MakalaSiasa

JAMVI: 'Nyumba ya Jubilee itaporomoka kabla ya 2022'

March 10th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Matukio ya hivi punde katika uga wa siasa nchini yanaashiria kwamba huenda chama tawala cha Jubilee kikaporomoka kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Wadadisi wanataja misimamo tofauti ya viongozi wa chama hicho kuhusu vita dhidi ya ufisadi, muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na miito ya kura ya maamuzi kama masuala yanayoweza kuharakisha kusambaratika kwa chama hicho.

Wengi wanahisi kwamba viongozi wa chama cha Jubilee Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Wake William Ruto wametofautiana vikali kuhusu masuala hayo matatu jambo linaloonyesha mpasuko katika chama hicho unaendelea kupanuka.

Kulingana na mwanauchumi maarufu Dkt David Ndii ambaye alikuwa mwanamikakati wa Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, ni dhahiri kwamba Jubilee hakiwezi kudumu hadi uchaguzi mkuu ujao.

“Jubilee kilibuniwa kwa sababu ya kesi zilizowakabili viongozi wake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ambazo kwa sasa haziko. Hakuna cha kuwaunganisha,” Bw Ndii alisema akihojiwa na runinga moja ya humu nchini Jumatano usiku.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2013, Rais Kenyatta na Bw Ruto waliendesha kampeni yao wakitumia kesi zilizowakabili ICC kurai jamii zao kuwachagua.

Bw Ndii alisema kuna hisia kwamba Bw Ruto ni hatari kuwa rais wa Kenya na hivyo kuna juhudi za kumzuia ili asimrithi Rais Kenyatta jambo ambalo litavunja Jubilee.

Mwishoni mwa mwaka jana, aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama hicho David Murathe, mwandani wa Rais Kenyatta alitangaza wazi kwamba atahakikisha Bw Ruto hataingia Ikulu.

Rais Kenyatta alijitenga na kauli ya Bw Murathe akisema wakati wa siasa ulipita.

Wadadisi wanasema msimamo wa Bw Ruto na wandani wake kwamba vita dhidi ya ufisadi vimeingizwa siasa ni dhihirisho kwamba nyumba ya Jubilee iko njia panda.

“Hatua ya Bw Ruto ya kulaumu asasi ambazo Rais Kenyatta anasema ana imani nazo katika vita dhidi ya ufisadi na matamshi ya wandani wake kwamba ni jamii moja inayolengwa yanaonyesha nyumba ambayo imegawanyika,” asema Bw Joram Kasumbi mtaalamu wa masuala ya kisiasa.

Katika muda wa wiki moja, Bw Ruto amekuwa akilaumu Idara ya Upelelezi wa Jinai kwa kudai kwamba Sh21 bilioni zilizolipwa kwa ujenzi wa mabwawa mawili Elgeyo Marakwet zilipotea.

Hata hivyo, Rais Kenyatta anasisitiza kuwa idara hiyo inafaa kupatiwa nafasi kufanya kazi yake akisema ana imani nayo.

Ingawa Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa muafaka wake na Bw Odinga ulilenga kuunganisha nchi iliyogawanyika baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Ruto amekuwa akimlaumu kiongozi wa chama cha ODM kwa kuvuruga chama cha Jubilee. Mara kwa mara, amekuwa akimlaumu Bw Odinga kwa kutaka kuvunja chama hicho tawala na kuapa kwamba hatakubali kutimuliwa katika serikali aliyokuwa msitari wa mbele kuunda.

Kulingana na mdadisi wa siasa Bw Ocheing Kadundi, kuporomoka kwa Jubilee kunatokana na muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga. “Muafaka ulitikisa nyumba ya Jubilee ambayo haikuwa na msingi imara na sasa kuporomoka kwake hakuepukiki,” alisema Bw Kadundi.

Kulingana na Bw Kasumbi, nafasi ya salamu zilizotumiwa kama alama ya Jubilee 2017 ilichukuliwa na salamu za Rais Kenyatta na Bw Odinga 2018.

“Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mwisho wa ndoa ya Jubilee,” asema.

Wadadisi wanakubaliana kwamba kilichowaleta pamoja viongozi wa Jubilee ni kesi zilizowakabili pekee.

“Rais Kenyatta sasa hamhitaji Bw Ruto alivyokuwa akimhitaji walipougana 2013 kubuni muungano wa Jubilee na walipovunja vyama vyao kuunda chama c?ha Jubilee,” aeleza.

Bw Kasumbi asema viongozi wa Jubilee wametofautiana kama ardhi na mbingu kuhusu suala la marekebisho ya katiba. “Ingawa Rais Kenyatta hajazungumzia hadharani miito ya kubadilisha katiba, wandani wake wanayaunga mkono ilhali Bw Ruto na wandani wake wanayapinga. Katika hali kama hii, Jubilee haiwezi kudumu,” aeleza.

Hisia za Bw Ruto na washirika wake ni kwamba marekebisho ya kikatiba yanalenga kumzuia asishinde au asigombee urais ilhali wale wanaomuunga Rais Kenyatta wanasema yatahakikisha Wakenya wataishi kwa amani.

“Rais Kenyatta hajazungumzia miito ya kurekebisha katiba hadharani, mshirika wake katika handisheki, Bw Odinga, hasimu mkuu wa Bw Ruto, anasisitiza ni lazima yafanyike. Ukimsikiliza kwa makini Rais Kenyatta kwenye baadhi ya hotuba zake, utapata dokezo kuhusu msimamo wake kwa vile amekuwa akisizitiza siku za mshindi wa uchaguzi kutwaa mamlaka yote zimepita,” alisema.

Kulingana na Bw Kadundi, Jubilee haiwezi kudumu katika mazingira ya kisiasa yaliyopo nchini kwa wakati huu.

Mdadisi wa siasa Profesa Makau Mutua anasema kusambaratika kwa jubilee sio suala la ikiwa kutatokea.

“Uhuru Kenyatta hana haja na Jubilee kwa sababu anahudumu kipindi cha mwisho na ndio maana itaporomoka na Bw Ruto hataweza kuiokoa,” alisema Profesa Mutua.