Makala

JAMVI: Raila alivyocheza reggae huku Uhuru akimtazama

November 22nd, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga, alionekana kuwa msitari wa mbele zaidi kushinikiza juhudi za kurekebisha katiba kuliko mshirika wake katika mchakato huo Rais Uhuru Kenyatta.

Ingawa wakati wa hafla za kitaifa kiongozi wa nchi alielezea nia yake ya kutaka katiba irekebishwe kupitia mpango wa maridhiano, ni Bw Odinga ambaye amekuwa akitetea mchakato huo zaidi tangu ulipoasisiwa na kabla ya kusitishwa Alhamisi.

Tangu viongozi hao walipozindua ripoti ya jopokazi la maridhiano wiki tatu zilizopita, Bw Odinga amechukua msimamo ambao umekosolewa vikali na makundi mbalimbali kwa kupuuza maoni na malalamishi yao.

Wadadisi wa kisiasa wanasema msimamo wa Bw Odinga unamfanya aonekane kama ndiye pekee anayesukuma marekebisho ya katiba yaliyopendekezwa katika BBI.

“Mbinu anayotumia ni tofauti na anayotumia Rais Kenyatta. Kwa hakika, inamfanya aonekane kuwa ndiye anayekataa maoni ya makundi na watu wanaolalamika kuhusu mapendekezo ya ripoti hiyo,” asema mbunge mmoja wa chama cha Jubilee ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa sababu ya ukuruba wake na vinara hao wawili.

Alisema Bw Odinga anatumia mbinu ya kugawanya makundi ya wanaolalamika tofauti na Rais Kenyatta ambaye amekuwa akisisitiza kuna haja ya kuwa na muafaka ili kuepusha refarenda yenye ubishi.

Anatoa mfano wa hatua yake ya kukutana na magavana wa sehemu mbalimbali baada ya kushindwa kuwashawishi magavana wote alipokutana nao na kupuuza ushauri wa viongozi.

“Tangu ripoti ilipozinduliwa, hatujamuona Rais Kenyatta na washirika wake wa karibu kisiasa wakiwa msitari wa mbele kuichangamkia japo wanasema wanaiunga. Ni Bw Odinga na wandani wake ambao wamekuwa msitari wa mbele kupinga wanaotaka ifanyiwe mabadiliko. Ni Bw Odinga ambaye amekuwa akikutana na kujibu wanaolalamika au kutoa matakwa yao kabla ya kuiunga. Msimamo wake umekuwa ni mmoja tu; kwamba ripoti haitabadilishwa,” asema mdadisi wa siasa Paul Katana.

“Je, ameachiwa mchakato huo? Na ikiwa ni kweli, kwa nini? Mbona washirika wa Rais Kenyatta wameonekana kurudi nyuma ilipozinduliwa? Je, wanafahamu kitu ambacho Bw Odinga na watu wake hawafahamu?” ahoji BwPeter Katana.

Japo Rais Kenyatta ana kazi nyingi kuweza kuhusika na mchakato huu kila wakati, wadadisi wanasema kuwa angekuwa anawakilishwa na washirika wake wa karibu wa kisiasa kutoka Mlima Kenya katika mikutano ambayo Bw Odinga amekuwa akikutana na makundi mbalimbali ili kiongozi huyo wa ODM asionekane kusukuma mchakato huo peke yake.

Alipokutana na magavana wa eneo la magharibi, Bw Odinga alikuwa ameandamana na mawaziri.

Bw Katana anasema kuwa kufikia sasa, Bw Odinga amepata pigo baada ya makundi mbalimbali kusisitiza kuwa BBI inafaa kusimamishwa hadi maoni na malalamishi ya Wakenya wote yazingatiwe.

“Lakini Bw Odinga amekataa ngumu huku Rais Kenyatta akinyamaza. Hii bila shaka inamuacha katika hali ya upweke,” asema. Viongozi hao wawili wamekuwa wakikutana na makundi mbalimbali katika juhudi za kuwarai kuunga na kuupigia debe mswada wa kura ya maamuzi.

Wiki hii walikutana na viongozi wanawake kabla ya hafla ya kuzindua ukusanyaji wa sahihi za kuunga mswada huo kufutiliwa mbali. Hii ni licha ya kuwa Bw Odinga alikuwa ametangaza kuwa angezindua shughuli hiyo Alhamisi akiwa na Rais Kenyatta akisema hakuna wakati wa kupoteza katika kukamilisha mchakato huo.

“Ni muhimu kuzingatia kwamba Rais Kenyatta hakuwa ametangaza hafla hiyo wala washirika wake wa kisiasa hawakuwa wameizungumzia,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

“Inaonekana ni kama Bw Odinga anacheza reggae peke yake. Hii ni kwa sababu anahisi kwamba mabadiliko yanayokusudiwa yatamfaidi kisiasa na hasa katika azima yake ya kugombea urais kwa mara ya tano kwenye uchaguzi mkuu wa 2022,” asema Bw Kamwanah.

Wadadisi wanasema kwamba matukio ya tangu ripoti ilipozinduliwa na kufutwa kwa mkutano wa Alhamisi ni ishara kuwa huenda Bw Odinga anatumia mchakato huo kutimiza malengo ya kibinafsi na ndio sababu anaonekana msitari wa mbele.

“Bw Odinga ana malengo yake binafsi mbali na anayokusudia Rais Kenyatta ya kuunganisha Wakenya. Kumbuka kuwa Rais Kenyatta anajiandaa kustaafu 2022. Hii ndio sababu Bw Odinga na Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakishambuliana vikali kuhusu mchakato huo,” asema Bw Kamwanah.