Makala

JAMVI: Ruto alivyoruka mtego wa Raila katika BBI

November 22nd, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto amefanikiwa kukwepa mtego wa kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kuunga mkono mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) bora tu uwepo mdahalo unaohusisha pande zote muhimu.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa hatua ya Dkt Ruto ni pigo kwa Bw Odinga ambaye amekuwa akiashiria kuwa alitaka Naibu wa Rais apinge mpango wa maridhiano.

Bw Odinga amekuwa akipinga mapendekezo yanayotolewa na makundi yanayoonekana kuegemea upande wa Dkt Ruto.

Bw Odinga alipuuzilia mbali mapendekezo ya viongozi wa makanisa baada ya Dkt Ruto kuwaunga mkono.

Kiongozi wa ODM alisema viongozi wa kidini walifaa kuwasilisha maoni yao mbele ya jopokazi la BBI lilipokuwa likikusanya maoni ya Wakenya kote nchini.

Akizungumza alipokutana na madiwani kutoka Kaunti ya Wajir, Jumatatu, Naibu wa Rais alionekana kudokeza namna alivyotibua njama ya viongozi ambao wamekuwa wakiunga mkono BBI.

Kulingana na Dkt Ruto, Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta walitaka apinge ili watumie fursa hiyo kumponda katika uchaguzi mkuu wa 2022 iwapo angepoteza.

“Wanaharakisha kura ya maamuzi sio kwa kuitakia mema nchi hii bali wana njama fiche kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa 2022. Lengo lao ni kuibua makundi mawili; linalounga mkono na linalopinga. Tuketi chini tuafikiane ikiwa kweli tunahitaji kuunganisha nchi hii,” akasema Dkt Ruto.

Akaendelea: “Mtu anayepinga anaambiwa kwenda kuunga mkono upande wa ‘Hapana’ ilhali inawezekana kuafikiana na kujenga Kenya moja iliyoungana.”

Naibu wa Rais alishutumu wanaounga mkono BBI kwa ‘kutenganisha’ Wakenya badala ya kuwaunganisha kupitia BBI.

“Tunajaribu kuondoa tatizo la mgawanyiko nchini. Haiwezekani kutatua tatizo hilo kwa kuandaa kura ya maamuzi ambayo imeacha taifa limegawanyika.

“Kwa nini kura ya maamuzi inaharakishwa? Je, kuna njama fiche kuhusiana na siasa ya 2022?” akauliza Dkt Ruto.

Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa mswada wa BBI hautafanyiwa marekebisho licha ya Rais Kenyatta kusema kuwa mapendekezo yaliyotolewa na makundi mbalimbali yatazingatiwa.

Mkutano wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto Jumatano ulisababisha kusitishwa kwa shughuli ya kukusanya saini kwa ajili ya mswada wa BBI iliyopangiwa kuzinduliwa Alhamisi.

Duru za kuaminika zinasema kuwa suala la BBI ni miongoni mwa ajenda kuu zilizozungumziwa katika mkutano huo wa faragha.

Baada ya mkutano huo, wandani wa Dkt Ruto walisherekea huku wakisema kuwa alifanikiwa kusimamisha ‘rege’, yaani mchakato wa BBI.

Wanablogu wanaoongozwa na aliyekuwa mkurugenzi wa dijitali katika Ikulu ya Rais Denis Itumbi, walijigamba kwamba matakwa yao yamefanikiwa kwa asilimia 75.

Kulingana na wakili Felix Otieno, kuna uwezekano kuwa Bw Odinga alipendelea kuwa upande tofauti na Naibu Rais wakati wa kampeni za kura ya maamuzi.

“Nadhani kuna njama ya kutaka Naibu wa Rais apinge mswada wa BBI ili uwe mwisho wa uhusiano baina yake na Rais Kenyatta. Talaka baina ya Rais Kenyatta itakuwa ni baraka kwa Bw Odinga kwani kuna uwezekano mkubwa wa rais kumuunga mkono iwapo atawania urais 2022,” anasema Bw Otieno.

Bw Mark Bichachi ambaye ni mdadisi wa masuala ya kisiasa anakubaliana na Bw Otieno kuwa kiongozi wa ODM angenufaika zaidi kisiasa iwapo Naibu wa Rais angepinga mswada wa BBI.

“Iwapo Naibu wa Rais na Bw Odinga watakuwa katika pande tofauti wakati wa kura ya maamuzi, wangetumia fursa hiyo kupimana nguvu ya umaarufu katika maeneo ya Mlima Kenya, Pwani na Magharibi. Lakini lingekuwa pigo wa Rais Kenyatta iwapo watu wa Mlima Kenya wangeunga mkono upande wa Dkt Ruto,” anasema.

Bw Bichachi pia anasema kuwa Naibu wa Rais huenda anahofia kutumia fedha nyingi kupinga mswada wa BBI ambazo ameandaa kwa ajili ya kinyang’anyiro cha urais 2022.

Wadadisi pia wanasema kuwa Bw Odinga ambaye hajatangaza rasmi ikiwa atawania urais 2022 au la, anataka kutumia kura ya maamuzi ili kubaini wanasiasa wanaomuunga mkono na wale walio katika upande wa Dkt Ruto.