MakalaSiasa

JAMVI: Rais Kenyatta anavyopotoshwa na washauri wake

June 2nd, 2019 3 min read

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kunyamazia baadhi ya changamoto zinazowakumba Wakenya na kukurupuka kuchukua hatua baada ya vilio vyao imeibua hofu ya ikiwa huenda anapotoshwa na washauri wake kuhusu hali ilivyo nchini.

Hilo linajiri baada ya Rais kugutukia kilio cha wafanyabiashara wengi nchini, hasa jijini Nairobi, kuhusu kuzuiliwa kwa makasha yao katika eneo kukagulia makasha la Embakasi.

Wafanyabiashara katika sehemu zingine nchini wamekuwa wakilalamika kuhusu sheria kali za kuingiza na kusafirisha bidhaa zao katika nchi za nje, hali ambayo wadadisi wanaitaja kama dalili za pengo la kimawasiliano kati ya Rais Kenyatta na washauri wake wakuu.

“Mtindo wa rais kuzindukia baadhi ya matatizo yanayowaandama Wakenya, hasa wafanyabiashara unaashiria wazi ukosefu wa mawasiliamo mazuri kati yake na wale wanaomshauri kuhusu masuala hayo,” asema Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya siasa.

Masuala mengine yanayozua hofu ni kutosuluhishwa kwa changamoto zinazowakumba wakulima, hasa katika sehemu ya Mlima Kenya.

Wakulima wa majanichai na kahawa katika ukanda huo wametishia kuanza kung’oa mazao hayo, wakilalamikia kutotekelezwa kwa ripoti mbalimbali ambazo ziliandikwa kuhusu mikakati ya ufufuzi wake.

Vilevile, wakulima wa zao la miraa katika kaunti za Meru na Embu wanalalamikia kutotekelezwa kwa ripoti ya jopokazi lililobuniwa na Rais kubaini mikakati ya ufufuzi wa zao hilo.

Wakiongozwa na Seneta Mithika Linturi wa Kaunti ya Meru, viongozi mbalimbali wamejitokeza kulalamika kwamba wakulima hawajaona matokeo ya ruzuku ya Sh1 bilioni ambazo Rais Kenyatta alitangaza kutolewa ili kutekeleza ulainishaji wa sekta hiyo.

“Hatumlaumu Rais, lakini tungetaka kuona matokeo ya ahadi alizotoa kwa wakulima. Je, Sh1 bilioni ambazo zilitolewa zilitumika vipi?” akashangaa seneta huyo.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, pia anaitaka serikali kuelezea kuhusu pale mikakati ya ufufuzi wa sekta ya kahawa ilipofikia.

Mbunge huyo anadai kuwa sekta hiyo imeendelea kudorora, licha ya baadhi ya serikali za kaunti, kama Kirinyaga kutangaza kuwa zimepata soko lake nchini Amerika.

“Kuna mikakati mingi ambayo imekuwa ikitangazwa kuhusu ufufuzi wa sekta ya kahawa, lakini wakulima wake bado wanateseka,” asema Bw Kuria.

Sheria na maagizo mengine ya serikali ambayo yanakosolewa ni ile kuhusu vipuri vya magari. Awali, serikali ilikuwa imetangaza kuwa vipuri hivyo havitakuwa vikiingizwa nchini, lakini ikageuka, Halmashauri ya Ukaguzi wa Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS) iliposema kuwa si vipuri vyote vitakavyozuiwa.

Kwa hayo, wachanganuzi wanasema kuwa imefikia wakati Rais aonyeshe msimamo kuhusu masuala mbalimbali yanayowakumba Wakenya, kwani huenda akapoteza uungwaji mkono wa kisiasa.

Kulingana na Kiprotich Mutai, ambaye ni mchangnuzi wa kisiasa, Rais hapaswi kungoja hadi pale anapofikiwa na kilio cha wananchi, ili kuchukua hatua.

“Mfano mzuri wa rais kuchelewa ni kuhusu utata unaozunguka kuzuiliwa kwa baadhi ya makasha katika eneo la Embakasi. Ingawa wafanyabiashara wengi walielezea kuridhika kwao, baadhi walinung’unika kuwa alichelewa sana,” asema Bw Mutai.

Kulingana naye, hatua ya Rais kutoandamana na Waziri wa Viwanda na Biashara Peter Munya vilevile kunaashiria pengo kubwa la kimawasiliano kati yake na mawaziri husika. Badala yake, aliandamana na Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i na Katibu wa Wizara Karanja Kibicho.

Mchanganuzi huyo anasema kuwa hilo pia lilidhihirishwa na mkwaruzano kati yake na Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, ambapo alimkemea hadharani mara mbili kuhusiana na sakata ya mahindi, ambapo inaaminika kuwa karibu Sh2 bilioni ziliporwa.

“Kuna pengo kubwa la kiutendakazi, kati ya Rais na washauri na mawaziri wake. Baadhi ya hasira anazoonyesha hadharani na kuwakemea ni ishara ya ukosefu wa mshikamamo ufaao, hali ambayo bila shaka inaonyesha kuwa hawaamini au hawamwarifu kuhusu yanayoendelea katika wizara wanazosimamia,” asema Bw Muta.

Wachanganuzi pia wanataja tukio la Namimbia mnamo Machi, ambapo Rais Kenyatta aliwakashifu mawaziri wake hadharani, wakiwemo Kiunjuri, Munya na Dkt Monicah Juma (Mashauri ya Kigeni).

Wanasema kuwa hilo ndilo lilikuwa dalili ya wazi zaidi kuhusu pengo la kiutendakazi lililopo kati ya rais mawaziri na washauri wake.

Dalili nyingine inayotajwa ni kumpa mamlaka na kuonekana kumpendekea Dkt Matiang’i ikilinganishwa na mawaziri wengine.

Wachanganuzi wanasema kuwa huenda hilo likazua taswira ya ulegevu miongoni mwa baadhi ya mawaziri.

“Kwa kawaida, hatungekuwa tukimwoma Dkt Matiang’i akishughulikia baadhi ya masuala ambayo hayahusiani na wizara yake. Hiyo ni ishara kuwa anaaminiwa zaidi na Rais kuliko wenzake,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wachanganuzi wanasema kuwa ni kinaya kwa rais kuonekana kukurupukia baadhi ya masuala yanayowasumbua wananchi, ilhali kando na mawaziri wake, ana washauri wakuu katika kila idara muhimu ya utawala wake.

“Ilivyo, ni dhahiri kuwa washauri hao wanatekeleza majukumu yao kawaida, lakini huenda ikawa vigumu kwao kumfikia Rais moja kwa moja kwani huenda kukawa na watu fulani anaoonekana kuwaamini zaidi,” asema Prof Ngugi.

Hata hivyo, anaonya kuhusu mtindo huo, akisema kuwa unaionyesha serikali yake kama dhaifu na isiyofuatilia kwa kina yanayoendelea katika sekta muhimu za kiuchumi.