MakalaSiasa

JAMVI: Rais katika njia panda kuhusu kura ya maamuzi

June 16th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta yuko katika njia-panda kuhusu kura ya maamuzi ya marekebisho ya katiba huku mirengo miwili mikuu ya kisiasa nchini ikimweka pembeni kwa masharti.

Huku Rais akishikilia kuwa handisheki yake na Raila Odinga kuleta uthabiti wa utawala wake katika awamu hii ya pili, na akijaribu kutunza uthabiti ndani ya serikali yake katika mkataba wa maelewano na mrengo wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, siasa za referenda zinaonekana kumzubaisha katika mataa ya kisiasa

Shida kuu ni kwamba, mirengo hii miwili inalumbana vikali ikihujumiana waziwazi, Rais naye akionekana kutokuwa na mustakabali wa kuendeleza chama chake cha Jubilee katika siasa za urithi za 2022, hivyo basi kuzua hali ya kuchanganyikiwa katika ngome za Jubilee.

Tena Rais akionekana kulenga kuondoka afisini 2022 akiwa na nembo ya kuunganisha Wakenya, suala hili la referenda halijapata uwiano wa hasa nini kinafaa kibadilishwa, mrengo wa Odinga ukipendekeza kupanuliwa kwa vyeo vya kugawana, Ruto akipinga kuundwa kwa vyeo, makundi ya kijamii yakiwa na mapendekezo chungu nzima…. hivyo basi kuweka Rais katika njia panda ya uhakika.

Hali ni mbaya kwake kiasi kwamba ufichuzi wa serikali wa Taifa Leo unaonyesha kuwa idara ya ujasusi nchini (NIS) imempa tahadhari kuwa siasa za sasa ambazo zinaendelezwa huku jina lake liking’ang’aniwa kutumiwa kama idhini ya urithi wa 2022, ni hatari kwa msingi wa amani.

Tayari, wandani wa Raila Odinga ambao hujumuika katika handisheki wakiongozwa na mbunge wa Ruaraka, Tom Kajwang’ wamesema kuwa “mpende msipende tunaelekea kwa kura ya maamuzi na tuna idadi tosha ya wapiga-kura kupitisha maazimio yetu.”

Akiongea majuzi, Kajwang’ alisema kuwa “wafuasi wa Ruto na mrengo wake wa Tangatanga waelewe kuwa Rais Uhuru na Kinara wetu, Raila ndio walio na ufuasi mwingi wa kisiasa hapa nchini. Wakiunganisha wafuasi wao pamoja, tutapitisha malengo yetu ya mabadiliko ya katiba.”

Hata hivyo, Spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi alisema kuwa “kuna wanasiasa waneoneza ndoto kuwa ni rahisi kwa sasa kuandaa kura hiyo.”

Akasema, “Ninataka kuwapa onyo kuwa hata Rais Kenyatta anajua kuwa kwa sasa hatuna sheria za kuongoza kura hiyo na haijulikani kama sheria hizo zinaweza kuwa maarufu katika ukumbi wa mabunge yote nchini kuandaa sheria hizo.”

Bw Muturi alisema kuwa kwa sasa “migawanyiko iliyoko katika siasa za Kenya inatia wasiwasi kuhusu maandalizi ya kura hiyo kwa kuwa ni lazima kwanza yakumbatiwe kwa umoja na nusu ya mabunge yote ya kaunti na pia yale ya seneti na bunge la kitaifa.”

Mabunge hayo kwa sasa yamegawanyika katika mirengo ya Kieleweke, Handisheki, Tangatanga na walio na imani kwa vyama vingine vya kisiasa hivyo basi kuzua mng’ang’ano mkuu.

Tayari, Dk Ruto amesema kuwa hataunga mkono mito ya kubadilisha katiba ikiwa nia kuu itakuwa ni kuunda vyeo vya kugawana mamlaka ya serikali.

Amesema kuwa Kenya ya sasa ni lazima ikombolewe kutoka kwa siasa za wachache kusaka makuu ya kugawana keki ya kitaifa hadi ziwe kuhusu manufaa ya Wakenya wote kwa ujumla.

“Wengi husema kuwa siko tayari kuungana na Wakenya katika kutekeleza kura ya maamuzi ili tubadilishe katiba eti tupanue nyadhifa za ugavi mamlaka. Huo si uongo, siwezi nikaunga mkono kura ya maamuzi ambayo itaandaliwa kwa msingi huo,” akasema.

DP Ruto akionekana kumlenga Bw Odinga, alisema kuwa “hizi siasa za eti ni lazima mtu fulani afurahishwe ndio kuwe na amani, ni lazima mtu huyu akianguka kura ahifadhiwe katika wadhifa au yule ndio atuhakikishie amani ni lazima agaiwe kipande cha serikali ni kiini cha ghasia za baada ya uchaguzi.”

Dkt Ruto alisema kuwa ataunga kura ya maamuzi ambayo nia yake ni kuleta usawa wa ugavi wa raslimali, uthabiti wa gharama ya mishahara na pia usawa wa kijinsia katika ugavi wa mamlaka.