Makala

JAMVI: Refarenda: Mpango fiche wa jamii kubwa nchini kunufaika

November 22nd, 2020 3 min read

Na WANDERI KAMAU

IMEIBUKA kwamba lengo kuu la kura ya maamuzi iliyopangiwa kufanyika mapema mwaka 2021, ni mkakati wa jamii tano kubwa nchini kusuluhisha ushindani wa kisiasa ambao umekuwepo kati yazo tangu 1992.

Jamii hizo ni Wakikuyu, Waluhya, Waluo, Wakamba na Wakalenjin.

Kulingana na wadadisi wa siasa, huo ndio mpango uliopo kwenye ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), hasa kwenye pendekezo lake kuhusu kubuniwa kwa nafasi tano kubwa za kisiasa kwenye Serikali ya Kitaifa.

Kando na Rais na Naibu Rais, ripoti inapendekeza kubuniwa kwa nyadhifa tatu zaidi; za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili.

Wadadisi wanaeleza hiyo ndiyo sababu kuu ambapo Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, wameweka kila juhudi kuhakikisha Wakenya wameipitisha ripoti hiyo kabla ya mwaka 2022.

“Lengo fiche la BBI ni kukosoa makosa ya refarenda zilizofanyika 2005 na 2010. Sababu kuu ni kuwa zilikosa kutambua kwamba tatizo ambalo limekuwa likiiandama nchi ni ushindani wa kisiasa kati ya jamii hizo kuu tano tangu mwanzo wa vyama vingi vya kisiasa mnamo 1992,” asema Prof Peter Kagwanja, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Licha ya juhudi za viongozi hao wawili, Naibu Rais Wiliam Ruto na washirika wake wamejitokeza wazi kupinga jinsi mpango wa kuipigia debe BBI unavyoendeshwa, wakidai “umetekwa” na kuonekana kumilikiwa na Bw Odinga na washirika wake katika ODM.

Baadhi ya makanisa, likiwemo Kanisa Katoliki pia yamejitokeza kushinikiza mpango huo kuwashirikisha Wakenya wote.

Mnamo Jumatano, mpango wa kukusanya saini kuhusu ripoti hiyo kutoka kwa wananchi uliahirishwa ghafla katika hali tatanishi. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wenyeviti wanaosimamia mchakato huo, Bw Dennis Waweru na mbunge Junet Mohamed (Suna Mashariki) “lengo la uamuzi wao ni kutoa nafasi kwa Bunge la Kitaifa kumaliza kuandaa Mswada kuhusu Kura ya Maamuzi.”

Hata hivyo, ripoti zinadai kuahirishwa kwa mchakato huo kulitokana na mkutano uliofanyika kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto siku iyo hiyo.

Awali, Bw Odinga alikuwa amesisitiza hakuna lolote ambalo lingesimamisha zoezi la kukusanya saini kutoka kwa wananchi siku ya Alhamisi iliyopita.

Kutokana na matukio hayo, wadadisi wanaeleza ni wazi huenda Rais Kenyatta amegundua kuwa huenda akarudia kosa la refarenda za hapo awali, ikiwa lengo lake ni kuiunganisha nchi.

“Sababu ambapo refarenda ya 2005 haikufaulu ni kuwa lengo lake kuu lilikuwa ‘kumwadhibu’ Bw Odinga na washirika wake katika serikali ya Narc, baada ya mkataba wa kisiasa (MoU) kati yake na Rais Mwai Kibaki (kwa sasa ni Mstaafu) kuvunjika,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Mdadisi anaeleza kuwa badala ya kuiunganisha nchi, zoezi hilo liliwagawanya Wakenya katika sehemu mbili kuu—waliomuunga mkono Rais Kibaki na walioegemea upande wa Bw Odinga.

“Serikali ya Rais Kibaki ilishindwa kwenye zoezi hilo na mrengo wa ‘La’ aliouongoza Bw Odinga. Uhasama uliozuka ndio ulisababisha vita vya baada ya uchaguzi tata wa 2007, ambapo Wakenya 1,300 walipoteza maisha yao,” asema Bw Muga.

Anaeleza kuwa kiundani, refarenda hiyo ilikuwa mvutano wa kisiasa kati ya jamii za Wakikuyu na Waluo, zikiwakilishwa na Mabwana Kibaki na Odinga mtawalia, hivyo haingeungwa mkono na Wakenya wote kwani baadhi ya jamii kubwa zilihisi kutengwa.

Prof Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa, anasema taswira fiche ya ghasia za 2007 ilikuwa muungano wa jamii 41 dhidi ya jamii moja zilizohisi “inajipenda kisiasa.”

Anaeleza mvutano wa jamii hizo tano vile vile ulidhihirika mnamo 2010, baada ya Dkt Ruto kuungana na makanisa kuipinga refarenda hiyo.

“Sababu ya Dkt Ruto kuipinga refarenda hiyo ilikuwa kama ‘adhabu’ kwa Bw Odinga ‘kuwasaliti’ Wakalenjin kwa kutowapa nyadhifa za kutosha kwenye serikali ya muungano kati yake na Rais Kibaki. Hii ni ikizingatiwa jamii hiyo ilimpigia kura kwa wingi alipowania urais 2007 kwa tiketi ya ODM,” akasema Prof Munene.

Kama 2005, anasema mzozo fiche kwenye refarenda ya 2010 ulikuwa kati ya jamii za Wakalenjin na Waluo, zikiwakilishwa na Dkt Ruto na Bw Odinga mtawalia.

Anasema taswira ya 2010 ndiyo inajirudia kwenye mvutano kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga kuihusu BBI, kwani Dkt Ruto anahisi “Wakalenjin wanatengwa na jamii zingine nne.”

“Kijumla, asili ya refarenda hizi zote ni juhudi za jamii tano kubwa kujaribu kung’ang’ania mamlaka ya kisiasa. Hata hivyo, kosa kuu limekuwa uendeshaji wa mazoezi hayo kwa kuonekana kuitenga ama kuipendelea moja kati yazo,” asema Prof Munene.

Asema ili kuepuka makosa hayo, ni lazima Rais Kenyatta, kama kiongozi anayejitayarisha kustaafu, ahakikishe jamii zote zimeshirikishwa ili kuepuka migawanyiko iliyoshuhudiwa 2005 na 2010.