Siasa

JAMVI: Raila, Kalonzo kwapani mwa Uhuru, hawasemi

August 2nd, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta amewaleta karibu kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka na kuwafanya mateka wa kisiasa ili wamsaidie kutimiza malengo yake ikiwa ni pamoja na kuendeleza ngome ya Mlima Kenya.

Kwa kuwavuta upande wake, aliwafanya waache ajenda na malengo ya Muungano wa NASA kwa kutumia Mchakato wa Maridhiano (BBI) kama chambo.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba tangu handisheki yake na Bw Odinga, Rais Kenyatta aliwaweka wawili hawa makwapani nao wakadhani alikuwa na nia njema ilhali alinuia kuwatumia.

“Handisheki na BBI ziliwafanya viongozi wa upinzani kuwa mateka wa Rais Kenyatta. Wanaunga ajenda zake zinazolenga kunufaisha ngome yake wakisubiri katiba ibadilishwe ili washirikishwe serikalini kwa kile ambacho kinadaiwa kuwa kuunganisha Wakenya,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Anasema kufikia sasa, Rais Kenyatta hajaonyesha kujitolea kwa dhati kuonesha kwamba anakumbatia BBI hasa baada ya wandani wake kuanza kuitumia kutisha ODM.

“Ulimsikia kiranja wa wengi katika seneti Bw Irungu Kang’ata akiambia ODM kwamba isipounga ajenda za serikali, hawatapigia debe BBI na kutaja mchakato huo kama mtoto wa ODM. Hii inamaanisha upande wa serikali una njama fiche japo Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa ni mpango wa kuunganisha Wakenya,” asema Bw Kamwanah.

Wiki jana, Bw Kang’ata alinukuliwa akisema kwamba Jubilee haitapigia debe BBI iwapo maseneta wa ODM hawataunga mfumo wa kugawa pesa za kaunti ambao unalenga kunufaisha kaunti za ngome ya Rais Kenyatta na kupokonya pesa baadhi ya ngome za Bw Odinga na Bw Musyoka.

“Kwa sababu Odinga na Musyoka ni mateka wa Rais Kenyatta waliunga mfumo huo. Usisahau kwamba walifanya hivyo kwa sababu wanataka kulinda BBI,” asema.

Kabla ya handisheki, wawili hawa walikuwa wakiongoza muungano wa NASA kukosoa serikali kwa kubagua ngome zao katika uteuzi serikalini na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hata hivyo, Rais Kenyatta alipowaweka makwapani, walinyamaza licha ya nyadhifa kuu serikalini kukabidhiwa watu kutoka maeneo ya Rais.

“Walifungwa minyororo ya utumwa Odinga alipovutwa karibu kupitia handisheki na kuonjeshwa vinono kwa kupewa kazi katika Muungano wa Afrika naye Musyoka akateuliwa balozi wa amani Sudan Kusini. Hata wakiona serikali ikitendea watu wao maovu hawasemi chochote. Ngome zao zinarushiwa makombo kuwafumba macho huku zile za Rais zikinufaika.

Kwa mfano, kuna hospitali mbili za Level Six eneo la Mlima Kenya katika kipindi cha miaka mitatu. Kuna miradi ya barabara ya zaidi ya Sh500 bilioni eneo hilo ilhali serikali imeshindwa kukamilisha miradi iliyoanzisha Magharibi ya Kenya na Ukambani ambazo ni ngome za Odinga na Musyoka na hawawezi kusema chochote,” asema mdadisi wa siasa, Derick Onyango.

Mdadisi huyu anasema kwamba wawili hawa watajilaumu wenyewe kwa kusahau muungano wa NASA ambao uliwapa zaidi ya kura milioni saba ili wawe watumwa wa Rais Kenyatta.

“BBI iliundwa kuvutia viongozi wa upinzani ambao walikuwa kwenye baridi ya kisiasa kwa miaka mingi na kutuliza wafuasi wao. Wanamikakati wa Rais waliitumia kutuliza hali, kuua upinzani ili waweze kufurahia minofu kimyakimya. Handisheki ilifumba Odinga mdomo akawa mwanasiasa bubu. Musyoka alijitangaza kuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta na kujipeleka utumwani akidhani BBI itamfaidi 2022. Ameamua kukaza minyororo ya utumwa kwa kuungana na Jubilee,” asema Onyango.

Aliyekuwa mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando anasema kwamba BBI haitafaulu na kwamba ODM inajitahidi kukata minyororo ya utumwa ambayo Odinga alifungwa na Uhuru.

“Inasikitisha kuwa BBI itafeli. Si vizuri. Rais anashughulikia janga la corona na ufisadi,” asema. Hata hivyo, anakiri kwamba Rais amezungukwa na watu wanaojifanya wazuri lakini ni maadui.

Wakili mmoja ambaye aliomba tusitaje jina lake anadai kwamba handisheki na BBI ulikuwa mpango wa shirika la ujasusi nchini wa kumweka Odinga makwapani ili kutuliza wafuasi wake ndipo rais aweze kumaliza kipindi chake cha pili kwa amani.

“Uhuru aliweka imani kwa NIS na haikumvunja moyo. Ninaamini hata kama aligeuza Odinga na Musyoka kuwa watumwa, alikuwa na nia njema katika handisheki lakini wandani wake wameiteka nyara,” asema wakili huyo.

Wabunge wa ODM na Wiper wamekuwa wakiunga mkono ajenda za serikali bungeni hata kama zinakandamiza wafuasi wao kwa baraka za Odinga na Musyoka. Vyama hivyo vina idadi kubwa ya wabunge baada ya Jubilee.