JAMVI: Ruto anasa ‘samaki’ mkubwa Gavana Mvurya akiingia Hasla

JAMVI: Ruto anasa ‘samaki’ mkubwa Gavana Mvurya akiingia Hasla

Na SIAGO CECE

KAMPENI za Naibu Rais William Ruto maeneo ya Pwani zimeanza kuzaa matunda baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya.

Bw Mvurya, hatimaye amevunja kimya chake kuhusu siasa za urais 2022 na kutangaza anaunga mkono azimio la Dkt Ruto.Gavana huyo ambaye ni mwanachama wa Jubilee, amekuwa akiacha wengi kubahatisha mwelekeo atakaochukua mwaka ujao hasa baada ya Jubilee kupasuka vipande viwili.

Upande mmoja wa Jubilee humuunga mkono Dkt Ruto huku mwingine ukifuata misimamo ya Rais Uhuru Kenyatta. Rais Kenyatta kwa muda mrefu ameashiria ataunga mkono msimamo wa Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, katika uchaguzi ujao.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa Biblia ya Kiduruma, Bw Mvurya alisema Naibu Rais alikuwa ndani ya serikali iliyofanikisha miradi mingi ya maendeleo Kwale, na hivyo basi anastahili kupewa nafasi ya kukamilisha kazi ambazo zimebaki.

‘Sisi tuna kaulimbiu ya ‘Kazi Iendelee’ katika kaunti na kitaifa. Hilo linawezekana tu kutekelezwa na wale ambao tayari wako mamlakani. Kwa hivyo kazi ya Ruto iendelee,’ akasema. Bw Mvurya ambaye anatumikia kipindi chake cha mwisho cha ugavana kikatiba, hutumia kaulimbiu hiyo kumpigia debe naibu wake, Bi Fatuma Achani, ili arithi kiti chake mwaka ujao.

Alitaja miradi kama vile ujenzi wa barabara ya Samburu kuwa miongoni mwa mafanikio ambayo serikali ya Jubilee ilitekeleza.Bi Achani tayari alithibitisha nia yake kutumia Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kuwania ugavana Kwale mwaka ujao.

Ijapokuwa Bw Mvurya hakuwa ametangaza msimamo wake kuhusu siasa za urais 2022 awali, dalili zake kuelekea upande wa Dkt Ruto zilionekana wakati wa uchaguzi mdogo Msambweni mwaka uliopita.Katika uchaguzi huo, Bw Mvurya na Dkt Ruto pamoja na wandani wao waliungana kumpigia debe Bw Feisal Bader, ambaye aliibuka mshindi dhidi ya Bw Omar Boga wa ODM ambaye aliungwa mkono na wanasiasa wa Jubilee wanaoegemea upande wa Rais Kenyatta.

Baadhi ya viongozi wa Pwani humshinikiza Dkt Ruto kumtangaza gavana huyo kama mgombea mwenza wake 2022.Kati ya magavana wote watatu wa kaunti za Pwani ambao wanaondoka, ni Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi ambaye sasa amesalia kutangaza mwelekeo atakaochukua kuhusu kura ya urais 2022.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho angali amesimama wima na Bw Odinga, huku Bw Kingi akisalia kimya kuhusu mgombeaji urais ambaye ataunga mkono kupitia chama kipya cha Pamoja African Alliance (PAA).Gavana wa Taita Taveta, Bw Granton Samboja wa Chama cha Wiper, amekuwa akiegemea upande wa Bw Odinga sawa na mwenzake wa Lamu, Bw Fahim Twaha (Jubilee), na Dhadho Godhana wa Tana River ambaye ni mwanachama wa ODM.

Katika hotuba yake jana Kwale, Dkt Ruto alisisitiza kuwa nia ya kuunda UDA ilikuwa ni kuondoa siasa za kikabila nchini.Kando na hayo, aliibua madai kuwa kuna wanasiasa ambao wameanza kuendea waganga wa nchi jirani ili wasaidiwe kupata ushindi uchaguzini.

‘Ninashukuru kwa jinsi neno la Mungu linatusaidia sisi wanasiasa. Kuna wengine ambao husuguliwa majivu na waganga na wanateseka na wengine wamekufa kwa sababu ya mienendo hiyo. Kwa hivyo nashukuru ninapoona kuna matumaini kwao kuokoka,’ akasema.

Biblia ya Kiduruma ilizinduliwa miezi michache baada ya ile ya Kidigo. Idadi kubwa ya jamii za Wamijikenda wanaotumia lugha hiyo inapatikana Kwale ingawa wengi ni Waislamu.

You can share this post!

Mimba za mapema zapungua

Gavana ataka uchaguzi uahirishwe

T L