenda kinyume na matakwa ya watu wetu,” akasema Bw Nyamoko.

Wadadisi wanasema mwelekeo huo ni pigo kuu kwa Dkt Ruto, ikizingatiwa alikuwa amefanikiwa kujizolea uungwaji mkono kutoka kwa wabunge kadhaa.Wakati wa mazishi ya Mzee Nyachae, Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi na mbunge Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini), ambao ni washirika wa Dkt Ruto, walikamatwa katika hali tatanishi.

Licha ya masaibu waliyopitia, wawili hao hawajatangaza ikiwa watamuunga mkono Dkt Matiang’i au la.Hali hiyo pia inatajwa kumwacha Bw Charles Nyachae, kwenye njiapanda kisiasa, ikizingatiwa ni mwanawe Mzee Nyachae.

Bw Nyachae alihudumu kama mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Utekelezaji Katiba (CIC) na amekuwa miongoni viongozi wachache eneo hilo waliobaki katika kambi ya Dkt Ruto.V

iongozi ambao wanaunga mkono juhudi za kumkweza Dkt Matiang’i kama kiongozi wa Abagusii wanamtaja kuwa mtu “anayefaa zaidi kurejesha umoja na mwelekeo sawa wa kisiasa” katika jamii hiyo.Wanasema watabaki kuwa wapweke kisiasa, ikizingatiwa maeneo mengine nchini yana viongozi wao yanaowaangalia.

Wanatoa mfano wa Rais Kenyatta (Mlima Kenya), Raila Odinga (Luo Nyanza), Kalonzo Musyoka (Ukambani), Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula (Magharibi) kati ya wengine kama ishara ya wazi hata wao wanamhitaji kiongozi atakayewawakilisha kitaifa.

Hata hivyo, Bw Osoro anakosoa juhudi hizo, akizitaja kama “kuirejesha Kenya katika enzi ya siasa za ukabila.”“Hatutakubali Wakenya kurudishwa kwa siasa za ukabila. Tunataka uwepo wa siasa zitakazowaunganisha Wakenya wote badala ya kuwagawanya,” akasema.

You can share this post!

Mudavadi sasa akimbilia baraka za wazee kabla ya Muhkisa...

Ghasia katika kampeni za UDA